Home Makala UPANGAJI MBOGA NA MATUNDA CHINI UNAVYOCHOCHEA MAGONJWA YA MLIPUKO JIJI LA DODOMA.

UPANGAJI MBOGA NA MATUNDA CHINI UNAVYOCHOCHEA MAGONJWA YA MLIPUKO JIJI LA DODOMA.

0

Mfanyabiashara wa mbogamboga na matunda wa soko Kuu la Majengo jijini Dodoma wakiwa wamepanga bidhaa zao kwa ajili ya kuuza  katika mazingira hatari kwa mlaji pamoja na afya zao.

Wateja wakiwa wananunua matunda katika soko  Kuu la Majengo lililopo jijini Dodoma ambapo biashara hizo zikiuzwa  katika mazingira hatari kwa mlaji pamoja na  afya za wauzaji zao.

Mfanyabiashara wa mbogamboga katika soko Kuu la Majengo lililopo jijini Dodoma akiwa amepanga bidhaa zao kwa ajili ya kuuza  katika mazingira hatari kwa mlaji .

………………………………………………………………………….

Na Alex Sonna, Dodoma

KIPINDUPINDU ni miongoni mwa magonjwa ya mlipuko ambayo hujitokeza mara kwa mara katika Jiji la Dodoma.

Ugonjwa huu husababishwa na kutozingatiwa kwa kanuni za usafi wa mazingira na hujitokeza hasa kipindi cha masika ambacho huambatana na msimu wa matunda.

Fullshangweblog hivi karibuni ilitembelea masoko mbalimbali ya Jiji hilo ikiwemo la Majengo  na kubaini licha ya kuwepo na mazingira yasiyo safi baadhi ya maeneo ya wafanyabiashara katika msimu huu wa mvua lakini bado wanapanga bidhaa zao hasa za matunda na mboga chini.

Soko hilo ambalo linatumiwa kwa kiasi kikubwa na wafanyabiashara wa mboga na matunda baadhi yao wamekuwa wakipanga bidhaa chini bila kuzingatia kanuni za usafi kwenye eneo la biashara.

 

Kauli za wananchi

Mkazi wa Kisasa Jijini hapa, hadija Hassan anasema katika msimu wa mvua zilizoanza mwishoni mwa Novemba 2020 hadi sasa ni kipindi ambacho wafanyabaishara wanapaswa kuzingatia kanuni za usafi ili kujiepusha na kuchochea magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu.

“Kipindupindu ni ugonjwa unaotokana na uchafu, sasa wafanyabiashara wa Majengo hapa mboga zimepangwa chini na matunda hii inahatarisha afya ya mlaji kwanini wasiwe wabunifu kwa kuwa na meza ndogo za kupanga bidhaa zao,”anasema.

Anaeleza kuwa wafanyabaishara wa soko hilo kwa kiasi kikubwa wanahudumia wakazi wa Dodoma 

“Hii inawaweka hatarini wengine wanapanga bidhaa jirani na mitaro, hata kama ni kitambulisho cha mjasiriamali basi tuangalie maeneo ya kufanyia biashara yaliyorafiki kwa wateja wetu ili kusiwe sehemu ya kuchochea kipindupindu,”anasema.

Naye, Sule Mlondolwa anasema magonjwa ya mlipuko ni magonjwa yanayoenea kwa kasi zaidi kwa jamii.

KAULI YA OFISA AFYA

Akizungumzia kuhusu hali hiyo, Ofisa Afya wa Jiji la Dodoma, Abdallah Mahia, anasema kuna changamoto kubwa kwa wafanyabiashara wa matunda na mboga kutozingatia kanuni za usafi.

Anasema Jiji limekuwa likitoa elimu mara kwa mara kuwataka wafanyabiashara kufanya biashara zao kwa kuzingatia sheria na kanuni za afya ili kujiepusha na magonjwa ya mlipuko.

“Ikumbukwe kuwa wale wanaofanya biashara kwa kuweka chini siyo wa kudumu ndani ya soko bali ni wakulima ambao wanaleta mboga zao kuja kuuza,wafanyabiashara tulinde afya za walaji,”anasema.

OFISA MASOKO

Ofisa Masoko wa Jiji hilo, James Yuna, anawataka wafanyabaishara hao kuacha kupanga bidhaa chini ili kuwaepusha walaji na magonjwa ya milipuko.

Akikagua hali ya usafi wa masoko jijini humo, Yuna anasema wafanyabiashara wanapaswa kupanga bidhaa zao kwenye meza na kuzingatia usafi hasa kipindi hiki cha mvua ili kujiepusha na magonjwa hayo.

“Jiji la Dodoma linatamani kuona wafanyabiashara wote wanakuwa salama pamoja na wateja wanaowahudumia,hivyo mvua ambazo zimeanza kunyesha zisiwe kikwazo kwenu cha kutofanya kazi zenu kwa uhuru,”anasema.

Anawaasa kuwa waangalifu katika kipindi hiki ambacho tayari mvua zimeanza kunyesha.

“Tuonyeshe ushirikiano wa kufanya biashara zetu sehemu zilizo salama kwa ajili yetu na hata kwa wateja wetu badala ya kuzipanga sehemu zisizo salama tupange kwenye meza,”anasisitiza.

Kadhalika, anawataka wafanyabiashara hao kutoa ushirikiano na Halmashauri ya Jiji kwa kufanya wa usafi wa mazingira ili maeneo yaliyopo yaendelee kuwa kwenye hali ya mazuri.

“Pamoja kuna kampuni mbalimbali zinazofanya usafi lakini na nyinyi muwe sehemu ya kuhakikisha pia jiji linakuwa kwenye mazingira mazuri mkizingatia kuwa hata nyinyi ni wazalishaji wa taka kupitia bidhaa mbalimbali mnazouza kwenye maeneo yenu,”anasema.

Anawataka wafanyabiashara kufuata maelekezo, kanuni na sheria zilizotolewa na Halmashauri hiyo ili kujiepusha kufanya biashara kwenye maeneo hatarishi kwao.

Anasema kuwa mpango wa Jiji ni kuona wafanyabiashara ndogo wote wanafanya biashara zao bila kubugudhiwa.

KAULI YA SERIKALI

Mganga Mkuu wa Serikali Prof.Abel Makubi, anatoa tahadhari kwa wananchi dhidi ya magonjwa ya mlipuko na kuwataka kuzingatia suala la usafi kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha nchini.

Anasema kutokana na mvua zinazonyesha kwasasa ni wazi kuna uwezekano mkubwa wa kuibuka kw magonjwa kama kuhara ikiwemo kipindupindu, kuhara damu na yale yanayoenezwa na mbu ikiwemo ugonjwa wa malaria na dengue endapo wananchi wasipozingatia kanuni za afya na kuchukua tahadhari mapema.

Anashauri wananchi kuepuka kula chakula kilichopoa au kuandaliwa katika mazingira yasiyo safi na salama.

Prof.Makubi anasema kutokana na jitihada zinazofanywa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto hadi sasa hakujaripotiwa mlipuko wa ugonjwa kipindupindu kwa kipindi cha mwaka mmoja na nusu hadi sasa.