Mhe. Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Isdor Mpango (MB) akizungumza na Wakuu wa Taasisi za Serikali na Mashirika ya Umma (hawapo pichani) kwenye kikao kazi kilichofanyika katika ukumbi wa Kambarage uliopo Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dodoma.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mwanaidi Ali Khamis (MB), akitoa hotuba fupi wakati wa kikao kazi cha Wakuu wa Taasisi za Serikali na Mashirika ya Umma kilichoitishwa na Mhe. Waziri wa Fedha na Mipango Jijini Dodoma ambapo amewataka watendaji hao kujiepusha na vitendo vya rushwa na ubadhirifu wa mali za umma.
Baadhi ya Wakuu wa Taasisi za Serikali na Mashirika ya Umma wakifuatilia hotuba ya Mhe. Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt Philip Mpango (MB) wakati alipokutana na Wakuu hao katika kikao kazi kilichofanyika katika ukumbi wa Kambarage uliopo Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dodoma.
Msajili wa Hazina, Bw. Athumani Mbuttuka akizungumza na Wakuu wa Taasisi za Serikali na Mashirika ya Umma (hawapo pichani) kwenye kikao kazi kati ya Wakuu hao na Mhe. Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Isdor Mpango (MB), kilichofanyika katika ukumbi wa Kambarage uliopo Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dodoma.
Viongozi wa Taasisi za Serikali na Mashirika ya Umma wakiwa katika kikao kazi kilichoitishwa na Mhe.Waziri wa Fedha, Dkt. Philip Isdor Mpango (MB) katika ukumbi wa Kambarage uliopo Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dodoma.
Meza Kuu ikiongozwa na Mhe. Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Isdor Mpango (MB) wa pili kushoto, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mwanaidi Ali Khamis (wa kwanza kushoto), Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Adolph Ndunguru (wa pili kulia) na Msajili wa Hazina Bw. Athumani Mbuttuka (kulia)) wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wakuu wa Taasisi za Serikali na Mashirika ya Umma mara baada ya kikao kazi kilichofanyika ukumbi wa Kambarage Jijini Dodoma.
Viongozi wa Taasisi za Serikali na Wizara ya Fedha na Mipango kutoka kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Kilimo Tanzania, Bw. Japhet Justine, Julieth Magambo Kamishna Msaidizi wa Idara ya Mipango ya Kitaifa Wizara ya Fedha na Mipango na Kamishna Msaidizi wa Idara ya Bajeti ya Serikali Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Meshack Anyingisye, wakifuatilia hotuba ya Mhe. Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Isdor Mpango (MB) wakati wa kikao kazi katika ukumbi wa Kambarage uliopo Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dodoma.
Baadhi ya Wakuu wa Taasisi za Serikali na Mashirika ya Umma wakifuatilia hotuba ya Mhe. Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Philip Isdor Mpango (MB) wakati alipokutana na Wakuu hao katika kikao kazi kilichofanyika katika ukumbi wa Kambarage uliopo Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Philip Isdor Mpango (MB) akisalimiana na Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Dkt. Yamungu Kayandabila mara baada ya kikao kazi kilichofanyika katika ukumbi wa Kambarage Jijini Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (MB) akifurahia jambo na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Dkt. Allan Kijazi, mara baada ya Kikao kazi kilichofanyika katika ukumbi wa Kambarage jijini Dodoma.
(Picha na Ramadhani Kissimba-WFM-Dodoma)
************************************************
Na Benny Mwaipaja, Dodoma
Waziri wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), ametoa muda wa siku 9 kuanzia 22 hadi 31 Desemba 2020 kwa Wakuu wa Taasisi na Mashirika ya Umma kujieleza kwa maandishi sababu zilizozifanya taasisi zao kuchangia mfuko mkuu wa Serikali chini ya kiwango, kutochangia huduma za jamii pamoja na kutozingatia ukomo wa matumizi ya asilimia 60 ya mapato ghafi ya taasisi na mashirika yao kwa mujibu wa Sheria
Dkt. Mpango ametoa maagizo hayo Jijini Dodoma alipokutana na Wakuu wa Taasisi za Serikali na Mashirika ya Umma 236 kutoka nchi nzima ikiwa ni mwendelezo wa mikutano yake ya kikazi na taasisi mbalimbali za Serikali ili kutoa mwelekeo mpya wa utendaji wa taasisi hizo hususan kuimarisha na kuongeza mapato ya Serikali.
“Michango kutoka kwa Taasisi na Mashirika ya Umma kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali bado hauridhishi. Kwa mwaka 2019/20, mchango wa Taasisi na Mashirika ya Umma katika pato la Taifa ulikua chini ya asilimia moja (1%), kiwango hiki ni kidogo sana ikilinganishwa na uwekezaji wa Serikali katika Taasisi na Mashirika haya” Alisema Dkt. Mpango
Alimwagiza Msajili wa Hazina Bw. Athumani Mbuttuka kuhakikisha taarifa hiyo ya maandishi kutoka kwa wakuu hao wa Taasisi inamfikia tarehe 31 Desemba 2020 na kutangaza kufuta likizo za sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya kwa Viongozi hao ili watekeleze maelekezo yake.
Alifafanua kuwa Kifungu cha 47 cha Sheria ya Fedha ya Mwaka 2015 na kifungu cha 8 cha Sheria ya Msajili wa Hazina Sura 370 iliyorekebishwa mwaka 2015, kinazitaka Taasisi na Mashirika ya Umma kuchangia asilimia 15 ya mapato ghafi kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali lakini bado kuna Taasisi ambazo zinachangia chini ya kiwango kilichowekwa kisheria na zipo Taasisi na Mashirika hata mchango kwa jamii (CSR) hawatoi kabisa!
Dkt. Mpango alisema kuwa Kifungu cha 46 (1) cha Sheria ya Fedha ya Mwaka 2015 na Kifungu cha 10A cha Sheria ya Msajili wa Hazina iliyorekebishwa mwaka 2015, kinaweka ukomo wa gharama za uendeshaji kwa Taasisi na Mashirika ya Umma yasiyo ya kibiashara kutozidi asilimia 60 ya mapato ya ghafi lakini bado kuna Taasisi na Mashirika ya Umma zinavunja sheria hiyo.
“Kifungu 46 (2) cha Sheria ya Fedha ya Mwaka 2015 kinaelekeza Taasisi na Mashirika ya Umma kuwasilisha asilimia sabini (70) ya ziada kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali baada ya kuondoa gharama za mishahara na kuzingatia ukomo wa matumizi ya uendeshaji uliotajwa kwenye aya 2.1(b) lakini yapo mashirika na Taasisi hayatekelezi matakwa haya” alisisitiza Dkt. Mpango
Aliwaagiza wakuu hao wa Taasisi kuhakikisha kuwa wanapunguza matumizi yasiyo na tija na yasiyo ya lazima ikiwemo misafara mikubwa ya watendaji na wajumbe wa bodi kutembelea miradi ili kuziwezesha taasisi zao kuwa na fedha za kuchangia kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali kwa ajili ya kugharamia miradi mikubwa ya kijamii na ya kimkakati inayotekelezwa nchini.
“Serikali chini ya uongozi shupavu wa Mhe. Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, inaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya kielelezo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), mradi wa umeme (MW 2115) Mto Rufiji, uboreshaji wa usafiri wa anga na majini, ujenzi wa barabara na madaraja makubwa, Elimu bila ada, usambazaji wa umeme vijiji vyote nchini, na uboreshaji wa huduma za afya na maji” Alifafanua Dkt. Mpango
Alisema Idara zote zinazokusanya maduhuli, na Halmashauri zote lazima zifanye jitihada kubwa zaidi kuongeza ukusanyaji wa mapato ya kodi na yasiyo ya kodi ili kuwezesha kutekeleza miradi hiyo kwa kutumia fedha za ndani kwa kiwango kikubwa na kwamba mambo hayo yatafanikiwa endapo watendaji hao wataacha kufanyakazi kwa mazoea.
Aidha, Dkt. Mpango alimpongeza Msajili wa Hazina Bw. Athumani Mbuttuka kwa Kusimamia na kuwezesha urejeshwaji wa mali za Serikali, kupitia Kamati Maalum ya Uhakiki wa Mali za Serikali, ambazo zilikuwa zinamilikiwa na watu binafsi bila kufuata sheria na taratibu.
“Hadi kufikia tarehe 30 Juni, 2020, jumla ya mali zisizohamishika 1,562 zilibainika kushikiliwa au kumilikiwa kinyume cha sheria kwenye mikoa 19 kati ya 26 iliyohakikiwa. Mali hizo zinajumuisha nyumba/majengo (862), viwanja (559), mashamba (43), kampuni (2) na maghala (96)” Alifafanua Dkt. Mpango
Alisema mali hizo za Serikali zilikuwa zinamilikiwa na baadhi ya watu wasio waaminifu bila kuwa na hofu na kwamba zoezi la kutambua na kurejesha mali za Serikali zilizoko kwenye mikono isiyohusika ni endelevu.
Aliipongeza pia Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa kufanya kazi nzuri ya kusimamia Taasisi na Mashirika ambayo ilisababisha kuongezeka kwa ukusanyaji wa mapato ya Serikali kutoka shilingi bilioni 161 mwaka 2014/15 hadi kufikia shilingi bilioni 983 mwaka 2019/20, ikiwa ni ongezeko la asilimia 510.
Dkt. Mpango aliziagiza Taasisi zote za umma zihakikishe zinajiunga na mifumo ya kukusanya mapato ya Serikali (GePG), mfumo wa matumizi ya fedha za Serikali (MUSE) pamoja na mifumo mingine ya uandaaji na usimamizi wa bajeti ili kuongeza ufanisi na madhibiti matumizi yasiyosahihi ya fedha za Serikali.
Naye Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Bi. Mwaidi Alis Khamis aliwataka watendaji hao kujiepusha na vitendo vya ukiukaji wa maadili ikiwemo rushwa na matumizi mabaya ya Serikali na kuonya kuwa yeye na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango hawatavumilia vitendo hivyo.
Alisema kuwa Serikali inamatarajio makubwa na viongozi hao ili kuhakikisha kuwa wananchi masikini wanaondokana na hali hiyo kwa kuboresha maisha yao na kwamba mambo hayo yatawezekana kutokana na utendaji kazi wao mzuri ikiwemo kukusanya ipasavyo mapato ya Serikali.
Kwa upande wake Msajili wa Hazina Bw. Athumani Mbuttuka, alimhakikishia Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango kwamba maelekezo aliyoyatoa yatafanyiwa kazi na kuwaagiza wakuu hao wa Taasisi kusimamia ipasavyo maelekezo hayo.