Home Mchanganyiko SEKTA YA MISITU KUKUZA UCHUMI,MAENDELEO

SEKTA YA MISITU KUKUZA UCHUMI,MAENDELEO

0
Naibu Kamishna wa Uhifadhi TFS Mohamed KIlongo akifuatilia kwa umakini uuzaji wa vitalu vya misaji katika mnada wa Shamba la Miti Mtibwa Morogoro
Kaimu meneja shamba la miti Longuza Elinema Mwasalanga kushuto akiteta jambo na Mbunge wa Muheza Mhe. Hamisi Mwinyijuma
………………………………………………………………..
SULEIMAN MSUYA
SERIKALI imeanza kuweka mazingira mazuri yatakayowezesha sekta ya misitu kuchangia kikamilifu katika ukuaji wa uchumi; kuwaongezea wananchi kipato na kuzalisha ajira. 
Hayo yamebainishwa na Naibu Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Uhuduma za Misitu (TFS) Mohamed Kilongo mara baada ya kumalizika kwa mnada wa miti ya Misaji uliofanyika hivi karibuni katika Shamba la Miti Mtibwa wilayani Mvomero mkoani Morogoro na Longuza wilayani Muheza mkoani Tanga.
Naibu Kamishna Kilongo amesema hatua hiyo inalenga kuimarisha utekelezaji wa Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji nchini ili shughuli za uchumi na biashara ziongezeke na kuzalisha ajira.
Amesema hii ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na agizo la Rais John Magufuli la kujenga uwezo wa ndani wa wafanyabiashara kuvuna na kuchakata rasilimali misitu.
“Serikali ya miaka ya nyuma ilianzisha mashamba makubwa ya mitiki ili kuepukana matumizi makubwa ya mbao ngumu za miti ya asili, misaji ina ubora sawa na mbao za mninga na mkongo.
TFS ina mashamba makubwa ya miti ya misaji ambayo kwa mwaka inatoa zaidi ya mita za ujazo 20,000 na tumeanza kuhamasisha watu watumie mbao za misaji lakini pia kuhakikisha mbao za misaji zinaingia kwenye mlolongo wa Serikali na kutambulika kama ilivyo kwa mkongo na mninga,“ amesema Naibu Kamishna Kilongo.
Mwenyekiti wa mnada huo, Afisa Misitu wa Wizara ya Maliasili na Utaliii, Seleboni Mushi anasema mnada waliouendesha ulikuwa tofauti kutokana makundi tofauti kujitokeza kununua malighafi ya misaji.
“Katika mnada wa huu tumekuwa na makundi matatu kutoka kampuni 13 za wanunuzi jambo ambalo si la kawaida, kulikuwa na kundi la wale anaopeleka nje ya nchi, watu binafsi wenye kipato cha kati wanaopasua mbao na kuzipeleka sokoni lakini pia wenye kupata kandarasi mbalimbali za serikali, na watengeneza samani na kufanikiwa kununua miti yenye mita ya ujazo 6000 yenye thamani ya bilioni 3.2,” amesema Seleboni Mushi.
Panataleo Banzi, Mwenyekiti wa Wafanyabiashara za Samani wa Keko jijini Dar es Salaam ni miongoni mwa wadau walioshiriki mnada huo amesema kwa muda mrefu wamekuwa wakiogopa kushiriki kwenye mnada wa misaji lakini baada ya kupata elimu wameshiriki na kubaini mbao za misaji licha ya ubora wake zinapatikana kwa urahisi na hivyo kuwashauri watu kuziangalia kwa jicho la tatu.
Kwa upande wake, mwakilishi wa wafanyabiashara wanaosafirisha Mbao za Misiaji nje ya nchi kutoka Kampuni ya Prime Timber, Malima Mrungu amesema mbao za misaji zina soko kubwa na kuthaminiwa zaidi nje ya nchi kuliko hapa ndani hivyo kunusuru misitu ya asili.
Amesema serikali ielekeze nguvu kwenye miti ya misaji na kuona namna ya kuacha kabisa matumizi ya mbao ngumu za asili.
Charles Kessy, Mwakilishi wa Kampuni ya Darworth wasambazani wa samani mbalimbali nchini amesema katika siku za karibuni wananchi wameonyesha kuelewa thamani ya mbao za misaji jambo lililowalazimu kushiriki na kununua vitalu vya miti katika Shamba la Miti Mtibwa kwa ajili ya kupata malighafi ya kiwanda chao kilichopo Moshi, Kilimanjaro.
Akizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara wanaovuna miti ya Misaji katika Shamba la Miti Longuza, Mkurugenzi wa Kampuni ya Royal Timber LTD, Yusuphy Ngage amesema kufuatia ombi hilo wameazimia ndani ya wiki moja kuhakikisha wanakuja na majibu juu ya nini hasa wanakwenda kuanza kuchangia kama sehemu ya mchango wao kwa jamii.
Katika kutimiza adhima hio wafanyabishara hao walimtaka Diwani na Mtendaji wa Kisiwani waliokuwepo kwenye mnada huo kama watazamaji kukaa na kuwasilisha maeneo ya kipaumbele ambayo wafanyabishara hao watakwenda kuyafania kazi.
Ayubu Mhina ni Mtendaji wa Kisiwani, Muheza anasema katika eneo lake la utendaji kuna changamoto nyingi ambazo Serikali pekee itailazimu kuchukua muda mrefu kuzitatua lakini kwa kushirikiana na viongozi wenzake watakwenda kuainiasha maeneo ya kipaumbele na kuyawailisha tayari kwa utekelezaji.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Muheza, Hamisi Mwinjuma aliyekuwepo kwenye mnada wa Shamba la Miti Longuza lililoko Muheza mkoani Tanga amesema amefika katika mnada huo pamoja na mambo mengine kuhakikisha Ilani ya CCM na maelekezo ya Rais Magufuli ya kutaka kuwepo na ushirikishwaji wa sekta binafsi kwenye masuala mbalimbali na kuhakikisha biashara inaendelea na serikali inakusanya mapato yake huku watu wakifanya biashara.
“Sisi tunachotaka nikuwaomba mshiriki kwenye masuala yanayohusisha jamiii, sisi sio wanasiasa ambao tutakaokuja kuchukua fedha kwenu tuziweke kwenye mifuko yetu, tutakuja kurahisisha biashara yenu kwa namna yoyote inayowezekana ikiwa ndani ya sheria za nchi hii  lakini tutaomba basi jamii zinazozunguka maeneo mnayofanyia biashara na nyinyi mzisaidie kuzirahisishia, kama kuna madarasa yanatakiwa kujengwa, miundombinu inatakiwa kurekebishwa mtusaidie kwa kadri mnavyoweza,” amesema, Mwinjuma maarufu kwa jina la Mwana FA.