Home Mchanganyiko Wenye Ulemavu wa Kusikia Manyara, wapewa Elimu ya Utambuzi wa Bidhaa Feki.

Wenye Ulemavu wa Kusikia Manyara, wapewa Elimu ya Utambuzi wa Bidhaa Feki.

0

************************************

Na John Walter-Manyara

Katika kuhakikisha  bidhaa bandia zinadhibitiwa nchini, Tume ya Ushindani  (FCC), imepanga kuyafikia makundi yote maalum kwa njia ya kuwapatia Elimu ya Utambuzi wa bidhaa hizo ili kuepuka kuzitumia.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Udhibiti Bidhaa  bandia  tume ya Ushindani,  Godfrey Gabriel Mshana  kwenye Semina ya watu 50  wenye Ulemavu wa wa Kusikia, iliyofanyika Mjini Babati leo Septemba 17,2020.

Mshana  amesema sambamba na elimu hiyo kwa kundi la Viziwi, njia nyingine wanayoitumia ni kuzuia soko la bidhaa hizo ambazo hazijathibitishwa na Mamlaka husika.

Mshana amesema bidhaa bandia ni changamoto na zinamwathiri kila mmoja  na vita dhidi ya bidhaa hizo  ni mtambuka  hivyo jamii itoe ushirikiano  na tume  ipo tayari kwa ajili ya kupokea malalamiko muda wowote au kituo cha polisi.

“Vita ya bidhaa bandia ni Mtambuka, athari ya bidhaa bandia haichagui hivyo  tunahimiza ushirikiano kwa jamii nzima” alisema Mshana

Ameeleza kuwa Sheria ya alama za bidhaa ni sheria ya Jinai ambapo mtuhumiwa wa makosa hayo anaingia kwenye kesi ya uhujumu uchumi ambapo  adhabu yake ni Kifungo au  faini, kuharibu bidhaa hizo na kuwafidia walioathirika.

Amesema Watu ambao wamebainika  kujihusisha na makosa mbalimbali katika bidhaa ni watu 635  kwa mwaka wa fedha  uliopita  ambao walikuwa wakiingiza bidhaa  hizo bandarini huku katika masoko wakiwa  wafanyabiashara wakubwa zaidi ya 300 katika masoko mbalimbali nchini.

Wametoa elimu hiyo kwa kundi hilo maalum la watu wenye ulemavu wa kusikia ikiwa ni mpango wa tume kuhakikisha kwamba wanayafikia makundi yote ya aina hiyo  ili kuwapatia mbinu ya kutambua bidhaa feki.

Tume inafikisha elimu hiyo kwa wahusika kwa kutumia wataalamu wa kutafsiri  lugha ya alama ambayo ni rahisi kuwafikia walengwa.

Akifungua semina hiyo Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Joseph Mkirikiti,  alisema licha ya kuipongeza tume hiyo kwa kazi kubwa inayoifanya hasa kuyapa elimu makundi ya watu wenye ulemavu lakini alitaka utaratibu huo kuigwa na taasisi, mashirika na watu wengine.

Mkirikiti amesema watu wanaojihusisha na bidhaa bandia wanahitaji kupata faida kubwa ambapo watu wa aina hiyo sio wazalendo wa nchi hii na wanakwepa kodi.