Home Mchanganyiko RC Wangabo awaonesha wananchi njia ya kupata kipato kikubwa kwa nguvu ndogo...

RC Wangabo awaonesha wananchi njia ya kupata kipato kikubwa kwa nguvu ndogo kwa mwaka 2021.

0

Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa David Kilonzo (katikati) akishiriki katika kupanda mti wa parachichi katika eneo la nyumba ya Mkuu wa Mkoa huo ikiwa ni moja ya mipango ya mkoa kuhamasisha wananchi kupanda miti katika maeneo ya nyumba na kuongeza mazao ya kudumu ya biashara. 

Mke wa Mkuu wa Rukwa Veronica Wangabo akishiriki katika kuweka kumbukumbu ya mti wa Mparachichi katika eneo la nyumba ya Mkuu wa Mkoa huo lakini pia kuonesha mfano katika kushiriki kuhamasisha miti ya matunda katika maeneo ya nyumba. 

Mmoja wa Wadau wa Mazingira na Mwenyekiti wa Taasisi ya Rukwa Environmental Youth Organization (REYO) Issa Rubega akishiriki kupanda mti katika eneo la nyumba ya Mkuu wa mkoa huo ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha wananchi kuendelea kupanda miti ya matunda katika maeneo yao. Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (kushoto) akipanda mti wa Mparachichi katika eneo la makazi yake ikiwa ni alama ya kuhamasisha wananchi mkoani humo kuwa na utamaduni wa kupanda miti ya matunda kwenye maeneo yao lakini pia kuongeza mazao ya kudumu ya biashara ndani ya Mkoa. pembeni yake ni Meneja Msitu wa Mbizi Mohamed Kiangi.

***************************************************

Katika kuhakikisha wananchi wa mkoa wa Rukwa wanakuwa na mazao mbadala ya kibiashara ili kuwa na kipato cha uhakika Mkuu wa mkoa huo Mh. Joachim Wangabo ameendelea kuwaonesha wananchi namna ambavyo wanaweza kuwekeza kwa muda mfupi na kupata faida kubwa baada ya miaka mitatu na kuendelea na kuepukana na wasiwasi wa kutegemea zao moja kila mwaka.

Mh. Wangabo amesema kuwa katika kuuanza mwaka huu mpya ni vyema wakulima wakaanza kupanda mazao ya kimkakati ya mkoa ikiwemo Parachichi, Kahawa, Chikichi, na Korosho mazao ambayo vitalu vyake vipo tayari na vingine vikiendelezwa katika halmashauri za mkoa huo ili kuwapa wananchi fursa ya kuwa na mazao ya kudumu yatakayowaongezea kipato.

Aidha ameongeza kuwa watu wengi wamekuwa wabinafsi kutokana na mazao huyo kutokuwa na matokeo ya haraka tofauti na mahindi na maharage na hivyo kutothubutu kupanda kwa kuona hatofaidika nayo lakini badala yake hukaa miaka mingi bila ya kuchukua hatua ya kupanda mazao hayo na matokeo yake kuendelea kuwa masikini.

“Mtu analima zao la chakula mahindi anafanya biashara pia analima na maharage na mpunga halafu akaongeza miti 20 katika eneo dogo anapata milioni tano kwa maramoja, sasa Mungu akupe nini? Lakini mara nyingine watu wanakuwa sio wepesi wa kupanda miti kwasababu wanafikiria sasa huu mti nikiupanda utaninufaisha lini, lakini miaka inakwenda 10,20,30 hana hata mti mmoja, alkini siku zote tukumbuke kila tunachofanya sio unafanya kwa manufaa yako mwenyewe, tunafanya kwa manufaa ya watu wengine,” Alisema.

Mh. Wangabo ameyasema hayo jana tarehe 1.1.2021 wakati alipokuwa akipanda miparachichi 20 katika eneo la nyumba yake katika hafla fupi iliyohudhuriwa na watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa ili kuwahamasisha watumishi hao Pamoja na taasisi za kiserikali kupanda miti ya matunda katika taasisi zao pamoja na kuwa mabalozi kwa wananchi ili Mkoa huo kuwa na utamaduni wa kupanda miti hiyo.

Aidha alitahadharisha kuwa Pamoja na kuwa hatarajii kuendelea kuwepo ndani ya miaka mitatu ijayo ambayo miparachichi hiyo inategemewa kuanza kuzaa lakini hata yeye alikuta miti imepandwa na watangulizi wake katika nyumba hiyo nay eye anapata faida ya kuvuta hewa safi Pamoja jambo ambalo hata hizo faida za miparachichi anawaachia watakaokuja baada yake.

Wakati akielezea faida za kibiashara za parachichi alisema kuwa mparachichi mmoja unatoa parachichi 200 hadi 500 baada ya miaka mitatu na kila parachichi moja huuzwa shilingi 500 hadi 1000 hivyo ukiwa na maparachichi 500 ukizidisha kwa 500 utakuwa na 250,000/= na miti 20 ni saw ana Shilingi milioni 5.

Awali akitoa taarifa fupi ya mpango huo wa kuongeza mazao ya kudumu ya biashara mkoani Rukwa Meneja Wa Msitu wa Mbizi Mohamed Kiangi alisema kuwa hamasa hiyo ya kupanda miti ya matunda ilitolewa na Mkuu wa Mkoa baada ya kuwatembelea katika Msitu wao na hivyo kuwashauri kuanzisha upandaji wa miti ya matunda na kuwapatia wananchi wanaoishi kuzunga msitu huo.

“Miti hii ya matunda ni miti ya muda mfupi, ambapo wananchi wanaweza wakapata manufaa ya vipato na lishe bora kwa muda mfupi na wakati huo huo wakawa wanaendelea kutunza msitu wetu wa mbizi, kwahiyo nitumie fursa hii kumshukuru sana Mkuu wa mkoa ambaye ametushauri na mwaka huu tuna miche takriban 6,000 na akatushauri tuhakikisha tunigawa katika taasisi na watu binafsi, mpaka sasa hivi tumegawa miche 4,000 na tumebakiza miche 2,000,” Alisema.

Katika kipindi kifupi Mh. Wangabo amepanda amepanda miche 203 ya Kahawa katika eneo la nyumba yake Pamoja na miparachichi 20 ambapo mikahawa hiyo inategemewa kuanza kuzaa kuanzia miaka miwili ijayo huku miparachichi ikitegemewa kuanza kuzaa baada ya miaka mitatu ijayo.