Home Mchanganyiko TAKUKURU WAMFIKISHA MAHAKAMANI KWA KUTUMIA JINA LA DC KUJIPATIA FEDHA

TAKUKURU WAMFIKISHA MAHAKAMANI KWA KUTUMIA JINA LA DC KUJIPATIA FEDHA

0

Mkazi wa Wilayani Kiteto Mkoani Manyara, Moita Tapeno Paparai amefikishwa mahakamani kwa kosa la kutumia vibayajina la Mkuu wa Wilaya ya Kiteto.

…………………………………………………………………………………….

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU kwa kushirikiana na jeshi la polisi wamemfikisha mahakamani mkazi wa Wilayani Kiteto Mkoani Manyara, Moita Tapeno Paparai kwa kutumia jina la Mkuu wa Wilaya ya Kiteto kanali Patrick Songea na kujipatia shilingi laki tano.

Mwendesha mashtaka wa polisi D/C Ramadhan akisoma hati ya mashtaka mbele ya hakimu mkazi wa wilaya hiyo Mossy Sasi, amesema Moita amefanya kosa hilo kinyume cha kifungu cha 302 cha kanuni ya adhabu.

D/C Ramadhan amesema katika kesi hiyo namba CC 22/2020 pamoja na shtaka hilo pia Moita ameshtakiwa kwa kosa lingine la pili.

Amesema mshtakiwa huyo alijifanya Ofisa ustawi wa jamii kinyume cha kifungu cha 100 kanuni ya adhabu.

Hata hivyo, Moita alikana mashtaka hayo pindi alipoulizwa mahakamani hapo kama ni kweli ametenda kosa hilo.

Mshtakiwa huyo alipelekwa mahabusu kwenye gereza la wilaya ya Kiteto, baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana hadi Octoba 21 kesi hiyo itakapotajwa tena.

Mkuu wa TAKUKURU Mkoani Manyara, Holle Joseph Makungu ametoa rai kwa wananchi kuiga mfano wa mwananchi aliyetoa taarifa za Paparai kwenye ofisi ya TAKUKURU kwa kutokubali kutoa fedha kwa kisingizio cha kutumwa na viongozi wa Serikali.

Makungu amesema wananchi wanapaswa kutoa taarifa TAKUKURU au kituo cha polisi katika eneo la karibu ili hatua ziweze kuchukuliwa kama ilivyofanyika kwa Moita.