Na John Walter-Babati

Msimamizi wa uchaguzi  Jimbo la Babati Vijijini John Nchimbi amemkabidhi  cheti cha Utambuzi Mbunge wa Jimbo hilo  Daniel Sillo  pamoja na Madiwani  25 wa Chama cha Mapinduzi  waliochaguliwa .

Msimamizi huyo ambaye pia ni mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Babati amewataka Madiwani kutambua kuwa wao ni sauti ya wananchi  hivyo wakafanye  kazi walizowaahidi.

Akizungumza baada ya kupokea cheti hicho leo Oktoba 30, 2020 katika ofisi za Halmashauri za wilaya ya Babati Mbunge huyo amesema  atashirikiana na wanachi katika kutatua changamoto zilizopo za Maji,Umeme pamoja na kuongeza vituo vya afya  ili kusogeza huduma karibu.

Amesema kazi iliyopo kwa sasa baada ya Uchaguzi mkuu kumalizika ni kuwahudumia wananchi wa Babati akishirikiana na Madiwani katika kata 25 za Jimbo hilo.

Katika upande mwingine Sillo ameahidi kushirikiana na vijana kwa kuwashauri kujiunga kwenye vikundi ili waweze kujiajiri wenyewe kupitia mitaji isiyokuwa na riba watakayopatiwa kutoka Halmashauri.

Katibu wa Chama cha Mapinduzi  Babati Vijijini  Filbert  Mdaki amewapongeza wasimamizi wa uchaguzi ambao wamesimamia haki na kufanya uchaguzi kuwa wa utulivu na amani katika Jimbo hilo.

Jimbo la Babati Vijiji lina jumla ya kata 25 na zote zimechukuliwa na Chama cha Mapinduzi.