Home Mchanganyiko LILAMBO WAONDOKANA NA KERO YA MAJI

LILAMBO WAONDOKANA NA KERO YA MAJI

0

 Mkurugenzi wa ununuzi wa ugavi kutoka wizara ya maji Dkt Christopher Nindi kulia,akimtwisha ndoo ya maji mkazi wa mtaa wa Lilambo A Emalisiana Mumba  mara baada ya kukagua ujenzi wa mradi mkubwa wa maji uliotekelezwa na wakala wa maji vijijini  na mjini Ruwasa na Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira manispaa ya Songea Souwasa kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 1

Mkurugenzi wa ununuzi na ugavi wa wizara ya  maji Dkt Christopher Nindi katikati akifungua koki  wakati wa ukaguzi wa mradi wa maji katika mtaa wa Lilambo A uliotekelezwa na wakala wa maji vijijini na mjini Ruwasa  kwa kushirikiana na mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira manispaa ya Songea Souwasa,kushoto mkurugenzi wa Ruwasa mkoa wa Ruvuma Mhandisi Patrick Hans na katikati Mkurugenzi wa Souwasa Mhandisi Patrick Kibasa.

Picha zote na Muhidin Amri,

……………………………………………………………………………………….

Na Muhidin Amri,Songea

ZAIDI ya wakazi 11,981 wa mitaa miwili ya Lilambo A na Lilambo B katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, wameondokana na kero ya muda mrefu ya maji safi na salama baada ya kukamilika kwa mradi mkubwa wa maji uliotekelezwa na Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira manispaa ya Songea(Souwasa).

Mkurugenzi wa Souwasa Patrick Kibasa amesema hayo jana, wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo kwa wataalam kutoka wizara ya maji wakiongozwa na  Mkurugenzi wa Ununuzi wa Ugavi wa wizara hiyo Dkt Christopher Nditi.

Kibasa amesema, mradi huo umetekelezwa chini ya program ya maendeleo ya  sekta ya Maji(WSDP)kupitia program ndogo ya maji na usafi wa mazingira vijijini(RWSSP) ulianza mwezi Mei 2019 na ulitarajiwa kukamilika mwezi Machi 2020 chini  ya usimamizi wa wakala wa maji vijijini na mjini Ruwasa.

Hata hivyo, kutokana na mabadiliko ya sheria ya usimamizi wa huduma za maji safi na  usafi wa mazingira,mkataba wa mradi huo ulihamishwa kutoka Wakala wa maji safi na Usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa) na kwenda Mamlaka ya maji safi na Usafi wa mazingira Songea.

Kwa mujibu wa Kibasa,mradi huo ni wa awamu moja kwa  gharama ya  shilingi bilioni 1,164,555.586 ambapo  kazi zilizopangwa kufanyika ni ujenzi wa chanzo cha kukusanya maji,nyumba ya mashine na uzio wa mita 160,ufungaji pampu,kujenga visima miwili na kusambaza bomba mita 4050 za kusafirishia maji pamoja na meta 10,970 za usambazaji.

Alitaja kazi nyingine, ni kuchimba mitaro na kulaza bomba za usafirishaji na usambazaji maji,ujenzi wa tenki la lita 150,000,kujenga vituo  18 vya kuchotea maji,chemba ya maungio ya maji safi,mifumo ya mfano  ya uvunaji wa maji ya mvua katika taasisi za Serikali na uwekaji wa nguzo za alama za bomba.

Kwa upande wake meneja ufundi wa Souwasa Jafari Yahaya alisema, hadi sasa kazi zilizofanyika  kulingana na mkataba ni ujenzi wa chanzo,visima,tanki la meta za ujazo 25, usambazaji na ufungaji wa pampu na transifoma ya umeme pamoja na kupima wingi wa maji katika chanzo.

Jafari alieleza kazi nyingine zilizotekelezwa katika mradi huo ni ujenzi wa kibanda cha mashine na ufungaji wa mifumo ya umeme,kujenga uzio wa meta 160 katika chanzo na kibanda cha mashine,kusambaza na kuchimba mitaro.

Alisema, mbali na kazi hizo pia ulihusisha ulazaji bomba za kusafirisha na kusambaza maji,kujenga vituo 18 vya kuchotea maji,chemba 4 za kufungia maji,tanki la lita 150,000 na tanki za kutibu maji kutumia klorini.

Alisema, mpaka sasa kazi ambazo hazijafanyika ni pamoja na ujenzi wa mifumo ya mfano wa uvunaji maji ya mvua katika taasisi za Serikali,uandaaji wa michoro baada ya kujenga miundombinu ya maji,na kuandaa mwongozo wa maelekezo  kulingana na mkataba.

Kwa upande wake mkurugenzi wa ununuzi wa ugavi wa wizara ya maji Dkt Christopher Nditi amepongeza  kazi nzuri inayofanywa na Souwasa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maji katika manispaa ya Songea inayolenga kumtoa mama ndoa]o kichwani.

Nditi alisema, adhima ya Serikali ni kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma ya maji safi na salama  na kutoa fursa kwao kujikita zaidi katika shughuli za kiuchumi, badala ya kutumia muda mrefu kwenda kutafuta maji mbali na makazi yao.

Hata hivyo alisema, bwawa la maji linalotumika kama chanzo kikubwa  kwa wakazi wa manispaa hiyo ni ndogo na wizara itaangalia uwezekano wa kuisaidia Souwasa fedha ili kujenga bwawa kubwa lenye uwezo wa kukidhi mahitaji ya wananchi majira yote ya mwaka.

Baadhi ya wakazi wa mtaa wa Lilambo A Emalisiana Mumba na Esha Ahmad wameishukuru serikali ya awamu ya tano  kwa uamuzi wake wa kutoa fedha kwa ajili ya kutekeleza mradi wa maji katika kata ya Lilambo.

Emalisiana alisema, kwa muda mrefu wananchi wa  kata hiyo walilazimika kutembea umabli mrefu kwenda kutafuta maji katika vyanzo visivyo rasmi,kwa hiyo kukamilika kwa mradi huo ni faraja kubwa kwa sababu utawezesha kutumia muda mwingi kujikita katika uzalishaji mali.