Home Mchanganyiko MAELFU YA VIJANA WANUFAIKA NA PROGRAMU YA KUKUZA NA KURASIMISHA UJUZI-MAVUNDE

MAELFU YA VIJANA WANUFAIKA NA PROGRAMU YA KUKUZA NA KURASIMISHA UJUZI-MAVUNDE

0

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu,Kazi, Ajira na Vijana, Anthony Mavunde,akizungumza kwenye mahafali ya vijana 988 waliohitimu mafunzo ya programu ya kukuza na kurasimisha ujuzi katika fani mbalimbali kwenye Taasisi ya Don Bosco  jijini Dodoma.

Sehemu ya vijana waliohitimu mafunzo hayo wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu,Kazi, Ajira na Vijana, Anthony Mavunde (hayupo pichani)  kwenye mahafali ya vijana 988 waliohitimu mafunzo ya programu ya kukuza na kurasimisha ujuzi katika fani mbalimbali kwenye Taasisi ya Don Bosco  jijini Dodoma.

Mkurugenzi wa Donbosco Net Tanzania, Father Merkades Lukanyaga,akitoa taarifa kwenye mahafali ya vijana 988 waliohitimu mafunzo ya programu ya kukuza na kurasimisha ujuzi katika fani mbalimbali kwenye Taasisi ya Don Bosco  jijini Dodoma.

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu,Kazi, Ajira na Vijana, Anthony Mavunde,akiwakabidhi vyeti baadhi ya  vijana 988 waliohitimu mafunzo ya programu ya kukuza na kurasimisha ujuzi katika fani mbalimbali kwenye Taasisi ya Don Bosco  jijini Dodoma.

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu,Kazi, Ajira na Vijana, Anthony Mavunde,akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kuhudhuria mahafali ya vijana 988 waliohitimu mafunzo ya programu ya kukuza na kurasimisha ujuzi katika fani mbalimbali kwenye Taasisi ya Don Bosco  jijini Dodoma.

…………………………………………………………………………………….

Na Alex Sonna, Dodoma

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu,Kazi, Ajira na Vijana, Anthony Mavunde, amesema hadi kufikia Juni mwaka huu vijana 58,328 wamenufaika na programu ya kukuza na kurasimisha ujuzi katika fani mbalimbali.

Mavunde ameyasema hayo leo kwenye mahafali ya vijana 988 waliohitimu mafunzo hayo kwenye Taasisi ya Donbosco Dodoma.

Amesema mafunzo hayo yametolewa kwa vijana 100 kutoka kila Halmashauri nchini, chini ya uratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu katika fani ya ufundi uwashi, magari, bomba, umeme, uchomeleaji, uwekaji terazo na marumaru, seremala, ushonaji nguo, mapishi, uchongaji vipuri, umeme jua.

Amefafanua kati ya idadi hiyo vijana walionufaika na mafunzo ya uanagenzi ni 28,941, urasimishaji ujuzi ni  14,432, mafunzo kwa vitendo kwa wahitimu wa vyuo vya kati na juu ni 5,975, kilimo cha kisasa kupitia teknolojia ya kitalu nyumba umwagiliaji kwa njia ya matone ni 8,980.

“Mafunzo haya hakuna mwanafunzi hata mmoja ambaye amelipia ada bali wamelipiwa na serikali, pia tumewawezesha kutoa usafiri kwa kutoka Sh.100,000 kila mwezi kwa muda wote ambao wapo kwenye mafunzo,”amesema.

Mavunde amesema vijana hao wengine wamepata kazi kwenye miradi mikubwa na waajiri wameendelea kupigana vikumbo kuhitaji vijana hao.

Hata hivyo, amesema serikali imeanza kuongea na wamiliki wa viwanda vya chuma na neti ili vijana hao watengeneze na kuwa sehemu ya ajira kwao.

Naibu Waziri huyo amesema kuwa dira ya maendeleo ya Taifa inalenga ifikapo mwaka 2025, Tanzania ishindane na nchi zingine katika soko la dunia kwa bidhaa zinazochakatwa viwandani.

“Nguvu kazi yenye ujuzi stahiki inahitajika ili viwanda vitengeneze bidhaa zinazohitajika na zenye ubora, kutokana na umuhimu huo serikali imeamua suala la ukuzaji ujuzi wa nguvu kazi ya Taifa kuwa miongoni mwa vipaumbele vya Taifa,”amesema.

Mavunde amesema Rais John Magufuli amechukua hatua mbalimbali za kuhakikisha kunakuwepo na nguvu kazi ya vijana wenye ujuzi wa kutosha.

 “Serikali ina program nyingine inaitwa RPL ni mfumo wa urasimishaji wa ujuzi, kwa vijana wenye ujuzi ambao hawajapitia mfumo rasmi wa mafunzo ya ufundi, ukienda leo mtaani wapo vijana wanaojua kupaka rangi, kujenga, kutengeneza magari hawajawahi kusoma, serikali inachofanya inapeleka wakufunzi na kukaa na vijana hao kubaini mapungufu na kuwapa vyeti,”amesema.

Aliwataka vijana kuunda vikundi ili kupatiwa mikopo isiyo na riba kupitia fedha zinazotolewa na Halmashauri nchini na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana.

Naye, Mkurugenzi wa Donbosco Net Tanzania, Father Merkades Lukanyaga, amesema mafunzo hayo ni ya miezi saba na yamefadhiliwa na serikali kwa asilimia 100 na yalianza mwaka 2019 na kampuni 900 zilitoa nafasi ya mafunzo kwa vitendo kwa vijana hao.

Amesema mafunzo hayo yanatolewa kwenye vituo 18 ambapo umewafikia vijana katika mikoa 13 Tanzania ambayo ni Dodoma, Singida, Iringa, Lindi, Ruvuma, Dar es salaam, Morogoro, Shinyanga, Geita, Kagera, Mara, Kilimanjaro na Arusha.

Kwa upande wake, Mmoja wa wahitimu, Elia Hargo, ameshukuru serikali kwa mafunzo hayo kwa kuwa yamesaidia kutimiza ndoto yake na kupata ajira.