Home Mchanganyiko “TUMEREJESHA NYUMBA 3 NA MAGARI 3 KWA KIWANDA CHA KUKOBOA KAHAWA MOSHI”...

“TUMEREJESHA NYUMBA 3 NA MAGARI 3 KWA KIWANDA CHA KUKOBOA KAHAWA MOSHI” -KUSAYA

0

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya (katikati) akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Anna Mghwira ( kushoto) wakiwa wameshika kadi za magari matatu yaliyorejeshwa kwa kiwanda cha kukoboa kahawa (TCCCo) kufutia kazi iliyofanywa na Kamati ya Waziri Mkuu kufuatilia mali za ushirika zilizouzwa kinyume cha utaratibu.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Anna Mghwira ( kushoto) akiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya (kulia) wakionyesha hati za umiliki nyumba tatu zilizorejeshwa na serikali kwa kiwanda cha kukoboa kahawa cha Moshi kutoka waliouziwa kinyume cha utaratibu kufuatia kazi iliyofanywa na Kamati Maalum ya Waziri Mkuu aliyounda mwaka 2016 kufuatilia mali za vyma vya ushirika nchini.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Anna Mghwira akiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya mara baada ya kukbaidhi magari matatu ( yanaonekana nyuma yao) kwa kiwanda cha kukoboa kahawa cha Moshi jana.

Pichani ni nyumba yenye hati namba 11293  iliyoko mtaa wa Rindi Lane mjini Moshi iliyorejeshwa toka kwa Isaack Mowo kwa Kiwanda cha Kukoboa Kahawa ( TCCCo) kufuatia kuuzwa kinyume cha utaratibu kwa shilingi Bilioni 1.5

Nyumba yenye 11234 iliyorejeshwa kwa kiwanda cha kukoboa kahawa cha Moshi (TCCCo) toka kwa Zadock Koola aliyeuziwa kinyume cha utaratibu kwa gharama ya shilingi milioni 450 eneo la Shanty Town mtoni road mjini Moshi kufuatia kamati maalum iliyoundwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa mwaka 2016 kufuatilia mali za vyama vya ushirika nchini.
( Habari na picha na Wizara ya Kilimo) 

……………………………………………………………………………………

Serikali imefanikiwa kurejesha mali za kiwanda cha kukoboa kahawa cha Moshi (TCCCo) zilizouzwa kwa watu binafsi kinyume cha utaratibu ikiwemo nyumba tatu na magari matatu zenye thamani ya shilingi Bilioni 2.2

Mali hizo zimekabidhiwa jana (03.10.2020) wilayani Moshi mkoa wa Kilimanjaro na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya alipofanya kikao na watumishi wa kiwanda cha kukoboa kahawa cha Moshi.

Kusaya alisema mali hizo zimerejeshwa Serikalini kufuatia kazi nzuri iliyofanywa na Kamati iliyondwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa mwaka 2016 kufuatilia ubadhirifu kwenye vyama vikuu vya ushirika nchini kikiwemo Tanganyika Coffee Curing Company ( TCCCo) Limited.

“ Serikali ya Awamu ya Tano haitovumilia vitendo vya viongozi wa ushirika kuhujumu mali za wakulima,ndio maana imefanikiwa kurejesha mali hizi kwa wanaushirika baada ya kuuzwa kinyume cha utaratibu” alisema Kusaya

Katibu Mkuu huyo alikabidhi hati za nyumba tatu na kadi za magari matatu kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Kiwanda cha Kukoboa Kahawa Moshi John Boshe akishuhudiwa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Dkt.Anna Mghwira.

Nyumba zilizorejeshwa TCCCo ni Hati na.11293 ( 056021/45) iliyoko Shanty Town  mtaa wa Rindi lane iliyokuwa imeuzwa kwa Issac Mowo kwa Shilingi Bilioni 1.5

Kusaya alitaja nyumba nyingine iliyorejeshwa  ni yenye hati namba 11235 iliyoko Shanty Town mtoni road iiliyokuwa imeuzwa kwa Zadock Koola kwa Shilingi milioni 450 na nyumba ya tatu ni yenye hati namba 12254 iliyoko Shanty Town  Kaufman Estate iliyokuwa imeuzwa kwa Sylivester Koka kwa Shilingi milioni 250.

Aidha, serikali imekabidhi pia magari matatu kwa uongozi wa kiwanda cha kahawa Moshi ambayo pia yaliuzwa kinyume cha utaratibu ikiwemo lori lenye usajili T 215 ACD iliyouzwa mwaka 2011 kwa shilingi milioni 12.5 kwa John D.Tarimo

Magari mengine yaliyorejeshwa TCCCo ni Toyota Landcruiser T 199 ACD aliyokuwa ameuziwa Felix Mmasi kwa shilingi milioni 10.5 na T 187 ACD iliyokuwa imeuzwa kwa shilingi milioni 35 kwa Gabriel Mrema.

“ Magari haya tayari umiliki wake umebadilishwa kutoka waliokuwa wamenunua na kadi halisi za magari zimesajiliwa na kuwa mali ya TCCCo “ alisisitiza Kusaya

Kusaya alitoa onyo kwa Viongozi wa vyama vya ushirika nchini kuacha ubadhirifu wa mali za umma na kuwa wizara ya Kilimo itahakikisha mali zote zinazohamishika na zisizohamishika zinatumika kwa manufaa ya wana ushikika.

Akizungumza na wafanyakazi wa kiwanda cha kukoboa kahawa Moshi Kusaya aliwataka kuhakikisha wanafanya kazi kibiashara na kuendana na mabadiliko ya kisayansi ili ushirika uwe na manufaa.

Kwa upande wake  Mwenyekiti wa Bodi ya TCCCo Jonh Boshe aliishukuru serikali kwa kuwezesha mali zenye thamani ya Shilingi Bilioni 2.25 kurejeshwa kwa wakulima ikiwemo nyumba tatu na magari.

“ Tunatoa pongezi nyingi kwa serikali kupitia Tume ya Waziri Mkuu kwa kazi nzuri ya kuhakikisha kiwanda cha wakulima wa Kahawa  Moshi kinaendelea kuwepo na kustawi” alisema Boshe.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Anna Mghwira alisema anawasihi wakazi wa mkoa huo kuunga mkono jitihada za serikali kuhakikisha kiwanda cha kukoboa kahawa Moshi kinarejea kuanza kazi .

Mghwira aliongeza kusema lengo la mkoa ni kuona mali zote zilizokuwa za kiwanda cha kahawa na chama kikuu cha ushirika (KNCU) zilizouzwa kwa bei ya kutupwa zinarejeshwa kwa wanaushirika.

“ Kitendo cha leo kurejesha nyumba na magari matatu kwa kiwanda cha kukoboa kahawa Moshi ni ishara ya mwanzo kuwa mali zote zilizouzwa kinyemela zinarejeshwa kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi ili ziwanufaishe wakulima wengi wa kahawa” alisisitiza Mghwira

Mkuu huyo wa mkoa alisema mkakati wa mkoa ni kufufua kiwanda na kuwa muda si mrefu kitaanza kazi ya kukoboa kahawa ya wakulima baada ya benki ya CRBD kukubali kutoa fedha.

Kiwanda cha kukoboa kahawa cha Moshi kilianzishwa mwaka 1920 wakati wa Utawala wa Wajerumani na ilipofika mwaka 1970 kilitaifishwa na serikali na mwaka 1989 kilirudishwa mikononi mwa vyama vikuu vya ushirika kikiwemo KNCU chenye hisa asilimia 54.

Serikali ya Awamu ya Tano mnamo mwaka 2016 iliamua kufanya kazi ya kufuatilia mali za vyama vya ushirika zilizouzwa kinyume cha taratibu na kuzirejesha kupitia Kamati Maalum iliyoundwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Mwisho.

Imeandaliwa na;

Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

Wizara ya Kilimo

MOSHI

04.10.2020