Home Mchanganyiko TAKUKURU YAMSHIKILIA MTUMISHI BARAZA LA ARDHI KWA RUSHWA 

TAKUKURU YAMSHIKILIA MTUMISHI BARAZA LA ARDHI KWA RUSHWA 

0
Mkuu wa TAKUKURU Mkoani Manyara Holle Joseph Makungu akizungumza mjini Babati na waandishi wa habari.
………………………………………………………………………………………………….
Na Mwandishi wetu, Babati 
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU Mkoani Manyara, inamshikilia mtumishi wa Baraza la ardhi na nyumba Wilaya ya Babati Ruth Reniel Semkuyu kwa kosa la kudaiwa kuomba na kupokea rushwa ya shilingi laki moja kwa mkazi wa mkoa huo ili kukaza hukumu. 
Mkuu wa TAKUKURU Mkoani Manyara, Holle Joseph Makungu akizungumza mjini Babati Septemba 9 amesema Semkuyu anadaiwa kutenda kosa hilo kwenye ofisi ya ardhi. 
Makungu amesema Semkuyu alitenda kosa hilo kinyume cha kifungu cha 15 cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11 ya mwaka 2007.
Amesema awali walipata taarifa kutoka kwa mlalamikaji (jina lihahifadhiwa) ambaye alishinda kesi yake katika moja ya mabaraza ya ardhi ya kata hivyo alifika baraza la ardhi na nyumba Wilaya ya Babati ili kukaza hukumu. 
Amesema alipofika alielezwa amuone Semkuyu ili ampe utaratibu wa kukaza hukumu ambapo Semkuyu alimtaka kutoa shilingi 118,000 kwa madai kuwa ni gharama ya kukaza hukumu. 
“Mwananchi huyu alitilia mashaka kiwango hicho hivyo akafika TAKUKURU na kuelezea malalamiko yake nasi tukabaini kiwango kinachopaswa kutolewa kwa kukaza hukumu ni shilingi 18,000 tuu,” amesema Makungu. 
Amesema walimpa mwananchi huyo shilingi 118,000 na kisha akampelekea Semkuyu ambaye alimpa shilingi 18,000 kwa ajili ya kuzilipia benki kisha arudi na risiti ya malipo huku akibaki na shilingi laki moja. 
“Baada ya kukabidhiwa fedha hizo makachero wetu walimkuta na shilingi 100,000 ambayo alishindwa kujieleza fedha hizo ni za nini na anatarajiwa kufikishwa mahakamani September 9,” amesema Makungu. 
Ametoa rai kwa watumishi wa umma kuridhika na vipato wanavyopata kwa waajiri wao na wananchi watoe taarifa ofisi za TAKUKURU zilizopo karibu au namba ya dharura 113 ambayo wananchi hapaswi kulipa. 
“Wananchi fanyeni hivyo ili kuwaondoa watumishi wachache ambao bado hawaridhiki na kipato halali wanacholipwa na mwajiri,” amesema Makungu.