Afisa Sera na Majadiliano wa Mtandao wa jamii wa kuhifadhi misitu Tanzania Mjumita Bi. Elida Fundi wakati akiongea na Waandishi wa Habari mara baada ya kumaliza ziara ya siku tano ya kutembelea vijiji vipya vilivyoingia kwenye awamu ya tatu ya Mradi wa Usimamizi shirikishi wa Misitu ya jamiii.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Darajani Wilayani Liwale Mkoani Lindi bwana Hamisi Mbanila akizungumza mbele ya Waandishi wa habari,Wajumbe wa serikali ya kijiji na wajumbe wa Kamati ya maliasi ya kijiji sababu za kuamua kuomba kutekeleza mradi huo kwa sasa.
Mzee maarufu katika Kijiji cha Darajani Mzee Abdurahmani Ngokwe akieleza namna walivohamasika sasa kuomba kutekeelza mradi huo wa uhifadhi shirikishi wa misitu kwenye kijiji chao.Mwenyekiti wa kamati ya maliasili ya Kijiji cha Darajani Bi. Zaituni Likwata akieleza naman kamati yake ilivyojipanga kuhakikisha misitu ya kijiji inalindwa kwa manufaa ya wote.
Na. Calvin Edward Gwabara.
Serikali na wadau wengine wa mistu wameshauliwa kuhimiza vijiji vyote nchini kuanza kutumia mfumo wa usimimizi shirikishi wa misitu ya vijiji ili kulinda misitu hiyo kikamilifu kutokana na motisha wanayoipata ambayo kupunguza mzigo kwa serikali.
Wito huo umetolewa na Afisa Sera na Majadiliano wa Mtandao wa jamii wa kuhifadhi misitu Tanzania Mjumita Bi. Elida Fundi wakati akiongea na Waandishi wa Habari mara baada ya kumaliza ziara ya siku tano ya kutembelea vijiji vipya vilivyoingia kwenye awamu ya tatu ya Mradi wa Usimamizi shirikishi wa Misitu ya jamiii unaotekelezwa chini ya Mradi wa kuleta Mageuzi katika Sekta ya Mkaa Tanzania na Mradi wa kuhifadhi Misitu kwa kuwezesha biashara endelevu ya Misitu (CoFOREST) kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Uswis (SDC).
Amesema kuwa kumekuwepo na mafanikio makubwa katika uhifadhi shirikishi wa misitu kwenye wilaya ya Kilosa,Mvomero na Morogoro Vijijini kwenye vijiji vilivyoshiriki kwenye awamu ya kwanza na ile ya pili kwenye Uhifadhi shirikishi wa misitu ya vijiji hivyo huo ni Ushahidi tosha kuwa vijiji vikitumia mfumo huo vinaweza kusaidia kutunza misitu na kuitumia kwa njia endelevu.
“ Tumeona vijiji vinafanya vizuri sana katika usimamizi wa misitu,Tumeona namna gani usimamizi wa misitu unavyosaidia jamii iweze kunufaika na rasilimali za misitu zilizo kwenye vijiji vyao na tumeona namna gani mapato yanayopatikana kwenye misitu hiyo yalivyowekezwa kwenye kusimamia misitu na kwenye miradi ya maendeleo na usimamizi huo wa mistu umekuwa katika kiwango cha juu sana” Alifafanua Bi. Elida.
Aliongeza kuwa “Kwahiyo sisi kama MJUMITA tunatamani kuona kwamba usimamizi shirikishi wa mistu unasambaa katika maeneo mengi,vijiji vingi ambavyo vina misitu ambayo inaendelea kuteketea hivyo tunahamasisha wajiunge kwenye mpango shirikishi wa usimsmizi wa misitu, tunawaomba wadau,Serikali na watu mbalimbali wasaidie vijiji hivi ambavyo bado vina misitu mingi katika maeneo yao lakini inateketea nab ado haiku kwenye usimamizi wowote hii ni njia pekee inayoweza kuokoa misitu yetu”.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Kijiji cha Darajani Wilayani Liwale Mkoani Lindi bwana Hamisi Mbanila ambao mivutano ya kisiasa ya viongozi na Wananchi alikwamisha Kijiji hicho kushindwa kuingia kwenye mpango huo wa usimamizi shirikishi wa misitu miaka michache iliyopita na furasa hiyo kupewa Kijiji jirani yao amewashauri wananchi wengine vijijini kutochanganya siasa pale linapokuja swala la maendeleo.
“Migogoro na mivutano ya kisiasa amekwamisha Kijiji chetu kupiga hatua kubwa za maendeleo, tumeona wenzetu waliokubali mfumo huo wamefanya mambo makubwa kwenye Kijiji chao wamejenga ofisi nzuri ya kijiji, wanajenga zahanati lakini kubwa Zaidi wanamfumo mzuri wa kulinda misitu yao wakati sisi misitu yetu ikimalizika na hatupati faida yoyote maana hata ofisi ya Kijiji hatuna” Alifafanua Mwenyekiti wa Kijiji hicho bwana Mbanila.
Amesema wanaomba radhi kwa viongozi wa Serikali na wadau wa usimamizi shirikishi wa misitu kwa kukataa mpango huo huko awali na kwamba sasa wanaomba kupewa nafasi nyingine ya kusahihisha makosa yao ili waweze kushiriki kwenye mfumo huo na kunufaika na rasilimali hiyo ya misitu.
Nae Mzee maarufu katika Kijiji hicho mzee Abdurahmani Ngokwe ni kweli mradi huu waliukataa kwenye mkutano wa Kijiji lakini waliukataa kutokana na uelewa tofauti na muingiliano wa kisiasa,lakini kadri vijiji vitatu vya jirani yao ikiwemo Kijiji cha Mihumo walioukubali na kuanza kuona mafanikio yake wamejenga shule wanaingiza mamilioni wao wakabaki wa kutazama lakini sio hivyo tuu wale ile kamati yao wanavyokwenda kwenye doria wanavyovaa vizuri na kulipana posho wao wakabaki wamechanganyikiwa.
“Sasa hata wale waliokuwa wakisema hapana hapana hapana nao wakabaki wanaumia na kusema tutafanyaje,lakini tunamshukuru mwenyezi Mungu namna ambavyo tumejirudi na kuunza kuutaka huu mradi kwa kuwasiliana na Wilaya tukaomba radhi wakatuuliza sasa mmeona faida zake kwa wenzenu? Tukasema haswaa na sisi tunautaka na tunaishukuru sana wilaya ikatukubalia na tumeingia kwenye huu mradi” Alieleza Mzee Ngokwe.
Akizungumzia majukumu ya kamati yake mwenyekiti wa kamati ya maliasili ya Kijiji hicho cha cha Darajani Bi. Zaituni Likwata amesema wamejipanga kufanya doria za usiku na mchana katika msitu wao ili usiendelee kuharibiwa na hivyo baada muda nao waanze kuvuna mbao na mazao mengine kwa njia endelevu badala ya kuwaachia wezi kuharibu msitu wao wa Kijiji kwa faida ya mtu mmoja.
“Mungu akitujaalia matarajio yetu ni kupata fedha za kununulia vyombo vya usafiri kwaajili ya kufanya doria kwenye msitu, lakini pia tujenge shule yetu ya Kijiji maana hili ndio hitaji letu kubwa kwaajili ya Elimu za Watoto wetu, hivyo Msitu huu utatusaidia sana kama unavyosaidia wenzetu” Alieleza Bi. Likwata.
Amesema yeye kama mama kilichomfanya aingie kwenye kamati hiyo ya maliasili ya Kijiji ni kulinda maliasi za Kijiji chake lakini pia kutaka haki itendeke kwa watu wote kwakuwa maliasi za Kijiji ni za wanakijiji wote na kwamba kwa msimamo huo maendeleo kwenye Kijiji cha darajani yatapatikana.