Home Mchanganyiko DC CHILUMBA AFANYA UKAGUZI WA UJENZI WA BARABARA YA RAMI WILAYANI NYASA

DC CHILUMBA AFANYA UKAGUZI WA UJENZI WA BARABARA YA RAMI WILAYANI NYASA

0

************************************

Na Muhidin Amri,
Nyasa

MKUU wa wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma Isabela Chilumba, amekagua  maendeleo ya ujenzi wa barabara ya lami kutoka Mbambabay  hadi wilaya ya Mbinga inayojengwa na kampuni ya Chico  kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 103.

Akizungumza baada ya kujionea kazi ya ujenzi  katika eneo la mzunguko, Mkuu wa wilaya ameridhishwa na ujenzi wa barabara hiyo ambayo imejengwa kwa ubora wa hali ya juu kusisitiza kuwa, barabara hiyo ina umuhimu mkubwa kwa wananchi wa Nyasa na Watanzania kwa jumla.

Amesema,  kukamilika kwa barabara  kutasaidia sana wananchi wa Nyasa kusukuma maendeleo na kumaliza kero ya  kusafiri  muda mrefu kutoka Nyasa kwenda maeneo mengine ya mkoa wa Ruvuma.

Alisema, awali ilikuwa shida  kwa wananchi na magari hasa makubwa yanayotakiwa kupeleka bidhaa mbalimbali kushindwa kufika Nyasa kutokana na miundombinu mibovu,lakini  sasa wafanya biashara wa mazao  na bidhaa nyingine watafika wilayani humo kwa urahisi.

Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa wilaya, baada ya Serikali kukamilisha ujenzi huo,jukumu kubwa iliyobaki ni wananchi kujipanga na kufanya kazi kwa bidii kwani hawana sababu tena ya kulilia, badala yake  waitumie barabara  ya lami kama daraja la kujiletea maendeleo.

Aidha, ameishukuru serikali kwa uamuzi wake kujenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami  na wao kama serikalii ya wilaya watahakikisha wanailinda na amewataka wananchi kuiona barabara hiyo kuwa yao, hivyo wanapaswa kuwa walinzi  wa miundombinu yake.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Mbinga Kosmas Nshenye alisema,  barabara hiyo ina manufaa makubwa ya kiuchumi na kijamii kwani wananchi wa Mbinga kwa  sasa wana uhakika wa kusafirisha mazao yao kutoka shambani kwenda sokoni na kusafiri kwenda maeneo mengine kwa ajili ya shughuli mbalimbali.

Alisema, sasa  barabara itaanza kutumika kwa ajili ya matumizi ya rasilimali ambazo hapo mwanzoni hazikutumika vizuri  kutokana na ubovu wa barabara na kutolea mfano makaa ya mawe yanayochimbwa katika wilaya ya Nyasa ambayo yalishindwa kusafirishwa kwenda viwandani kutokana na ubovu wa miundombinu.

Nhenye,ameiomba  jamii kutumia barabara hiyo kama  fursa ya maendeleo na kuwataka wananchi wa Mbinga kutumia barabara hiyo vizuri  na kuepuka  hujumu zozote ambazo zitapelekea kuharibika mapema.

Alisema, barabara ya Mbinga- Mbambabay  yenye urefu wa km 66,  km 50 iko upande wa wilaya ya Mbinga kwa hiyo ni lazima wananchi wa Mbinga wajivunie kuwepo kwa barabara hiyo ambayo inatajwa kuwa na mchango mkubwa wa kiuchumi.

Gaudence Ndomba mkazi wa Mbinga mjini alisema, barabara hiyo ina manufaa makubwa kwa wananchi wa Mbinga kwani itawezesha wananchi hususani wakulima  kusafirisha mazao yao kutoka shambani kwenda kwa walaji.

Ndomba alisema, pia itaboresha baadhi ya huduma muhimu za kijamii kati ya wananchi wa wilaya ya Mbinga,Nyasa na mkoa mzima wa Ruvuma na kuipongeza kampuni ya Chico kwa kukamilisha ujenzi kwa  muda muafaka.

Dereva wa basi  la kampuni ya Furaha Safari linalofanya safari kati ya Mbinga-Mbambabay-Lundo Erasto Mbepera amefurahishwa na  kukamilika kwa ujenzi wa barabara hiyo ambapo alisema, awali walilazimika kutumia kati ya masaa 12 hadi 16 kusafiri kati ya Nyasa  kwenda Mbinga lakini sasa wanatumia saa 1 tu.

Hata hivyo,amewaomba watu wenye uwezo kuongeza magari ambayo yatafanya kazi ya kusafirisha abiria kwani hakuna kipingamizi  kutokana na kukamilika kwa barabara hiyo tofauti na hapo awali.