Home Mchanganyiko UVCCM MANYARA KUADHIMISHA KUZALIWA CCM KWA KUSAFISHA VICHUGUU

UVCCM MANYARA KUADHIMISHA KUZALIWA CCM KWA KUSAFISHA VICHUGUU

0
Katibu Hamasa wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana (UVCCM) Mjini Babati Mkoani Manyara, Iddi Sulle akiangalia kichuguu kilichopo kwenye shule ya msingi Darajani, ambapo wameazimia kuviondoa katika kushiriki maadhimisho ya miaka 44 ya kuzaliwa CCM.
Ofisa elimu wa Kata ya Babati Mkoani Manyara, Willy Mayo akikagua kichuguu kilichopo kwenye shule ya msingi Darajani.
…………………………………………………………………………….
Na Mwandishi wetu, Manyara
VIJANA wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi,  (UVCCM) Mkoani Manyara, imejipanga kufanya shughuli za kijamii kwa kuwaondoa mchwa kwenye vichuguu vilivyopo katika baadhi ya majengo ya shule za msingi Maisaka na Darajani na hospitali ya mji wa Babati (Mrara) katika kilele cha maadhimisho ya miaka 44 ya kuzaliwa CCM.
Katibu hamasa wa UVCCM mjini Babati, Iddi Sulle ameyasema hayo wakati akielezea mikakati ya vijana kwenye maadhimisho ya kuzaliwa CCM.
Sulle amesema wao kama vijana wameamua kuwaondoa mchwa hao kwenye vichuguu ambao wamekuwa kero mara kwa mara kwenye majengo hayo ya serikali ambayo yanatumiwa na wanafunzi na wagonjwa.
Amesema maeneo yote ya majengo hayo yamezungukwa na vichuguu ambavyo vinahifadhi mchwa hao waharibifu wa miundombinu ikiwemo milango na mbao za majengo hayo.
Amesema UVCCM kwa kushirikiana na wazazi, walezi, wanafunzi na wananchi kwa ujumla, wameamua kufanya kazi hiyo siku ya maadhimisho hayo ya kuzaliwa CCM.
“Tunawaomba wana CCM wote wa Babati mjini na wilaya jirani hasa Babati Vijijini kushiriki kwa wingi na kwa pamoja ili kusaidiana kulinda miundombinu ya majengo hayo,” amesema Sulle.
“Unaombwa kufika ukiwa na jembe, sururu na beleshi na endapo una kifaa kimoja kati ya hivyo usiache njoo nacho tufanye kazi hii ya kijamii wakati wa maadhimisho ya kuzaliwa CCM,” amesema Sulle.
Amesema wanatarajia kukutana shule ya msingi Darajani, saa 12 asubuhi ya siku ya jumatatu ya Februari mosi mwaka huu, huku wakiwa na vifaa hivyo vya kazi.