Home Uncategorized SERIKALI YAWAITA WAWEKEZAJI KATIKA SEKTA YA MAWASILIANO HAPA NCHINI

SERIKALI YAWAITA WAWEKEZAJI KATIKA SEKTA YA MAWASILIANO HAPA NCHINI

0

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt Faustine Ndugulile,akizungumza leo Januari 14,2021 wakati wa kikao kazi na wenyeviti wa bodi na wakuu wa taasisi zilizochini ya Wizara hiyo kilichofanyika jijini Dodoma. 

Katibu Mkuu Wizara ya Mawasiliano na  Teknolojia ya Habari , Dk Zainab Chaula,akieleza jambo leo  Januari 14,2021 wakati wa kikao kazi na wenyeviti wa bodi na wakuu wa taasisi zilizochini ya Wizara hiyo kilichofanyika jijini Dodoma. 

Mtendaji Mkuu UCSAF, Justina Mashiba,akizungumza kwenye kikao kazi na wenyeviti wa bodi na wakuu wa taasisi zilizochini ya Wizara hiyo kilichofanyika leo Januari 14,2021 jijini Dodoma. 

Baadhi ya washiriki wakifatilia kikao kazi na wenyeviti wa bodi na wakuu wa taasisi zilizochini ya Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kilichofanyika leo Januari 14,2021 jijini Dodoma. 

……………………………………………………………………….

Na.Alex Sonna,Dodoma

Serikali imewataka wawekezaji wenye uwezo wa kuwekeza katika sekta ya mawasiliano kuja kuwekeza hapa nchini  katika kipindi hiki ili kuimarisha mawasiliano na kutoa huduma kwa njia ya mtandao hasa katika kipindi hiki nchi imeingia katika uchumi wa kati.

Hayo yamebainishwa Jijini Dodoma na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt Faustine Ndugulile wakati wa kikao kazi na wenyeviti wa bodi na wakuu wa taasisi zilizochini ya Wizara hiyo katika kuweka mikakati ya pamoja kuinua Wizara hiyo Mpya hapa nchini.

Amesema kwa sasa Serikali inauhitaji mkubwa wa kukuza sekta ya mawasiliano katika maeneo yote hivyo wabunifu na wawekezaji wenye uwezo wa kuwekeza katika sekta ya mawasiliano ili kama nchi ijenge uwezo binafsi wa kimtandao (TEHAMA) katika kuendesha shughuli zake.

“Tumejipanga kuimarisha sekta ya mawasiliano kwahiyo muwekezaji yeyote mwenye uwezo wa kujenga kiwanda cha simu au katika sekta nyingine kwenye mawasiliano tunamkaribisha na tutampa kila ushirikiano atakao hitaji” amesema Dkt Ndugulile.

Amesema kama nchi inahitaji mifumo ya kimtandao TEHAMA kwa sababu dunia inapokwenda itahitaji uwekezaji mkubwa na kila shughuli itahamia katika mtandao hivyo kama nchi inatakiwa kuanza maandalizi mapema.

Amesema kama nchi  tayari wameanza maandalizi kuna kiwanda kinajengwa Jijini Mwanza cha kutengeneza simu janja ili zipatikane kwa wingi hapa nchini na kwa bei rahisi kabisa kurahisisha kazi nyingi.

” Tunataka simu janja zipatikane kwa wingi sana hapa nchini tunataka wakulima waliopo vijijini kabisa wawe na simu janja ambapo atakuwa na uwezo kutumia simu hiyo kupata elimu ya kilimo,

akiwa kijijini huko huko akaona ugonjwa au mdudu katika mazao yake akapiga picha na kutuma kwa wataalamu na kupata huduma kwa njia ya mtandao na shida yake ikaisha” amesema.

Aidha amesema kwa sasa biashara za mtandaoni zinafanya vizuri hivyo  Serikali itaendelea kuimarisha huduma za TEHAMA ili kwenda na kasi ya dunia inavyokwenda bila kuathiri udamaduni wa nchi ya Tanzania.

Amesema watashirikiana na Wizara nyingine ili kuhakikisha huduma nyingi zinazotolewa na Serikali zinatolewa kwa njia ya mtandao ili kupunguza foleni katika ofisi za Serikali kwa wananchi kutaka kupata huduma.

Pia ametumia mda huo kuzitaka taasisi zilizochini ya Wizara hiyo kufanya kazi kwa weredi na kuondoa kero nyingi zilizokuwa zikiwapata wananchi katika kupata huduma zitolewazo na taasisi hizo.

Akiongea kwa niaba ya wakuu wa taasisi   Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa wote Justina Mashiba amesema watakwenda kuyafanyia kazi yale yote wanayotakiwa kutekeleza na kufanya kazi kwa bidii.

Amesema kupitia mfuko wa Mawasiliano kwa wote  wamefikisha mawasiliano katika vijiji 3119 na bado vijiji 3900 ambavyo vipo katika hatua mablimbali na vingine vipo katika mpango wa kufikishiwa huduma hiyo.