Afisa Tarafa Mihambwe Emmanuel Shilatu akizungumza na Mkulima Bi Fadina Hassan pamoja na Mwenyekiti Ngonda Amcos Rashid Lingoni ofisini kwa Afisa Tarafa (hawapo pichani) wakati akitoa maelekezo ya kukamatwa kwao.
Mkulima Bi Fadina Hassan pamoja na Mwenyekiti Ngonda Amcos Rashid Lingoni wakiwa kituo cha Polisi cha wilaya Tandahimba kufuatia agizo la Afisa Tarafa Mihambwe Emmanuel Shilatu aliyeagiza kukamatwa kwa uongozi wa bodi nzima ya Ngonda Amcos
**************************************************
Na Mwandishi wetu Mihambwe
Afisa Tarafa Mihambwe Emmanuel Shilatu ameagiza kukamatwa kwa uongozi wa bodi nzima ya chama cha msingi cha Ngonda kufuatia upotevu wa gunia 10 za Wakulima.
Gavana Shilatu ametoa maelekezo hayo leo Jumatatu Januari 18, 2021 kufuatia lalamiko lililoletwa kwake na Bi Fadina Hassan aliyekuja kulalamika juu ya kutokulipwa kilogram 100 alizopima ghalani tangu Oktoba 23, 2020 ambapo Mwenyekiti wa Ngonda Amcos Rashid Lingoni alikiri kutambua deni hilo mara baada ya kubanwa na Gavana Shilatu juu ya upotevu huo.
“Sijaridhishwa na maelezo ya Mwenyekiti yamejaa ubabaishaji mwingi na kazi yetu Serikali ni kutatua kero za Wananchi wakiwemo Wakulima ambao wanafanya kazi zao na hatutakubali jasho lao lichezewe. Hivyo nimetoa maelekezo viongozi hao wa Amcos wakamatwe mara moja.” Alisema Gavana Shilatu wakati akizungumza na Mwandishi wetu.
Gavana Shilatu amewataka viongozi wa Amcos wenye michezo hiyo michafu waache mara moja na wahakikishe wamewalipa fedha zao Wakulima. Pia amewasihi Wananchi kuendelea kufanya kazi ipasavyo na Serikali inayoongozwa na Rais Magufuli na viongozi wapo tayari wakati wote kulinda maslahi yao ili kila Mtu anufaike na jasho lake.