Home Siasa CHADEMA KUBORESHA BEI YA KAHAWA KWA WAKULIMA WA KAGERA.

CHADEMA KUBORESHA BEI YA KAHAWA KWA WAKULIMA WA KAGERA.

0

Mgombea Urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Tundu Lisu akiongea na wananchi katika uwanja wa Mashujaa wa wilaya ya Missenyi mkoani Kagera kwenye mkutano wa kampeini akiomba kuchaguliwa.

Waendesha pikipiki maarufu Boda Boda wa Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera waliojitokeza kumpokea kwa maandamano na kidedea Mgombea urais wa (CHADEMA)  Tundu Lisu akitokea wilayani Missenyi na kusababisha shughuli kusimama na barabara kufungwa kwa takribani lisaa lizima

Mgombea Urais wa (CHADEMA) Tundu Lisu kushoto akimuombea kura mgombea ubunge wa jimbo la Bukoba mjini Chief Kalumuna kulia aliyenyoosha mikono kwenye mkutano wa Kampeni za chama hicho uliofanyika uwanja wa Gymkhana mjini Bukoba.

Wananchi wa wilaya ya Missenyi waliojitokeza kwenye mkutano wa Mgombea Uraisi wa CHADEMA tundu lisu wakimsikiliza kwa makini akimwaga sera kwenye mkutano wa kampeini.

*************************************

Na Allawi Kaboyo Missenyi.

Mgombea Urais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania kupitia chama cha demokrasia na maendeleo (CHADEMA) Tundu lisu amewataka wananchi mkoani Kagera kukichagua chama chake katika uchaguzi mkuu ujao ili kuweza kutatau changamoto mbalimbali zinazowasumbua wanakagera likiwemo suala la bei ya Kahawa.

Lisu ameyasema hayo kwenye mkutano wake wa kampeini alioufanya septemba 22 uwanja wa mashujaa mjini Bunazi wilayani Missenyi ambapo pamoja na mambo mengine ameeleza endapo wananchi watamchagua na kumpa madaraka kama Rais wa Tanzania atahakikisha suala la kahawa ya Kagera linabaki kuwa historia.

Lisu amesema kuwa wanakagera wamekuwa wakitegemea sana zao la kahawa kama mkombozi wa maisha yao ambapo wazee wa zamani walilitumia zao hilo kuwasomesha watoto wao na kuendesha maisha yao bila utegemezi.

“Sasa hivi kahawa haina thamani tena kwa mwanakagera, unalima mwenyewe unavuna mwenyewe lakini unapangiwa pakuuza na bei yenyewe sio rafiki, huu mkoa unapakana na Uganda ambao wao kahawa yetu wanainunua kwa bei ya juu lakini mkulima akiipeleka anaonekana kama kapeleka magendo, niwombe mnichague haya yote nitakomesha.”Amesema Tundu Lisu

Ameongeza kuwa suala la vitambulisho vya Taifa NIDA vimekuwa kikwazo kikubwa sana ambacho watu wengi ambao pia ni wakulima wa kahawa kushindwa kulipwa fedha zao baada ya kuuza kahawa kutokana na kutosajili namba zao za simu huku kero ikiwa ni vitambulisho hivyo.

Aidha amesema kuwa serikali imekuwa ikiwasumbua wananchi wa mipakani kwa kigezo cha Uraia hali inayowapelekea wananchi hao kuishi kwa woga kwenye nchi yao kutokana na viongozi wanaowaongoza kwenye maeneo yao kuwa wa kuteuliwa na sio chaguo lao.

Kwaupande wake mgombea ubunge jimbo la nkenge kupitia chama hicho Bi Kyai amesema wilaya ya Miseenyi inakabiliwa na kero nyingi ikiwemo migogoro ya ardhi, maji safi na salama, ukosefu wa Barabara upungufu wa walimu kwenye shule za msingi na sekondari ambapo ametumia jukwaa hilo kuwaomba wanankenge kumchagua ili kuweza kusaidia kutatua kero hizo.

Akiwa mjini Bukoba baada ya kupokelewa na maelfu ya watu wa mji huo,Lisu amewaomba watanzania kukichagua chama chake kwa kuwachagua madiwani wabunge na yeye mwenyewe ili kuweza kuwaletea wananchi maendeleo na kusisitiza kuwa wakichaguliwa wataweza kuigawa Tanzania  kwa mfumo wa majimbo hasa upande wa utawala ili kila jimbo liwe na kiongozi wake anayechaguliwa na wananchi husika.

“Mkituchagua sisi CHADEMA tutabadirisha katiba na kuleta katiba mpya, tunataka Tanzania kubadirishwa mfumo mzima wa kiutawala ili kila sehemu ama kila mkoa uwe na kiongozi wake anayetokana na wananchi wenyewe asiwe wa kuteuliwa na Rais, mfano mkuu wa wilaya achaguliwe na wananchi ili akichemka wananchi wenyewe waweze kumuondoa.” Amesema Tundu Lisu.

Septemba 22,mwaka huu Lisu amefanya mikutano ya hadha ya kampeini katika wilaya za Karagwe, Missenyi na Bukoba ambapo anatarajia kuendelea na kampein zake katika maeneo mengine ya mkoa wa Kagera.