Home Mchanganyiko BAKWATA MWANZA YAWATAKA WAISLAMU KUACHA KULALAMIKA, WAWEKEZE KWENYE ELIMU YA WATOTO

BAKWATA MWANZA YAWATAKA WAISLAMU KUACHA KULALAMIKA, WAWEKEZE KWENYE ELIMU YA WATOTO

0

*******************************************

NA BALTAZAR MASHAKA, Mwanza

SHEIKH wa Mkoa wa Mwanza, Alhaji Sheikh Hasani Kabeke ametoa rai kwa waumini wa Dini ya Kiislamu kuacha kulalamika wanaonewa na kunyimwa ajira na nyadhifa serikalini badala yake wawekeze kwenye elimu na waone fahari kuwasomesha watoto.
 
Alitoa rai hiyo jana wakati akimkaribisha mgeni rasmi kwenye hafla ya chakula cha pamoja na watoto yatima na wanaoishi kwenye mazingira magumu, kilichoandaliwa na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) mkoani Mwanza, akisema dira ya BAKWATA ni kuwafanya watoto washikamane na elimu, hivyo Waislamu waache kulalamika wanaonewa na kunyimwa ajira serikalini badala yake wawekeze kwenye elimu na waone fahari ya kusomesha watoto.
 
Hivyo aliwaasa wazazi wa Kiislamu wasibague ni mtoto gani asome (apate elimu) kati ya mvulana na msichana, waepuke kuwanyima elimu watoto wa kike kwa sababu ya kuwaandaa kuolewa na kwamba jambo hilo BAKWATA imelikataa ili wasome.

“Leo tunasherehekea mwaka mpya kwa kuwalisha watoto yatima na wanaoishi kwenye mazingira magumu na wajane,lakini kwenye majumba yetu tunaona taabu kuwalea watoto wa wenzetu wakati baada ya dakika moja tutaondoka na tutawaacha watoto wetu yatima,”alisena Sheikh Kabeke.

Aliongeza kuwa katika nyumba ya pepo hataingia mtu zaidi ya aliyecheza na kushiriki na watoto yatima,hivyo matajiri na watu wenye uwezo wawasaidie.

Mgeni rasmi Mbunge wa Nyamagana, Stanslaus Mabula akizungumza kwenye hafla hiyo,alisema jambo hilo linatimiza maandiko ya vitabu vyote vya dini katika kufikisha ujumbe wa malezi na makuzi ya watoto,wakijifunza dini watakuwa na maadili ya ucha Mungu na kuwafanya kuwa bora kwenye jamii na taifa.

“Mtoto akilelewa katika misingi bora ndivyo atakavyokuwa na tunawategemea katika kujenga taifa bora.Bado tuna kazi kubwa kuwatafuta yatima na kuwakusanya na kuhakikisha wanapata elimu baada ya serikali ya awamu ya tano kuanzisha elimu bila malipo kupitia Ilani ya Uchaguzi ya CCM,”alisema.

Mabula alisema, Wilaya na Jimbo la Nyamagana imeshika nafasi ya tatu kitaifa kwenye matokeo ya mtihani wa darasa la saba,hivyo mahitaji ya madarasa ni makubwa kutokana na wingi wa watoto wanaojiunga na kidato cha kwanza.

Kwa upande wake Katibu wa CCM Mkoa wa Mwanza,Julius Peter, akitoa salamu za Chama, alisema tukio la kuwakutanisha watoto yatima na kula nao chakula pamoja ni jambo la thawabu na kuomba mwaka huu 2021 uwe wa amani, upendo na maendeleo.

“Zaidi tuombee nchi yetu amani,tumwombee afya njema, Rais John Magufuli, na Mwenyezi Mungu ampe hekima ya kuliongoza taifa letu kwa weledi,”alisema.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Magu, Salum Kalli,alisema serikali ya awamu ya tano kwa watoto imeweka misingi mizuri ya elimu bila malipo bila kujali ni yatima au la.

“Serikali iko pamoja nanyi, imeweka mifumo mizuri ili watoto wapate haki zao chini ya CCM,tunapoanza mwaka mpya ni sehemu ya kutafakari, hivyo tusiwabague watoto hawa ni taifa la kesho , lazima tuwe nao karibu lakini pia na ninyi watoto msome ili muitumie elimu hiyo kwa maendeleo,”alisema Kalli.

Hafla hiyo iliandaliwa na BAKWATA mkoani Mwanza kwa ajili ya kula chakula cha pamoja na watoto yatima na wanaoishi kwenye mazingira magumu katika kuadhimisha mwaka mpya 2021.