Home Mchanganyiko WADAU WA MADINI YA TANZANITE WAASWA

WADAU WA MADINI YA TANZANITE WAASWA

0
Katibu wa chama cha wachimbaji Mkoani Manyara, (MAREMA) Tariq James akizungumza kwenye kikao hicho
Ofisa madini mkazi wa Mirerani, Hamis Kamando akizungumza na wadau wa madini ya Tanzanite kwenye ukumbi wa Kazamoyo kwa Luka
Mdau wa madini ya Tanzanite Japhary Matimbwa akizungumza kwenye kikao cha wadau wa madini ya Tanzanite Mji mdogo wa Mirerani.
******************************************
WADAU wa madini ya Tanzanite wa Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wametakiwa kuwa na msimamo mmoja katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu ili kuchagua viongozi bora watakaojali maslahi ya wachimbaji na siyo kufuata mkumbo kwa kudanganywa na wagombea wasiokuwa na sera.
Mdau wa madini Japhary Matimbwa aliyasema hayo jana mji mdogo wa Mirerani kwenye kikao cha wadau wa madini kilichoitishwa na Tume ya madini na chama cha wachimbaji mkoani Manyara (MAREMA).
Matimbwa alisema wachimbaji madini wanapaswa kujitambua kwani baadhi ya wanasiasa wamekuwa wanawatumia kipindi cha uchaguzi kwa maslahi yao na mwisho wa siku wanateseka wenyewe.
Alisema kila mwenye mgodi anapaswa kutambua wachimbaji wake waliojiandikisha wanapiga kura ili kuhakikisha wanapatikana viongozi bora watakaowasaidia wadau wa madini.
“Wadau mumewekeza fedha nyingi kwenye madini hivyo tunapaswa kwenda na CCM ili kupata viongozi ambao watakuwa msaada mkubwa kwetu kwenye sekta hii ya madini na siyo vinginevyo,” alisema Matimbwa.
Alisema mwaka 2015 wachimbaji walichagua madiwani na wabunge wa upinzani lakini Rais John Magufuli hakujali hilo kwani alinunua gari la wagonjwa wa kituo cha afya na kujenga barabara ya lami Kia-Mirerani.
Ofisa madini mkazi wa Mirerani, Hamis Kamando alisema Mirerani ya hivi sasa ni tofauti na ya miaka iliyopita kwani wadau wa madini ni wazalendo wenye kujali maslahi ya Taifa.
Kamando alisema wadau wa madini wanapaswa kuendelea na hali hiyo kwani Serikali itawaunga mkono na kuwapa kipaumbele pindi fursa nyingine zikitokea kupitia madini ya Tanzanite.
“Hivi karibuni Waziri wa Madini Dotto Biteko alipofika Mirerani aliwapa ahadi juu ya uchimbaji wa kitalu C hivyo vuteni subira na endelezeni ushirikiano na serikali matunda yake yataonekana,” alisema.
Kiongozi wa kamati ya usalama eneo la ukuta unaozunguka eneo la migodi ya Tanzanite, Meja Gerald Rwenyagira alisema wadau wa madini wanapaswa kuwa na umoja ili waweze kufanikiwa kwenye shughuli zao.
Meja Rwenyagira alisema wadau wa madini ya Tanzanite wanatakiwa kuchangia maendeleo ya jamii inayowazunguka ili serikali iwape ushirikiano mkubwa zaidi ya uliopo hivi sasa.
Hata hivyo, katibu wa MAREMA, Tariq James aliwataka wachimbaji kufanya shughuli zao kwa kufuata sheria ya madini ya mwaka 2010 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2017.
James alisikitishwa na kitendo cha wadau wa madini kushiriki kwa uchache kikao hicho japokuwa walipewa taarifa ya kuhudhuria kwa wingi.