Home Mchanganyiko WAHIFADHI TFS WAASWA KUDUMISHA UMOJA KUKUZA UZALISHAJI RASILIMALI

WAHIFADHI TFS WAASWA KUDUMISHA UMOJA KUKUZA UZALISHAJI RASILIMALI

0

……………………………………………………………………..
NA MWANDISHI WETU, MOROGORO

WAHIFADHI wa Kanda na Wasaidizi wa Uzalishaji Rasilimali za Nyuki wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) wametakiwa kudumisha umoja ili kuongeza uzalishaji.

Kauli hiyo ya kuwataka kuongeza uzalishaji imetolewa na Kamishina wa Uhifadhi wa TFS Profesa Dos Santos Silayo jana mkoani Morogoro katika kikao cha ndani na maofisa hao.
Alisema wahifadhi wa TFS katika ngazi zote na maeneo yote kujenga na kudumisha umoja lakini kuthamini juhudi za kila mmoja bila kubaguana.

Profesa Silayo amehimiza wahifadhi hao kuelewa nafasi ya kila mmoja kwenye uzalishaji kwa manufaa ya Taasisi na Taifa kwa ujumla.

“Changamoto zipo lakini huwezi kutatua changamoto bila kubadili mtazamo, ni lazima kuwa kitu kimoja, watu wa Nyuki katika maeneo yetu wapewe nafasi. Wahifadhi wakuu kwenye kanda wekeni mazingira bora ya uzalishaji Nyuki,” Profesa Silayo.

Profesa Silayo amepongeza kwa kuwataka wataalamu wa Nyuki kuacha kukimbilia kufanya kazi kwenye vizuia na badala yake wafanye kazi yao ya Uzalishaji wa Rasilimali Nyuki.

“Watu wa Nyuki waende kwenye kazi zao, hatusemi wasiende kwenye vizuia lakini wanaweza kufanya kazi vizuri zaidi kwenye kuzalisha Mazao ya Nyuki.wasaidizi wa Kamishina kwenye Kanda Muwasaidie”Profesa Silayo.

Awali Kamishina wa Uhifadhi TFS alishiriki  kikao cha Bodi ya ushauri ya TFS (MAB) kilichoongozwa na Mwenyekiti wa Bodi Brigedia Jenerali Mbaraka Mkeremy ambacho kilitanguliwa na ziara ya Bodi kutembelea Mradi wa Umeme wa Bwawa la Mwalimu Nyerere na Hafla ya kuvishwa vyeo Wahifadhi 963 wa TFS.

Naye Naibu Kamishina wa Uhifadhi anayesimamia Masoko na Matumizi ya Rasilimali Afande Mohamed Kilongo amewaasa Wahifadhi wa TFS kuendelea kupanda miti, kuhifadhi Misitu Asilia lakini zaidi sana kuhakikisha uzalishaji wa Rasilimali Nyuki wenye tija kwa maslahi mapana ya Taasisi na Taifa.

“Tuendelee kupanda miti, tuendelee kuhifadhi misitu Asilia lakini zaidi sana kuhakikisha tunakuza na kuimarisha  uzalishaji Rasilimali Nyuki kwa maslahi mapana ya Taasisi na Taifa “Afande Kilongo.

Kwa upande wake Msaidizi wa Kamishina anayeshughulikia Uzalishaji Rasilimali za Nyuki TFS Makao Makuu Hussein Msuya amewasilisha muhtasari wa hoja na maazimio mbalimbali yaliyoafikiwa na Wahifadhi hao kwa Kamishina wa Uhifadhi na inatarajiwa yatafanyiwa maamzi mapema.