Home Siasa WAJIBU WA MAWAKALA KUELEKEA UCHAGUZI MKUU 2020

WAJIBU WA MAWAKALA KUELEKEA UCHAGUZI MKUU 2020

0

………………………………………………………………………………

Na. Lilian Shembilu

Kifungu cha 134 sura ya 345 cha Sheria ya Mikataba kinamwelezea Wakala kama mtu aliyeajiriwa kufanya kazi au kitu chochote kwa niaba ya mtu mwingine au kumwakilisha mtu mwingine katika shughuli fulani, hivyo basi wakala ni mtu anayesimama kwa niaba ya mhusika mkuu.

Sheria ya Mikataba kifungu cha 135 na 136 inaeleza sifa za kisheria ambazo wakala
anapaswa kuwa nazo; ili kuwa wakala mtu anatakiwa awe na umri wa miaka 18 na
kuendelea na ni lazima awe na akili timamu. Pamoja na sifa hizo za kisheria mhusika mkuu anaweza kuongeza nyingine kutegemeana na uhitaji wa aina ya uwakala anaoutaka.

Wakala wa chama cha siasa kwenye uchaguzi ni mwakilishi aliyeteuliwa na chama baada ya kupata ridhaa ya mgombea kwa ajili ya kusimamia maslahi ya chama au mgombea, kila chama cha siasa kinatakiwa kuwa na wakala mmoja (1) tu kwa kituo ambaye atawakilisha wagombea wa chama hicho kwa uchaguzi wa Rais, Mbunge na Diwani katika kituo husika.

Kwa mujibu wa kifungu cha 57(1) na (2) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343, na kifungu cha 58 (1) na (2) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura
ya 292, chama cha siasa kinaruhusiwa baada ya kupata ridhaa ya mgombea au wagombea kuteuwa na kuwasilisha kwa Msimamizi wa Uchaguzi orodha ya majina ya mawakala wa upigaji kura siku saba (7) kabla ya siku ya uchaguzi.

Mawakala wa uchaguzi huteuliwa na vyama vyao vya siasa na kupewa kibali cha uteuzi, hata hivyo ni vizuri wakala akawa ni mkazi wa eneo la kituo anachokisimamia ili iwe rahisi kuwatambua wapiga kura wa eneo hilo ili kulinda maslahi ya chama na mgombea anayemuwakilisha, lakini pia wakala anapaswa kushirikiana ipasavyo na msimamizi wa kituo ili kuhakikisha sheria na taratibu zinafatwa muda wote wa zoezi la upigaji kura.

Mawakala hawa wanatakiwa kuapa kiapo cha kutunza siri mbele ya Msimamizi wa
Uchaguzi au Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi siku saba (7) kabla ya Uchaguzi, hii ni
kwa mujibu wa kanuni ya 50 (4) ya Kanuni za Uchaguzi wa Rais na Wabunge ya
mwaka 2020 na kanuni ya 43 (4) ya Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa
(Uchaguzi wa Madiwani) ya mwaka 2020.

Tume ya Uchaguzi (NEC) hutoa vijitabu vya maelekezo kwa vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi ili kuwapa mafunzo mawakala ya namna wanavyoweza kutekeleza wajibu na majukumu yao bila kuvunja taratibu na sheria zilizowekwa.

Mawakala wa upigaji kura wana wajibu wa kuhakikisha wanamtambua mpiga kura
kama ndiye mwenye jina lililoandikwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura. Hii
husaidia kupatikana kwa kura halali zilizopigwa na watu wa eneo husika na si vinginevyo lakini pia kudhibiti wale wadanganyifu.

Aidha mawakala wa upigaji kura wana wajibu wa kuhakikisha wanamwakilisha vizuri mgombea toka hatua ya kwanza ya upigaji kura na kulinda maslahi yake mpaka mwisho wa uchaguzi na kushirikiana na Msimamizi wa Kituo na Msimamizi

Msaidizi wa Kituo katika kuhakikisha kwamba mwenendo wa upigaji kura kituoni
unazingatia masharti ya Sheria na taratibu zilizowekwa. Wakala anatakiwa kuhakikisha kwamba hakuna udanganyifu wala matendo yanayoenda kinyume cha sheria na masharti yaliyowekwa katika kuendesha zoezi zima la upigaji kura.

Kwa mujibu wa Sheria za Uchaguzi, Mawakala wanatakiwa kuwa waaminifu na kuhakikisha wanasaini fomu, kama hakuwepo au amekataa kusaini fomu zozote anazotakiwa kusaini kisheria wakati wa upigaji kura, kuhesabu kura, au kujumlisha
kura, hakutabatilisha kazi yoyote itakayoendeshwa kwa mujibu wa sheria.

Wakala wa upigaji kura atapaswa kukiwakilisha vyema chama chake kwenye zoezi
zima la kuhesabu kura baada ya kukamilika kwa zoezi la upigaji kura kwani wakala
wa upigaji ndiye atakuwa wakala wa kuhesabu kura za chama chake.

Kwa mujibu wa kifungu cha 57 (3) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 chama kitaruhusiwa kuteua wakala mbadala endapo aliyeteuliwa awali amefariki au ameshindwa kutekeleza majukumu ya uwakala.

Tarehe 28 October Tanzania inaenda kufanya uchaguzi wake wa sita tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi, ambapo vyama mbalimbali vya siasa vimesimamisha wagombea wao katika nafasi ya rais, wabunge, na madiwani ambapo mpaka sasa wagombea hao wanaendelea kuzunguka katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya kampeni zao.