Home Mchanganyiko WANANCHI WA KIJIJI CHA SUNGAMILE MSALALA KAHAMA WALILIA MNARA WA MAWASILIANO

WANANCHI WA KIJIJI CHA SUNGAMILE MSALALA KAHAMA WALILIA MNARA WA MAWASILIANO

0
………………………………………………………………………………
Na.Faustine Gimu Galafoni.
Baadhi ya wananchi katika  kijiji cha Sungamile  Halmashauri ya Msalala  Wilayani Kahama Mkoani Shinyanga wameiomba serikali kuwasogezea huduma ya Mawasiliano hususan mnara katika kijiji hicho.
Wakizungumza na mtandao huu   Juma hili kijijini  hapo baadhi ya wananchi walisema mawasiliano ya simu yamekuwa ya kusuasua katika kijiji hicho hali ambayo husababisha kupanda juu ya miti au juu ya barabara ili waweze kuwasiliana.
Nkwabi Ndizu ni mmoja wa wakazi wa Sungamile ambapo alisema chanzo cha mawasiliano ya Simu kusuasua katika eneo hilo ni minara ya simu kuwa mbali ambapo hutegemea minara ya mawasiliano kutoka  mji wa Kagongwa ,Isaka na mnara wa Igusule uliopo Wilaya jirani ya Nzega mkoani Tabora .
“Kwa  kweli suala la mawasiliano katika kijiji hiki limekuwa changamoto kubwa tunapotaka kuwasiliana na ndugu na jamaa  inatulazimu kusimama barabarani kwenye mwinuko hali ambayo inaweza kusababisha ajali kama unavyojua barabara hii ni kubwa yanapita magari mbalimbali ya kwenda nje ya nchi ikiwemo Rwanda,Burundi,Congo DRC,pia wakati mwingine inatulazimu kupanda juu ya miti tunachoomba ni mnara wa mawasiliano utufikie wana Sungamile”alisema.
Naye Lucas Lumwecha alifafanua kuwa chanzo kingine cha Mawasiliano ya simu kusuasua katika kijiji hicho ni kuwa bondeni huku Saida Yagoda akieleza kuwa kutokana na mawasiliano kuwa ya chini panaweza kujitokeza madhara mbalimbali ikiwemo husababisha vifo kwani  pindi panapokuwa na mgonjwa huwezi kupiga simu ili kuokoa maisha.
Masanja Makelemo Mabula ni Kiongozi wa Kitongoji cha Igalula kijiji cha Sungamile Wilayani Kahama Mkoani Shinyanga alisema masuala ya Mawasiliano hususan internet  na kupiga simu ni shida katika kijiji hichoi.
“Wakati mwingine una mgonjwa unatafuta daladala network ni shida haisomi ni kilio kikuu katika eneo letu”alisema.
Castory Gwalila Kilio kikuu kwake ni pale anapojiunga kifurushi lakini mtandao haupatikani mwishowe muda unaisha kutokana na mawasiliano kusuasua .
“Wakati mwingine tunajiunga na vifurushi vinaisha tu maana network haipatikani  na pia tunapokimbilia barabarani kutafuta network kunaweza kusababisha ajali mfano matairi ya magari yanaweza kufyatuka “alisema.
Naye  Shija Mihambo ambaye ni kondakta wa mabasi yaendayo mikoani ambapo alifafanua kuwa pindi anapotafutwa na wateja akiwa katika kijiji hicho simu huwa hazipatikani huku Ismail Mipawa akiomba huduma za mawasiliano  kuboreshwa zaidi.
Marco Itenga ni Afisa Mtendaji wa kijiji cha Sungamile akifanya mahojiano maalum na mtandao huu  alikiri kuwepo kwa changamoto ya Mawasiliano katika kijiji hicho ambapo alisema
“Hata Ofisini kwetu ninapofika katika kijiji hiki huwa inanilazimu kutoka ofisini kutafuta eneo zuri  la mtandao kwa ujumla mawasiliano kwetu ni mwiba na tuna zaidi ya kaya 500 na zaidi ya wakazi 3000 katika kijiji hiki wanahangaika katika suala zima la mawasiliano”alisema.
Kama ilivyo changamoto ya Mawasiliano katika kijiji cha Sungamile Kahama  ,eneo la Mbulu mkoani Manyara nalo linachangamoto kama hiyohiyo Februari 10,2021 Bungeni jijini Dodoma mbunge wa Mbulu vijijini Flatei  Grigory Massay alihoji ni lini Serikali itajengwa minara ya simu  katika kata za  Endahagichen-Ndamilay,Mewadan-Magong   na Endaghadat -Qamtananat  katika jimbo la Mbulu vijijini Mkoani Manyara ambazo hazina mawasiliano.
Akisimama kwa  mara ya kwanza bungeni  tangu ateule kuwa Naibu Waziri wa Wizara mpya ya “Mawasiliano na Teknolojia ya Habari”Kundo Mathew alisema mpaka sasa kata 633  zilikwishapata  huduma ya mawasiliano huku kata  361 ujenzi ukiendea nchi nzima kwa ruzuku ya serikali  na mwezi huu serikali  inatarajia kutangaza zabuni zingine awamu ya 6  kufikisha huduma ya mawasiliano  katika kata 74 zenye vijiji 206 kote nchini .
Hata hivyo,Naibu Waziri Mathew alisema pamoja na jitihada za serikali ,bado kuna takriban  kata 1365 kati ya kata 3956 zilizopo Tanzania bara na Wadi 16  kati ya wadi 111 zilizoko Zanzibar bado zina changamoto ya  upatikanaji huduma ya mawasiliano ambapo serikali kupitia mfuko wa mawasiliano kwa wote [UCSAF] inafanya tathmini  ili vijiji vyote viingizwe katika kutangaza tenda ya  zabuni mwezi huu.