Home Mchanganyiko ‘Jambo letu’ kuhusu maji ni kwa wananchi wote

‘Jambo letu’ kuhusu maji ni kwa wananchi wote

0

Wananchi wa Kijiji cha Kinkima Wilayani Chemba mkoani Dodoma wakipata huduma ya mji wakati wa majaribio ya mradi wa maji wa Ntomoko

Afisa toka Wakala wa Usambaaji Maji na Usafi wa Mazingira Wilaya ya Kongwa. Barkat Ally akimtwisha mama ndoo ya maji mara baada ya kukagua mradi wa maji katika kijiji cha Mtanana Wilayani Kongwa mkoani Dodoma.

Maafisa wa Wizara ya Maji wakikagua mradi wa maji wilayani ManyaraWataalam wa Wizara Ya Maji wakiendelea na ujenzi wa chanzo cha maji cha Magadu Manispaa ya Morogoro.

***********************************

Na, Evaristy Masuha

Msemo wa ‘tuna jambo letu’ si mgeni kwa wazungumzaji wa Kiswahili na umekuwa ukitumika kuonesha matarajio ya suala lililokusudiwa. Nimeamua kuutumia katika kujenga hoja iliyoko ndani ya makala hii ambayo inaangazia lengo la Wizara ya Maji katika kazi kubwa ya kuwafikishia Watanzania huduma ya majisafi na salama, yenye kutosheleza na katika mazingira rafiki. 

Ni malengo yenye maono makubwa ambayo yamefafanuliwa katika nyaraka mbalimbali za Wizara ikiwemo mpango wa mwaka 2020/2021, kama ulivyowasilishwa Bungeni na Waziri wa Maji Mhe. Profesa Makame Mbarawa (Mb). 

Nyaraka na machapisho hayo ya Wizara ni udhibitisho kwa Watanzania kuwa ni ‘jambo lao’ linafanyiwa kazi, na likiwa limekamilika katika baadhi ya maeneo, kazi inaendelea kwa sababu tafiti zilizofanywa na wataalam zinaonesha nchi yetu inayo maji ya kutosha kwa matumizi mbalimbali ya maendeleo kwa wananchi, kuanzia viwanda, kilimo hadi matumizi ya majumbani. 

Atlasi ya Taifa ya Rasilimali za Maji, Toleo la Mwaka 2019 iliyochapishwa na Wizara ya Maji inaonyesha wazi kuwa nchi yetu ina maji ya kutosha na haina upungufu. Atlasi inaonyesha kuwa Tanzania inakadiriwa kuwa na rasilimali za maji zinazofaa kwa matumizi ya binadamu kwa wastani wa mita za ujazo bilioni 126, ambapo mita za ujazo bilioni 105 zipo  juu ya ardhi na mita za ujazo bilioni 21 chini ya ardhi. 

Kwa kuzingatia makadirio ya idadi ya watu milioni 54 katika mwaka 2018, kiasi cha maji kilichopo kwa kila mtu kwa mwaka (per capital water) ni takribani wastani wa mita za ujazo 2,300. Kiasi hiki  ni juu ya wastani wa mita za ujazo 1,700 ambacho ni kiwango cha chini cha mahitaji ya maji kwa mtu kwa mwaka kinachokubalika kimataifa; chini ya kiwango hiki nchi huhesabika kuwa na uhaba wa maji (water stress). 

Kazi ya kufikisha huduma ya maji kwa Watanzania inafanyika, usiku na mchana. Hatua imepigwa, na hadi hivi sasa huduma ilipotolewa ni mbali na mafanikio ni makubwa. Takwimu zinajihidhirisha wazi katika machapisho kuhusu sekta ya maji hapa nchini. Wakati  Bunge la Kumi na Moja la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Juni 16, 2020 likifungwa, ilifafanuliwa kuwa Watanzania wanaopata huduma ya majisafi na salama hadi mwezi machi mwaka 2020 walikuwa wamefikia asilimia 70.1 kutoka asilimia 47 iliyokuwepo mwaka 2015, na wale waishio mijini wakiwa wamefikia asilimia 84 kutoka asilimia 74 ya mwaka 2015.

Moja ya jambo kubwa ambalo lipo katika mpango ni kuhakikisha maeneo ya umma yanapata huduma ya maji. Miongoni mwa yatakayofanyika ni kuboresha huduma ya majisafi na usafi wa mazingira katika vituo vya afya na shule ambapo tathmini ya awali imebaini vituo vya afya 1,195 havina huduma ya maji kati ya vituo 6,134; na shule 5,721 kati ya shule 19,965. Katika kufanikisha hilo Wizara ya Maji imetenga kiasi cha shilingi bilioni mbili katika mpango wake wa 2020/2021. 

Jambo lingine ni kuyafikisha maji ya ziwa Viktoria katika miji ya Dodoma na Singida, (tathmini ya awali imefanyika),  kupitia mfumo wa Taifa wa Usambazaji Maji (National Water Supply Grid). Mfumo huu unalenga kuhakikisha maji yanapatikana kwenye maeneo yote nchini kwa kipindi chote cha mwaka bila kujali iwapo eneo husika lina vyanzo vya maji vingi au lina uhaba wa maji. Mfumo huu utahusisha ujenzi wa mtandao wa kusafirisha maji kutoka maeneo yenye maji mengi na kuyapeleka kwenye maeneo yenye uhaba wa maji. Utaratibu huu ambao unalenga kuwaletea maendeleo Watanzania ndio umewezesha maji ya ziwa Viktoria kufika katika miji ya Tabora, Igunga, na Nzega hivyo miji hii kuwa na uhakika wa majisafi, salama na yenye kutosheleza. 

Mpango wa kutoa maji ya ziwa Viktoria kwenda Singida na Dodoma ambapo upembuzi wa awali umefanyika na matokeo yake yanaonesha kuwa mradi huo unawezekana na utakuwa na manufaa makubwa kwa kupatikana kwa huduma endelevu ya maji katika miji ya Dodoma na Singida na hivyo kukabiliana na hali ya ukame katika mikoa hii. 

Wakati maeneo yenye maji mengi yakiwezesha maeneo yenye uhaba wa maji kupata huduma hiyo kupitia mpango wa Gridi ya Maji, Wizara ya Maji pia imejipanga kufanya matumizi ya maji ya Maziwa Makuu ambapo jambo hilo litahusu uboreshaji wa huduma ya maji katika vijiji vilivyopo kandokando ya maziwa hayo, maeneo ya pembezoni mwa maziwa ya; Tanganyika, Nyasa na Viktori kwa lengo la kuwapatia wananchi huduma ya majisafi, salama ya kutosha. 

Mgawanyo huo wa matumizi wa maji ya maziwa, umefafanuliwa kuwa ni pamoja na mradi wa kutoa maji Ziwa Tanganyika katika mikoa ya Kigoma, Rukwa na Katavi ambao utanufaisha vijiji 73 vya Halmashauri za Wilaya za Kigoma, Uvinza, Nkasi, Kalambo, Mpimbwe na Mpanda na mradi wa kutoa maji Ziwa Nyasa katika mikoa ya Njombe na Ruvuma utanufaisha vijiji 41 vya Halmashauri za Wilaya za Ludewa na Nyasa. 

Mradi mwingine ni kutoa maji ziwa Victoria na utatekelezwa katika mikoa ya Mwanza, Kagera, Geita, Mara na Simiyu na utahusisha vijiji 301 vya mikoa hiyo. 

Tunasema huu ndio uthubutu ambao viongozi wa sekta ya maji hapa nchini wamepanga kufanikisha kwa manufaa ya Watanzania. Ni jambo la Watanzania hili na kukumbusha tu, kazi inaendelea ambapo kwa kipindi cha miaka mitano jumla ya miradi ya maji 1423 imetekelezwa ambapo miradi 1,268 ikiwa ni ya vijijini na miradi 155 ikiwa imetekezwa mijini.

Takwimu hizi zinaongea na mipango itakamilishwa kufikisha huduma ya maji kwa kila mwananchi, hakuna Mtanzania atakayeachwa.