Bertrand Traore akiwa ameshika jezi ya Aston Villa baada ya kukamilisha uhamsho wake kutoka Lyon kwa dau la Pauni Milioni 19 PICHA ZAIDI SOMA HAPA
KLABU ya Aston Villa imekamilisha usajili wa mshambuliaji wa kimataifa wa Burkina Faso, Bertrand Traore kutoka klabu ya Lyon ya Ufaransa kwa dau la Pauni Milioni 19.
Mchezaj huyo mwenye umri wa miaka 25 aliyeibukia katika akademi ya Chelsea na kucheza mechi 16 za kikosi cha kwanza msimu wa 2015-16, amesaini mkataba wa miaka mitatu kupiga kazi Villa Park.
Anakuwa mchezaji wa nne mpya baada ya Ollie Watkins kutoka Brentford kwa Pauni Milion 28, zinazoweza kuongezeka hadi Milioni 33, Matty Cash kutoka Nottingham Forest kwa Pauni Milioni 14 na Emiliano Martinez kutoka Arsenal kwa Pauni Milioni 20.
Pamoja na kusajili wachezaji wapya, Aston Villa wiki iliyopita ilompa mkataba mpya wa miaka mitano Nahodha wake, kiungo Jack Grealish ambaye sasa atakuwa analipwa mshahara wa Pauni 135,000 kwa wiki.
Hadi sasa dirisha hili, Aston Villa wametumia Pauni Milioni 84 kusajili wachezaji wapya, wakati msimu ulioptia walitumia Pauni Milioni 143 na wakaishia kunusurika kushuka daraja.
Tangu wamerejea Ligi Kuu misimu miwili iliyopita, Aston Vlla wametumia Pauni Milioni 227 kusajili, kiwango ambacho ni Chelsea na Manchester City pekee wamekivuka kwa kipindi kama hicho.
Matumizi mabaya ya fedha ya Aston Villa ndani ya muda huo, yanafanana kabisa na ya Manchester United.