Home Mchanganyiko WAZIRI MKUU AZINDUA SAFARI YA MELI MPYA ZIWA NYASA

WAZIRI MKUU AZINDUA SAFARI YA MELI MPYA ZIWA NYASA

0

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na  wafanyakazi wa Kampuni ya Ujenzi ya Kichina ya CHICO baada ya kukagua ujenzi wa barabara ya Mbinga -Mbamba Bay Mkoani Ruvuma, Januari  5, 2021. Kampuni hiyo imejenga barabara hiyo kwa gharama ya sh.bilioni 129.361. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa meli ya MV Mbeya II baada ya kuzindua meli hiyo kwenye bandari ya Mbamba Bay wilayani Nyasa, Januari 5, 2021. Waliokaa pichani kutoka kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Songoro Marine, Bw. Songoro,  Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya,  Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania, Deusdedit Kakoko,  Mke wa Waziri Mkuu, Mama Mary Majaliwa na kulia ni Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Ruvuma, Odo Mwisho

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipozindua Meli ya MV Mbeya II kweye bandari ya Mbamba Bay wilayani Nyasa, Januari 5, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikata utepe wakati alipozindua Meli ya MV. Mbeya II kwenye Bandari ya Mbamba Bay wilayani Nyasa, Januari 5, 2021. Wengine pichani ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania,Deusdedit Kakoko, Mbunge wa Nyasa Mhandisi Stella Manyanya, Mke wa Waziri Mkuu, Mama Mary Majaliwa, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme, Naibu Waziri wa Ujenzi, Godfrey Kasekenya,Mwenyekiti wa Bodi ya MNamlaka ya Bandari Tanzania, Ignas Rubaratuka na kushoto ni Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Ruvuma, Odo Mwisho. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka Nahodha Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania, Abdullah Mwingamno kuhusu uendeshaji wa Meli ya MV. Mbeya II wakati alipozindua Meli hiyo kwenye Bandari ya Mbamba Bay wilayani Nyasa, Januari 5, 2021.
****************************************************

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezindua rasmi safari ya meli mpya ya MV Mbeya II itakayotoa huduma katika Ziwa Nyasa nchini na nchi jirani za Msumbuji na Malawi.

Meli hiyo yenye thamani ya shilingi bilioni 9.1 ni muendelezo wa Serikali ya Awamu ya Tano wa kuboresha miundombinu ya usafiri na usafirishaji wa mizigo na abiria kwa lengo la kuboresha uchumi.

Amezindua  safari za Meli hiyo leo (Jumanne, Januari 5, 2020) katika Bandari ya Mbamba Bay wilayani Nyasa. Amewataka wananchi waitunze meli hiyo ambayo imejengwa na kampuni ya Kitanzania ya Songoro Mrine.

Waziri Mkuu amesema Tanzania imezungukwa na nchi nane ambazo zinategemea kupata bidhaa mbalimbali kutoka nchini. “Wananchi tumieni fursa ya uwepo wa meli hii kufanya biashara.”

Amesema wananchi hawawezi kupata maendeleo bila ya Serikali kujenga miundombinu kama ya meli, barabara, bandari, hivyo amewataka waitumie vizuri kwa ajili ya kukuza uchumi wao.

“Serikali inajenga vitu kwa maendeleo ya watu na kwa kuzingatia hilo, Serikali imewekeza fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu itakayowanufaisha kiuchumi kama meli.”

Kadhalika, Waziri Mkuu ameagiza kuwe na kanzidata ya mafundi chipukizi wa Kitanzania wanaoshiriki katika ujenzi wa miradi mikubwa ya kimkakati kama meli na madaraja makubwa.

Waziri Mkuu amesema kanzidata hiyo itaiwezesha mafundi hao chipukizi kutambuliwa kwa lengo la kuwaendeleza zaidi na kuwa na ujuzi ili baadaye wapewe miradi ya ujenzi.

Pia, Waziri Mkuu alikagua hali ya ujenzi wa mradi wa barabara ya Mbinga-Mbambabay yenye urefu wa kilomita 66 ambayo ujenzi wake umekamili. Amesema ameridhishwa na ujenzi wake.

“Nimekuja na barabara hii nateleza tu, wakati ule ulikuwa unatembea katika mawe, makorongo lakini sasa unalala tu. Naipongeza kampuni ya CHICO kwa ujenzi wa mradi huu.”

Naye, Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya amesema ujenzi wa barabara hiyo ni kutimiza ndoto za Rais Dkt. John Pombe Magufuli za kuboresha miundombinu.

Amesema kukamilika kwa barabara hiyo pamoja na kuanza kwa safari ya meli  ni ukombozi wa kiuchumi kwa wananchi wa wilaya ya Nyasa na ukanda mzima wa kusini. “Sasa Nyasa imefunguka.”

Mhandisi Kasekenya amesema Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi itahakikisha inasimamia kikamilifu bandari katika kukusanya mapato yake kwa njia ya kielektroniki ili ziweze kujiendesha na kwamba haitamvumilia mtendaji yeyote atakayekwenda tofauti.

Kwa upande wake, Meneja wa Wakala wa Barabara wa Mkoa wa Ruvuma, Mhandisi Alinanuswe Lazeck amesema ujenzi barabara ya Mbinga-Mbamba Bay yenye urefu wa kilomita 66 umegharimu shilingi bilioni 129.361.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania, Deusdedit Kakoko alisema katika ziwa nyasa kuna jumla ya bandari 15 kati yake sita zipo mkoani Ruvuma, sita zipo mkoani Njombe na tatu zipo mkoani Mbeya.

Alisema katika kuboresha usafiri katika Ziwa Nyasa Serikali ilitoa shilingi bilioni 20.1 ambazo zimetumika katika kujenga meli tatu ambazo kati yake mbili ni za mizigo MV Ruvuma na MV Njombe kwa thamani ya shilingi bilioni 11 na meli ya abiria na mizigo ya MV Mbeya ii kwa shilingi bilioni 9.1. Meli ya MV Mbeya ii inauwezo wa kubeba abiria 300 na tani 200 za mizigo.