Home Mchanganyiko C-FM YAZINDUA KAMPENI YA ”NISITIRI NINA HAKI YA KUTIMIZA NDOTO ZANGU”

C-FM YAZINDUA KAMPENI YA ”NISITIRI NINA HAKI YA KUTIMIZA NDOTO ZANGU”

0

Balozi wa ”Nisitiri nina haki ya kutimiza ndoto zangu,Usinikekete na usinipe Mimba Utotoni” Msanii wa Muziki wa kizazi kipya Diana Exavery maarufu kwa jina la Malaika,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kutokomeza ukeketaji kwa Mikoa ya Kanda ya Kati inayoratibiwa na Redio hiyo iliyofanyika leo jijini Dodoma

Msimamizi Mkuu  wa vipindi vya Redio ya C-FM,Emmanuel Likuda,akisisitiza jambo kwa  waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kutokomeza ukeketaji kwa Mikoa ya Kanda ya Kati inayoratibiwa na Redio hiyo iliyofanyika leo jijini Dodoma

Balozi wa ”Nisitiri nina haki ya kutimiza ndoto zangu,Usinikekete na usinipe Mimba Utotoni” Msanii wa Muziki wa kizazi kipya Diana Exavery maarufu kwa jina la Malaika,akiwa katika picha ya pamoja na Msimamizi Mkuu  wa vipindi vya Redio ya C-FM,Emmanuel Likuda mara baada ya kuzindua kampeni ya kutokomeza ukeketaji kwa Mikoa ya Kanda ya Kati inayoratibiwa na Redio hiyo iliyofanyika leo jijini Dodoma.

……………………………………………………………………………….

Na. Alex Sonna, Dodoma

Kituo cha Redio C FM Mkoani Dodoma kimezindua Kampeni  ya ”Nisitiri nina haki ya kutimiza ndoto zangu,usinikekete,usinipe mimba utotoni” kwa mtoto wa kike ili waweze kutimiza ndoto zao.

kampeni  hiyo imezinduliwa leo Jijini Dodoma kwa lengo la  kutokomeza ukeketaji kwa Mikoa ya Kanda ya Kati inayoratibiwa  na Redio ya C-FM ya jijini Dodoma na Msimamizi Mkuu  wa vipindi wa Redio hiyo,Emmanuel Likuda .

Likuda ameeleza kuwa kwa mujibu wa ripoti ya  Tanzania Demographic and Health Survey and Malaria (TDHS) kwa mwaka 2015-2016 inaonesha  Mkoa wa Manyara unaongoza  kwa kukeketa wasichana  huku ripoti hiyo ikieleza kuwa wasichana wanaozaliwa au kulelewa na mama aliyekeketwa hukeketwa pia.

“hali ya ukeketaji nchini inaonesha kuwa Mkoa wa Manyara unaongoza kwa ukeketaji  kwa asilimia 58 ukifuatiwa na Dodoma kwa asilimia 47,Arusha asilimia 41,Mara 32 na Singida asilimia 31”, ameeleza Likuda.

Aidha Likuda amesema kuwa ripoti hiyo imefafanua kuwa ukeketaji hufanywa kwa asilimia 86 na mangariba au wakeketaji wa jadi na asilimia 25 hukeketwa  katika umri wa miaka 13 na zaidi.

Vile vile Ripoti hiyo imeeleza kuwa wasichana wanaozaliwa au kulelewa na mama aliyekeketwa hukeketwa pia na kuwa na asilimia 95 ya asilimia 86 ya wanawake waliokeketwa hawakubaliani na kitendo hicho na wanatamani kisiwepo kabisa

Naye Balozi wa kampeni hiyo  Msanii wa Muziki wa kizazi kipya Diana Exavery maarufu kwa jina la Malaika, amesema  madhara ya ukeketaji ni makubwa  kiafya kwa mtoto wa kike  ikiwemo kupata athari za kisaikolojia kama msongo wa mawazo kwani wengi hufanya hivyo bila ridhaa yao.

Pia Balozi huyo ameongeza kuwa Madhara ya afya ya uzazi ambayo hupelekea kuongezeka  kwa vifo vya mama na mtoto  wakati wa kujifungua pia maumivu makali wakati wa kukeketwa,kumwaga damu nyingi,kovu la kudumu sehemu za siri pamoja na kutokufurahia tendo la ndoa.