Home Michezo FAINALI KILIMO CUP DUNG’UNYI WILAYANI IKUNGI SINGIDA ZAFANA

FAINALI KILIMO CUP DUNG’UNYI WILAYANI IKUNGI SINGIDA ZAFANA

0

Mgeni
rasmi wa ‘Kilimo Cup Kata ya Dung’unyi’ na Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward
Mpogolo akikagua Timu ya Dung’unyi FC muda mfupi kabla ya kuanza kwa mchuano wa
fainali kati ya timu hiyo na Damankia FC jana. Dung’unyi FC ilitwaa ubingwa wa michuano
hiyo kwa kuilaza Damankia FC 2-1.

wa
Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo (katikati) akifuatilia fainali hiyo.

Matukio
mbalimbali yakiendelea kabla ya kuanza kwa mchuano huo.

Matukio
mbalimbali yakiendelea kabla ya kuanza kwa mchuano huo.

Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo akikagua Timu ya
Damankia FC muda mfupi kabla ya kuanza kwa mchuano wa fainali kati ya timu hiyo
na Dung’unyi FC.

Picha
ya pamoja ya wachezaji na viongozi wa ngazi mbalimbali ndani ya Wilaya ya
Ikungi , mkoani Singida waliohudhuria kabla ya kuanza kwa fainali hiyo jana.

Mkuu
wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo (wa pili kutoka kushoto) akiwa na baadhi ya
viongozi wa Kata ya Dung’unyi, kushoto ni mwanzilishi wa mashindano hayo ambaye
pia ni Mtendaji wa Kata ya Dung’unyi, Yahaya Njiku, Mjumbe wa Kamati ya Siasa
(CCM)Wilaya ya Ikungi, Salum Chima, na Afisa Kilimo wa Kata ya Dung’unyi Esther
Bayda.

Mgeni
rasmi akikabidhi zawadi ya fedha kwa mshindi wa pili ambaye ni Damankia FC .

Bingwa
wa michuano hiyo Dung’unyi FC wakiondoka na mbuzi wao..

Mtendaji
Kata Dung’unyi, Yahaya Njiku akizungumza. Kulia ni DC Mpogolo akifuatilia
matukio hayo.

Fainali hizo zikiendelea.

Na Dotto Mwaibale, Singida

 

HATIMAYE michuano ya kusisimua ya Kombe la Kilimo ‘Kilimo
Cup’ kata ya Dung’unyi wilaya ya Ikungi yamemalizika jana huku timu ya
Dung’unyi FC ikiibuka mshindi kwa kujinyakulia zawadi ya Mbuzi na fedha taslimu
baada ya kuichapa Damankia FC 2-1 kwenye fainali za mashindano hayo.

Kilimo Cup iliyoasisiwa na Mtendaji wa Kata hiyo Yahaya
Njiku, ni miongoni mwa ligi za mpira wa miguu zilizokuwa na hamasa na mvuto wa aina
yake, zikiambatana na shughuli mbalimbali za uelimishaji jamii kuhusu dhana ya
kilimo bora-lengo hasa ni kuhamasisha vijana na watu wazima kushiriki kikamilifu
katika shughuli za kilimo katika kipindi hiki cha msimu wa mvua.

Awali, kabla ya kufungua fainali hiyo, Mkuu wa Wilaya hiyo,
Edward Mpogolo, aliahidi kuboresha zaidi mashindano hayo kwa siku za usoni, na
kuahidi kupanua wigo kwa kuyafanya kuwa katika ngazi ya wilaya, azma ikiwa ni
kuzidi kutangamanisha wataalamu na jamii katika kuleta ustawi kwenye kilimo na
ufugaji.

“Natamani ligi hii tungeianza mapema zaidi kabla ya msimu wa
kilimo kuanza ili kuongeza tija kwenye kilimo, nafahamu mashindano haya
yamechagiza sana uelewa wa masuala ya kilimo kutoka kwa wataalamu kwenda kwenye
jamii hatua kwa hatua,” alisema Mpogolo.

Aidha, kupitia michuano hiyo, aliagiza Watendaji wa Kata
kuanza mara moja mchakato wa kufufua mchezo wa riadha kwenye maeneo yao na
kuahidi kusimamia ipasavyo, shabaha kubwa ni kutaka kurudisha mchezo huo kwenye
‘pick’ kutokana na huko nyuma kuwa ni kati ya michezo iliyoipa heshima kubwa wilaya
hiyo.

“Naagiza kila Tarafa, shule za Msingi na Sekondari kuwe na
kituo cha mchezo wa riadha…nafahamu Ikungi ni mahiri sana kwenye riadha ni
lazima tujipange kama wilaya kuhakikisha tunafufua mchezo huu na hatimaye hapo
baadaye kuwezesha wachezaji wake kushiriki katika michuano ya kimataifa,”
alisema Mpogolo

Katika hatua nyingine, alihamasisha wana-michezo hao
kuhakikisha wanajiunga kwenye vikundi ili kunufaika na fursa za mikopo ya
halmashauri, sambamba na kuongeza tija ya wingi wa uzalishaji wa mazao ya
kilimo na mifugo iliyopo, ili kukidhi hitaji kubwa la soko lililopo katika jiji
jirani la Dodoma na kwingineko nchini.

Kwa upande wake, mwanzilishi wa mashindano hayo Njiku
alisema mashindano hayo ambayo yalianza Desemba 20 mwaka jana, yalihusisha
vijiji 5 vya kata hiyo Dung’unyi, Damankia, Samanka, Munkinya na Kipumbuiko kwa
minajiri ya kuhamasisha shughuli za maendeleo ndani ya kata hiyo-na hasa
kilimo.

“Kwa wiki nzima mfululizo michuano hii imekwenda sambamba na
utoaji wa elimu kutoka kwa wataalamu wa kilimo juu ya tija ya kilimo, lakini
Jeshi la Polisi nao wamefika na kutoa elimu juu ya masuala mbalimbali
yanayohusu jukumu la raia katika ulinzi wa amani na usalama,” alisema Njiku.

Hata hivyo, Afisa Kilimo wa Kata hiyo, Esther Bayda, alimweleza
Mkuu wa Wilaya kuwa kupitia ligi hiyo wamefanikiwa kuhamasisha vijana
kuzingatia kanuni bora za kilimo, ikiwemo umuhimu wa matumizi ya mbolea na
mbegu bora katika kuinua tija na ustawi.

Bayda kupitia kauli mbiu ya ligi hiyo isemayo ‘kilimo ni
kazi kama zilivyo kazi nyingine’ alisema katika kipindi chote cha ligi hiyo
wamefanikiwa kuwafikia wakulima 50 na kuwafundisha mbinu bora za kilimo cha zao
la mtama kupitia mashamba darasa mawili yaliyopo katika vijiji vya Samanka na
Damankia.

“Bado kuna changamoto ya mwamko mdogo kwa kundi la vijana, hususani
wale wa kati ya miaka 18 na 25 kutojihusisha na shughuli za kilimo, jitihada za
uhamasishaji zinaendelea… na kuanzia jumatatu tutaanza kutoa mafunzo ya kilimo
bora kwa wanakijiji takribani 150 wakiwemo vijana, kupitia mashamba darasa 3
kwa vijiji vya kipumbuiko, Damankia na Munkinya,” alisema Bayda.