Home Uncategorized MTATURU AGAWA VIFAA VYA SHULE VYENYE THAMANI YA ZAIDI YA MILIONI 30...

MTATURU AGAWA VIFAA VYA SHULE VYENYE THAMANI YA ZAIDI YA MILIONI 30 JIMBONI KWAKE

0

MBUNGE wa Singida Mashariki, Miraji Mtaturu amegawa vifaa mbalimbali vya shule vyenye thamani ya takribani Sh Milioni 30 kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wapatao 1,165 kutoka katika familia zisizo na uwezo zilizopo jimboni kwake.

Zoezi hilo ni muendelezo wa utaratibu wake aliouanzisha tangu aingie bungeni kwa mara ya kwanza mwaka 2019 ambapo mwaka jana aligawa vifaa vyenye thamani ya Sh Milioni 6.8.

Akizungumza Januari 12,2021 wakati akigawa vifaa hivyo Mtaturu amesema hatua hiyo ni utekelezaji wa ahadi yake ya kuwasaidia wanafunzi katika jimbo hilo ikiwa ni kuunga mkono jitihada za Rais Dkt. John Magufuli za kutoa elimu bure kuanzia shule za msingi hadi sekondari.

“Katika vipaumbele vyangu nilivyovitaja cha kwanza ni elimu na niliahidi kuwa kinara katika hili,na hiki ninachofanya hapa ni muendelezo wake,najua serikali yetu chini ya Rais Dkt Magufuli imefanya mengi katika kuinua sekta ya elimu,nami mbunge pia nina nafasi yangu ya kuunga mkono jitihada hizo,”alisema.

Amesema amegawa sare za shule,madaftari na kalamu ili kwenda sambamba na kauli mbiu yake isemayo ‘ElimuYetu, Maendeleo Yetu’ inayochochea upatikanaji wa elimu kwa wote kama njia ya kuwezesha kupatikana kwa maendeleo.

“Serikali yetu ya awamu ya tano imewekeza kwenye elimu, inatoa elimu bila ya malipo nami kama mbunge wa jimbo hili nimeona niunge mkono jitihada hizo kwa kusaidia sare na vifaa vya shule ili kusiwepo kikwazo na hivyo kuwezesha lengo la serikali kutimia,” alisema Mtaturu.

Pamoja na kugawa vifaa hivyo,pia ameahidi kutoa Sh Milioni moja kwa shule itakayofanya vizuri jimboni humo na kwa mwanafunzi atakayeongoza kwenye darasa la saba na kidato cha nne atamzawadia Sh laki tatu,wa pili Sh laki mbili na watatu Sh laki moja.

“Kwa walimu wa hesabu na kiingereza somo lake likiongoza nitamzawadia Sh laki tatu,afisa elimu kata, kata yake itakayofanya vizuri nitamzawadia Sh laki tatu,na diwani ambaye kata yake itafanya vizuri nitamzawadia Sh laki tano za miradi ya maendeleo,yote hii ni motisha ili kuongeza ufaulu,”alisema.

Amewahimiza wazazi kushirikiana na walimu ili kusaidia watoto kupata elimu bora na kwa kila mzazi atimize wajibu wake.

Kwa upande wake Afisa Elimu Sekondari Wilaya ya Ikungi, Mwalimu Ngwano Ngwano amempongeza na kumshukuru Mtaturu kwa dhamira yake ya kusaidia maendeleo ya wananchi kwenye sekta mbalimbali katika jimbo hilo.

“Unachokifanya sio tu kinawasaidia watoto hawa bali kinasaidia jamii nzima,nakupongeza kwa hatua hii,”alisema afisa elimu huyo.

Akizungumza kwa niaba ya wazazi wengine,mzazi Hawa Chambo ameshukuru mbunge kwa moyo wake wa upendo wa kuwasaidia watoto wanaotoka kwenye familia zisizojiweza.

“Ulichofanya hapa mbunge wetu ni ibada kubwa kwa Mwenyezi Mungu yenye malipo makubwa sana,ni kweli watoto hawa walikosa sare za shule na madaftari huku shule zikiwa zimeshafunguliwa tangu Januari 11 2021,tunasema ahsante Sana,”alishukuru mzazi huyo.