Home Siasa MAJALIWA ASEMA KITI CHA URAIS SIYO MCHEZO

MAJALIWA ASEMA KITI CHA URAIS SIYO MCHEZO

0

Mjumbe wa Kamati Kuu, Kassim Majaliwa, akiwahutubia wananchi wa Jimbo la Kwimba, katika mkutano wa kampeni, uliyofanyika katika viwanja vya sokoni, Septemba 24, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Mjumbe wa Kamati Kuu, Kassim Majaliwa, akiwakabidhi nakala ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020-2025 Mgombea Ubunge wa Jimbo la Kwimba, Mansoor Jamal, katika mkutano wa kampeni, uliyofanyika katika viwanja vya sokoni, Septemba 24, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Wananchi wa Jimbo la Kwimba, wakimsikiliza Mjumbe wa Kamati Kuu, Kassim Majaliwa, wakati akiwahutubia katika mkutano wa kampeni, uliyofanyika katika viwanja vya sokoni, Septemba 24, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

***************************************

  • Ataka wananchi wampe kura zote Dkt. Magufuli

 

MJUMBE wa Kamati kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Kassim Majaliwa amesema kiti cha urais siyo cha mchezo, kinahitaji mtu makini.

“Uongozi wa nchi siyo jambo la mchezo, linataka kiongozi makini, kiongozi anayetetea rasilmali na anayetetea wanyonge dhidi ya rushwa na ufisadi,” amesema. 

Ametoa kauli hiyo leo mchana (Alhamisi, Septemba 24, 2020) wakati akizungumza na wakazi wa kata za Hungumalwa na Ngudu wilayani Kwimba, mkoani Mwanza kwenye mkutano uliofanyika kwenye viwanja vya sokoni.

“Wengine watakuja kuomba kura lakini kazi yao kubwa ni kukashifu kila jambo linalofanywa na Serikali. Naomba kura za wananchi wote, wana CUF, CHADEMA, ACT mkipigie kura Chama cha Mapinduzi sababu maendeleo hayana chama.”

“Wakija hapa muwasikilize; mkiwauliza Ilani yao watakwambia wanayo ila iko kwenye website. Sisi ya kwetu tunayo hii hapa,” alisema huku akionesha Ilani ya CCM ya 2020 – 2025.”

Amewataka wakazi hao wafanye maamuzi thabiti ya kutafuta viongozi tena wanaozungumza lugha moja. “Viongozi hao ninawaombea kura ni Rais, Mbunge na Diwani. Msichague viongozi ambao kazi yao ni kusema hapana kwenye mambo ya maendeleo au kwenye bajeti ya Taifa. Naomba kura kwa viongozi hao watatu,” amesema.

Mheshimiwa Majaliwa ambaye yuko mkoani Mwanza kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli, alitumia fursa hiyo kumwombea kura mgombea ubunge wa jimbo la Kwimba, Bw. Shanif Mansoor, mgombea udiwani wa Hungumalwa, Bw. Bukaba  Majoge na madiwani wa kata zote za wilaya ya Kwimba.

Wakati huohuo, mgombea ubunge wa jimbo la Geita Vijijini, Bw. Joseph Kasheku Msukuma ambaye aliwepo kwenye mikutano huo, alitumia fursa hiyo kuiomba Serikali iwajengee soko la kisasa wakazi wa Hungumalwa kwa sababu eneo hilo pana biashara kuwa ya dengu, choroko na kunde.