Home Mchanganyiko TAKUKURU SIMANJIRO YAMSHIKILIA MMILIKI WA MASHAMBA MAKUBWA

TAKUKURU SIMANJIRO YAMSHIKILIA MMILIKI WA MASHAMBA MAKUBWA

0

******************************

Na Mwandishi wetu, Manyara

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, inamshikilia mmiliki wa mashamba makubwa Thomas Meliyo kwa kutotimiza wajibu wa kuwalipa stahiki watumishi wa mashamba yake.

Mkuu wa TAKUKURU Mkoani Manyara, Holle Joseph Makungu ameyasema hayo mjini Babati wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Makungu amesema Meliyo mwenye mashamba ya zaidi ya ekari 200 Wilayani Simanjiro, ameajiri kwa kuwaweka kambini kwake wafanyakazi 23 kazi yao ikiwa kupanda, kupalilia, kuvuna, kupukuchua mahindi na kupigapiga maharawe.

Amesema vijana hao waliwasilisha malalamiko yao TAKUKURU kuwa tangu Novemba 2019 hadi sasa wamekuwa wakifanya kazi kwenye mashamba hayo bila kulipwa mshahara kinyume na makubaliano ya mikataba ya ajira zao.

“Ilidaiwa katika malalamiko yao kwamba wanachoambulia ni kupatiwa chakula cha asubuhi, mchana na jioni na kwamba baadhi ya vijana hao wanalalamika kutopelekewa maji ya kuoga kwani wengine hawajaoga kwa zaidi ya miezi sita wakiruhusiwa kunawa uso pekee,” amesema Makungu.

Amesema TAKUKURU Mkoani Manyara, imepokea malalamiko hayo na tayari imeanza kuyafanyia kazi ambapo wameahidi kuwa watahakikisha kuwa haki ya vijana hao inapatikana.

“Ni rai yetu kuwa wamiliki wa mashamba makubwa Mkoani Manyara na waajiri wote kwa ujumla kuhakikisha kwamba wametimiza wajibu wao wa kulipa mishahara ya waajiriwa na kuzingatia kanuni za afya sehemu za kazi, TAKUKURU itaendelea kufuatilia jambo hili ili kuhakikisha waajiri hao wanatekeleza wajibu wao,” amesema.