Home Mchanganyiko JAMII YATAKIWA KUBORESHA FURSA ZA WANAWAKE WANAOISHI VIJIJINI KUCHAGIZA UCHUMI WA VIWANDA

JAMII YATAKIWA KUBORESHA FURSA ZA WANAWAKE WANAOISHI VIJIJINI KUCHAGIZA UCHUMI WA VIWANDA

0

…………………………………………………………………………

Na.Mwandishi wetu,Dodoma

Watanzania wametakiwa kutambua fursa, changamoto na mafanikio ya wanawake wanaoishi Vijijini ili kuweza kuwajengea mazingira mazuri ya kupata haki zao za msingi na kuwawezesha kiuchumi.

Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dodoma na Kaimu Mkurugenzi wa  Maendeleo ya Jinsia , Mboni Mgaza alipokuwa akizungumza na waandishi wa babari  kuelekea maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Mwanamke anayeishi Kijijini.

Amesema Mamlaka za Serikali za Mitaa na wadau wametakiwa kutambua fursa, changamoto na mafanikio ya wanawake wanaoishi kijijini ili kuweza kuwajengea mazingira mazuri ya kupata haki za msingi na kuwawezesha kiuchumi.

Mboni ameongeza kuwa hali hii itasaidia kupiga hatua katika nchi, hivyo kuweka miradi endelevu ya kuwaendeleza wanawake wanaoishi vijijini

“Lengo la maadhimisho haya ni kutambua na kuenzi mchango wa wanawake wanaoishi vijijini hususani katika nyanja za uzalishaji kwenye kilimo, ufugaji, uvuvi na ujasiriamali ili kuhakikisha usalama wa chakula wa kaya hivyo kuchangia uchumi wa Taifa” alisema Mboni.

Ameongeza kuwa, siku hii inalenga kuwaunganisha wanawake na wadau katika mtandao wa kibiashara ili kuhakikisha wanafaidika na mfumo wa kifedha wa kidijitaji.

Aidha, kuwaelimisha wanawake jinsi ya kupata teknolojia rahisi na sahihi za uzalishaji ili kuweza kumudu ushindani wa biashara katika masoko ya ndani na nje ya Tanzania.

Amebainisha kuwa asilimia 65 ya wanawake wapo katika sekta ya kilimo ambayo inaonesha kuwa wanachangia kwa kiasi kikubwa mazao ya kilimo yanachangiwa na kundi hili.

Serikali imechukua hatua mbalimbali kuboresha miundombinu vijijini ikiwa ni hatua kubwa kuwainua wananchi hususani wanawake.

Maadhimisho ya Siku ya Mwanamke anayeishi Kijijini huadhimishwa kila tarehe 15 Oktoba na  mwaka huu, yatafanyika katika kijiji cha Kazole, kata ya Vikindu, Wilaya ya Mkuranga, Mkoa wa Pwani lakini kila Mkoa na Halmashuri zote nchini zitaadhimisha siku hii kwenye maeneo maeneo husika.

Kaulimbiu ya siku ni “Mwanamke anayeishi kijijini ni msingi na ustawi wa maendeleo ya nchi”.