Home Mchanganyiko WANANCHI WATAKIWA KUYATUMIA MABARAZA YA ARDHI KUPATA SULUHU YA MIGOGORO YA ARDHI

WANANCHI WATAKIWA KUYATUMIA MABARAZA YA ARDHI KUPATA SULUHU YA MIGOGORO YA ARDHI

0

Msajili wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba Stela Tulo (kushoto) akimsikiliza malalamiko kutoka kwa mwananchi alipotembelea Banda la Msajili wa Mabaraza wakati wa Maonesho ya Wiki ya Sheria yanayoendelea katika viwanja vya Nyerere Square Dodoma.

Afisa Ardhi Ramadhani Jingu akifafanua jambo kwa mwananchi aliyetembelea Banda la Msajili wa Mabaraza wakati wa Maonesho ya Wiki ya Sheria yanayoendelea katika viwanja vya Nyerere Square Dodoma. Watumishi kutoka Wizara ya Ardhi wakiwa na bango la Mabaraza ya Ardhi wakati wa Maonesho ya Wiki ya Sheria yanayoendelea katika viwanja vya Nyerere Square Dodoma.

***********************************

Na. Hassan Mabuye, Dodoma

Msajili wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba nchini Bibi Stela Tulo amesema kumekuwa na tabia ya baadhi ya wananchi walio na migogoro ya ardhi kutofuata ngazi na taratibu za kupata haki katika migogoro yao ya ardhi na kuacha kutumia vyombo vilivyowekwa kwa mujibu wa sheria jambo linachangia migogoro ya ardhi kutopata suluhu kwa wakati.

Tulo alisema hayo jana tarehe 29 Februari 2021 katika maonesho ya Wiki ya Sheria yanayoendelea kuadhimishwa na vyombo mbalimbali vya sheria, haki na mahakama katika viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma.

Kwa mujibu wa Msajili wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba nchini, vyombo vinavyohusika kisheria kutoa haki katika migogoro ya ardhi ni kuanzia ngazi ya Baraza la Ardhi la Kijiji, Kata, Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya, Mahakama Kuu kitengo cha Ardhi na Mahakama ya Rufaa.

Alisema, iwapo wananchi walio kwenye migogoro ya ardhi watafuata utaratibu wa kutumia vyombo vilivyowekwa kwa mujibu wa sheria wataweza kupata haki zao na wakati huo na kuepuka kupoteza muda mwingi wa kukata rufani kuhusiana na migogoro ya ardhi.

Aidha, Tulo alitumia fursa ya Maonesho ya Wiki ya Sheria yanayoendelea kuwataka wananchi wa jiji la Dodoma na mikoa jirani kujitokeza kwa wingi kwenye maonesho hayo ili kupata elimu kuhusiana na Mabaraza ya Ardhi na hivyo kujua taratibu za kutafuta wakati wa migogoro ya ardhi.

Maadhimisho ya Wiki ya Sheria yanafanyika kitaifa mkoani Dodoma katika viwanja vya Nyerere Square kuanzia Januari 23 hadi januari 29, 2021.