Home Mchanganyiko TANZIA:MBUNGE WA JIMBO LA MUHAMBWE ATASHASTA NDITIYE AFARIKI DUNIA

TANZIA:MBUNGE WA JIMBO LA MUHAMBWE ATASHASTA NDITIYE AFARIKI DUNIA

0

Spika wa Bunge, Job Ndugai ametangaza kifo cha aliyekuwa mbunge wa jimbo la Muhambwe, Atashasta Nditiye kilichotokea leo saa 4:00 asubuhi, ikiwa ni muda mfupi baada ya wabunge kuhoji kuhusu taarifa zake.

Kabla ya taarifa ya Ndugai, wabunge waliomba muongozo kwa Naibu Spika Tulia Ackson kutaka waelezwe kuhusu hali yake baada ya kupata taarifa kuwa alifariki kwa ajali ya gari iliyotokea Februari 10, 2021.

Akijibu mwongozo huo, Dk Tulia aliwaeleza wabunge kuwa Spika Ndugai alikuwa anashughulikia suala hilo na angetoa taarifa kuhusu suala hilo baadaye.

Baadaye, Spika Ndugai alithibitisha habari hizo akisema Nditiye alifariki wakati akipatiwa matibabu baada ya ajali ya gari aliyopata juzi eneo la Nanenane Nzuguni mkoani hapa.

Kutokana na kifo hicho, Ndugai ameahirisha shughuli za Bunge hadi kesho Jumamosi wakati itakapotolewa taarifa za taratibu za kuaga mwili na maziko.

Nditiye anakuwa mbunge wa pili kufariki katika Bunge la 12 baada ya Martha Umbulla, aliyekuwa mbunge wa viti maalum (CCM), kufariki hivi karibuni.