Home Siasa WAENDESHA BODABODA KUSAJILIWA ZANZIBAR ENDAPO DKT.MWINYI AKICHAGULIWA KUWA RAIS VISIWANI HUMO

WAENDESHA BODABODA KUSAJILIWA ZANZIBAR ENDAPO DKT.MWINYI AKICHAGULIWA KUWA RAIS VISIWANI HUMO

0

MGOMBEA Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM Dk.Hussein Ali Mwinyi, akizungumza na Bodaboda wa Mkoa wa Kusini Pemba katika ziara yake ya kutembelea makundi mbali mbali ya kijamii kisiwani Pemba.

********************************

NA IS-HAKA OMAR,PEMBA.

MGOMBEA Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama Chama Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi amewaahidi waendesha pikipiki (bodaboda) kuwa atakapochaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar atahakikisha Wanasajiliwa na kurasimishwa rasmi ili watambuliwe na kupata haki zao  kama wanavyopata wafanyabiashara wengine.

Amesema biashara zote zimerasimishwa hivyo hakuna sababu ya bodaboda hao kutopata fursa hiyo ya kutambuliwa rasmi kisheria.

Kauli hiyo aliitoa wakati akizungumza na bodaboda wa Mkoa wa Kusini Pemba huko katika kiwanja cha Mesi kilichopo Machomanne,katika ziara yake ya kukutana na vikundi mbali mbali vya wananchi.

Aliwambia vijana hao kuwa wakiwa wamoja watapata fursa mbalimbali ikiwemo mikopo ya kibenki na bima za Afya kwani taasisi nyingi za kifedha zinahitaji zikopeshe makundi yenye watu wengi.

“Nimefurahi sana kukutana na nyinyi na kusikia maoni yenu nakuahidini endapo niyachaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar changamoto zenu zitatafutiwa ufumbuzi ili muweze kufanya kazi yenu kwa ufanisi zaidi”, alisema. Dk.Hussein.

Alisema kuwa suala la amani na utulivu ni muhimu hivyo kila mwananchi ana wajibu wa kulinda amani hiyo isitoweke kwa kuepusha nchi isiingie katika machafuko.

Katika maelezo yake Dk.Hussein, aliwambia bodaboda hao kuwa licha ya kunadi Sera za CCM pia anawaombea kura wagombea wote wa CCM kuanzia ngazi za Urais hadi Madiwani.

Mapema akizungumza Mwenyekiti wa Jumuiya ya waendesha Pikipiki (Bodaboda) Mkoa wa Kusini Pemba, Kassim Juma Khamis alisema bodaboda hao wanaomba kupatiwa bima ya afya kwa gharama nafuu ili waweze kupata matibabu pindi wanapopata ajali wakiwa kazini.

Akizungumza kwa niaba ya bodaboda 650 waliopo katika Jumuiya hiyo, Kassim alimuomba Mgombea huyo endapo atakuwa Rais wa Zanzibar asaidie kuzisimamia taasisi za kibenki ziwapatie  mikopo ya pikipiki yenye masharti nafuu.

Alisema Sera,hoja na ahadi za mgombea Urais wa CCM Dk.Mwinyi zimewapa matumaini makubwa bodaboda hao na kwamba watamuunga mkono kwa kumpigia kura zitakazompa ushindi katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.