Home Mchanganyiko DK.CHAULA AFUNGUA MAFUNZO KWA WATENDAJI WA SHIRIKA LA POSTA TANZANIA JIJINI DODOMA

DK.CHAULA AFUNGUA MAFUNZO KWA WATENDAJI WA SHIRIKA LA POSTA TANZANIA JIJINI DODOMA

0

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia sekta ya Mawasiliano, Dk.Zainabu Chaula, akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo  kwa watendaji wa Shirika la Posta Tanzania yanayofanyika jijini Dodoma.

Sehemu ya washiriki wakifatilia hotuba ya Katibu  Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia sekta ya Mawasiliano, Dk.Zainabu Chaula,(hayupo pichani) alipokuwa akifungua  mafunzo  kwa watendaji wa Shirika la Posta Tanzania yanayofanyika jijini Dodoma.

Mtendaji Mkuu wa Shirika hilo, Hassan Mwang’ombe,akitoa taarifa kwa mgeni rasmi  Katibu  Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia sekta ya Mawasiliano, Dk.Zainabu Chaula,wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa watendaji wa Shirika la Posta Tanzania yanayofanyika jijini Dodoma.

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia sekta ya Mawasiliano, Dk.Zainabu Chaula,akiwa kwenye picha mbalimbali za pamoja mara baada ya kufungua  mafunzo  kwa watendaji wa Shirika la Posta Tanzania yanayofanyika jijini Dodoma.

……………………………………………………………………………….

Na.Alex Sonna,Dodoma

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia sekta ya Mawasiliano, Dk.Zainabu Chaula, amefungua mafunzo kwa watendaji wa Shirika la Posta Tanzania, huku akiwataka kuimarisha utendaji kazi wao ili kutoa huduma bora kwa watanzania.

Kauli hiyo ameitoa leo alipokuwa akifungua mafunzo hayo kwa viongozi wa Shirika hilo nchini yanayohusu uongozi na utendaji kazi, Jijini Dodoma.

Amesema kila Meneja wa Mkoa anatakiwa kuweka malengo ya juu ikiwemo kujitangaza zaidi kwa huduma zinazotolewa na shirika hilo.

“Nyie mnajukumu la usafirishaji vitu mbalimbali vya taasisi za umma kwa mfano Wizara ya Afya inawatumia kusafirisha sampuli za damu, sampuli za vitu vingi hadi maabara ya Taifa, “amesema.

Amewataka watendaji hao kufanya kazi kwa bidii ili kupata matokeo mazuri katika kuhudumia jamii na kupata fursa kiuchumi.

“Lazima katika kipindi cha miaka mitano ijayo tufike uchumi wa juu, lakini tutafikaje kama hatuna uwajibikaji wa pamoja wa matokeo, tupo Tanzania ya kidigitali, tunatumia mifumo, anuani za makazi, posta kiganjani hakuna haja ya kukimbizana na daladala, tuma mzigo kwa njia ya posta na utafikishiwa hadi nyumbani wakati unafanya kazi nyingine,”amesema.

Dk.Chaula amelitaka shirika hilo kujiimarisha zaidi kwenye utoaji huduma na kuifanya Tanzania kushika nafasi ya kwanza barani Afrika na ulimwenguni kwa utoaji huduma.

Naye, Mtendaji Mkuu wa Shirika hilo, Hassan Mwang’ombe alisema mafunzo hayo yamewakusanya mameneja wa shirika hilo wa mikoa yote nchini ili kuweka mikakati juu ya kuongoza shirika kwa pamoja.

“Tunatengeneza kitu cha maelewano ya pamoja, kwanini sisi ni viongozi, kitu gani tufanye ili twende mbele, tumekusanyika hapa ili kuangalia majukumu yetu ya kila siku, kila mtu apate kupangiwa majukumu na kuyasimamia ili kupata matokeo chanya,”amesema.

Amesema shirika hilo lina majukumu mbalimbali ya kuwahudumia wananchi, ikiwemo barua, usafirishaji wa nyaraka muhimu(EMS), kaunta na Wakala na kuna taasisi zaidi ya 350 ambazo zinatumia huduma ya posta huku watanzania asilimia 50 wanatumia huduma hizo.

“Posta imejiandaa kiutendaji kazi, Posta ndio tulikuwa wasafirishaji wakubwa wa sampuli za Corona na tumefanya kwa asilimia 100, tulipeleka Dar es salaam ndani ya saa 24,”amesema.

Ameeleza kuwa tayari wamejipanga kwa kuwa na wafanyakazi na pikipiki za kutosha ili  kusafirisha sampuli ambapo ilianza kazi hiyo tangu mwaka 2012.

“Tunafanya kazi kila siku, kadri soko linavyopanuka na sisi tupo tayari kuwahudumia watanzania,tunataka Tanzania iwe kama kijiji, ukienda kwenye mifumo ya posta, unafungua maduka mbalimbali na kununua bidhaa yeyote,”amesema.

&&&&&&&