Home Mchanganyiko DK.CHAULA:SERIKALI IMEJIPANGA KUFIKISHA HUDUMA YA TEHAMA KATIKA SHULE ZA UMMA

DK.CHAULA:SERIKALI IMEJIPANGA KUFIKISHA HUDUMA YA TEHAMA KATIKA SHULE ZA UMMA

0

Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano), Dk Zainab Chaula akizungumza wakati wa kufunga mafunzo ya TEHAMA kwa walimu wa shule za msingi na sekondari jijini Dodoma.

Mtendaji Mkuu UCSAF, Justina Mashiba,akizungumza wakati wa kufunga mafunzo ya TEHAMA kwa walimu wa shule za msingi na sekondari jijini Dodoma.

Baadhi wa walimu kutoka shule za msingi na sekondari kutoka Tanzania Bara na Visiwani wakimskiliza Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano), Dk Zainab Chaula (hayupo pichani) wakati wa kufunga mafunzo ya TEHAMA kwa walimu hao jijini Dodoma

Mkurugenzi wa Elimu Msingi TAMISEMI, Suzan Nusu,akizungumza wakati wa kufunga mafunzo ya TEHAMA kwa walimu wa shule za msingi na sekondari jijini Dodoma.

Mwalimu kutoka shule ya Sekondari Maswa,akitoa neno la shukrani wakati wa kufunga mafunzo ya TEHAMA kwa walimu wa shule za msingi na sekondari jijini Dodoma.

Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano), Dk Zainab Chaula akiwakabidhi baadhi ya  walimu waliohitimu mafunzo ya TEHAMA kwa walimu wa shule za msingi na sekondari jijini Dodoma.

Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano), Dk Zainab Chaula akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kufunga mafunzo ya TEHAMA kwa walimu wa shule za msingi na sekondari jijini Dodoma.

……………………………………………………………..

Na.Alex Sonna,Dodoma

KATIBU Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano sekta ya Mawasiliano, Dk Zainab Chaula amewataka walimu nchini kutokata tamaa ya ufundishaji na badala yake waifanye kazi hiyo kwa moyo mkunjufu huku wakijua wao ni zaidi ya walezi, wazazi wanapokuwa na wanafunzi mashuleni.

Kauli hiyo ameitoa jijini Dodoma wakati akifunga mafunzo ya Tehama kwa walimu 297 kutoka mikoa yote Nchi nzima ambayo yalitolewa na Taasisi ya Mfuko wa Mawasiliano kwa wote ambapo amesema kwa dunia ilipofikia tehama haiepukiki katika kila eneo la utendaji kazi.

Dk Chaula amewataka walimu hao kutumia mafunzo hayo ya wiki moja waliyoyapata katika kuboresha maisha yao, taaluma zao na kuwa msaada kwa watoto wanaowafundisha huko mashuleni lengo likiwa kuzalisha kizazi chenye uelewa wa tehama.

” Zamani watu tulikua tunamaliza darasa la saba au hata kidato cha sita na hatujui hata kuwasha Kompyuta, sasa hivi serikali inatoa mafunzo kwenu walimu ambayo siyo tu yatawasaidia nyie peke yenu bali yanaenda kuwa msaada kwa wale wanafunzi mliowaacha mashuleni mwenu.

Ombi langu kwenu nendeni mkawape na wengine haya mliyojifunza kwa siku tano hapa, kuna walimu wenzenu hawajapata bahati ya kupata mafunzo haya kwa sababu tusingeweza kuchukua wote lakini kupitia nyinyi na wao wakafaidike, kupitia nyinyi pia wanafunzi wetu wakapate uelewa wa tehama pia,” Amesema Dk Chaula.

Dk Chaula amewapongeza walimu hao kwa kumaliza mafunzo hayo salama huku akiwapa changamoto Mfuko wa Mawasiliano kwa wote kuhakikisha awamu ijayo wanafikia kundi kubwa la walimu nchi nzima kwani kwa kasi ya Rais Dk John Magufuli ya kuifanya Tanzania kuwa Nchi ya viwanda ni wazi kila sekta inahitajika kuwa na uelewa wa tehama.

Naye Afisa  Mtendaji Mkuu UCSAF, Justina Mashiba amesema kuwa mfuko huo umekuwa ukipeleka vifaa vya TEHAMA katika shule za umma pamoja na kutoa mafunzo kwa walimu ili kurudisha heshima katika shule hizo.

Bi.Mashiba amesema kuwa tangu UCSAF ianze kutoa mafunzo hayo mwaka 2016, jumla ya walimu 2,213 wa shule za msingi na sekondari wamepata mafunzo hayo ili kuwajengea uwezo wa kutumia vifaa vya TEHAMA na kufundishia.

Hata hivyo ameongeza kuwa, UCSAF inaendelea kujipanga kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ili kuendelea kuinua matumizi ya TEHAMA nchini hususani kwa kuwezesha shule za umma.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Elimu Msingi TAMISEMI, Suzan Nusu amesema kuwa walimu waliohudhuria mafunzo hayo walikuwa na vigezo na Wizara itahakikisha mafunzo yaliyotolewa yanatekelezwa kwa vitendo ili kutimiza lengo lililokusudiwa.

Mafunzo hayo yamefanyika katika Chuo cha Dodoma yakishirikisha walimu 297 ambapo kati yao asilimia 73 wakiwa walimu wanaume na asilimia 15 wakiwa walimu wanawake.