Home Mchanganyiko Bodi ya Maziwa kuimarisha masoko ya maziwa na bidhaa zake nchini .

Bodi ya Maziwa kuimarisha masoko ya maziwa na bidhaa zake nchini .

0

****************************************************

Kaimu Msajili wa Bodi ya Maziwa Ndugu, Noely Byamungu amesema kuwa Bodi ya Maziwa imejipanga kuimarisha masoko ya maziwa na bidhaa zake ili kuongeza usindikaji wa Maziwa unaofanywa chini ya kiwango na viwanda vya maziwa nchini.

Hayo amesema leo (29.12.2020) jijini Dar es Salaam wakati alipotembelea kiwanda cha Maziwa cha Milkcom Dairies kilichopo Kigamboni jijini Dar es salaam kwa lengo la kuangalia namna bora ya ushirikishwaji wa wasindikaji maziwa katika mpango wa majaribio wa Programu ya Unywaji Maziwa Shuleni pamoja na unywaji wa maziwa katika ofisi za serikali.

Kiwanda cha Milkcom kinasindika takribani lita 20,000 tu za maziwa chini ya uwezo wa kiwanda uliosimikwa wa kusindika lita takribani 100,000 kwa siku.

Ndugu Bymungu, amesema kuwa Bodi ya Maziwa ipo katika hatua za mwisho za utekelezaji wa Mpango wa majaribio wa Programu ya Unywaji Maziwa shuleni utakaoanza hivi karibuni katika mikoa mbalimbali nchini utakaoimarisha masoko ya maziwa kwa wenye viwanda.

Ndugu Byamungu amesema kuwa mpango huo utasaidia viwanda kupata masoko ya maziwa kwa wingi lakini pia kuimarisha afya ya mwili na akili za watoto pindi wawapo darasani na hivyo kuongeza ufaulu wa wanafunzi.

Sanjari na hilo, Ndugu Byamungu amesema kuwa Bodi ya Maziwa itahakikisha ofisi za serikali zinakuwa wanunuzi wa kubwa wa maziwa kwa kutumia maziwa yanayozalishwa ndani ya nchini ili kuongeza unywaji wa maziwa nchini ambapo kwa sasa wastani wa unywaji maziwa kwa mtu kwa mwaka ni lita 54.7 tu ukilinganisha na lita 200 zinazopendekezwa na WHO pamoja na FAO.

Byamungu amesema kuwa ongezeko la unywaji wa maziwa litasaidia kuimarisha kipato cha mfugaji na kuimarisha uchumi wa viwanda vya ndani.

Nae Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Milkcom Ndugu Abubakar Faraji, amesema usindikaji huo mdogo umesababishwa na miundo mbinu mibovu ya uzalishaji maziwa ikiwemo Barabara pamoja na umeme vinavyosababisha kiwanda kusindika maziwa chini ya uwezo wake.

Bw. Faraji amesema kukatika kwa umeme mara kwa mara na kwa muda mrefu kunaisababishia kampuni hasara kwani kampuni hulazimika kutumia genereta katika usindikaji wa maziwa ili kuepuka hasara ya maziwa kuharibika.

“Kutokana na changamoto hiyo, kampuni imejikuta ikitumia gharama kubwa za uendeshaji wa biashara ya maziwa kuliko ilivyotarajiwa na hivyo kusindika chini ya uwezo wake” Alisema

Hivyo, Bw. Faraji ameitaka Bodi ya Maziwa kuja na mikakati itakayosaidia wasindikaji kupata masoko ya maziwa ili kuweza kuzalisha maziwa kwa wingi ikiwemo kutoa hamasa kwa wananchi kupitia vyombo vya habari juu ya umuhimu wa maziwa na hatimaye kuongeza unywaji wa maziwa na bidhaa zake nchini.