Home Mchanganyiko SERIKALI YATENGA BILIONI 9.5 KUIMARISHA KARAKANA ZA TEMESA

SERIKALI YATENGA BILIONI 9.5 KUIMARISHA KARAKANA ZA TEMESA

0

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi) Arch. Elius A. Mwakalinga (wa pili kulia) akipewa maelezo kuhusu vitendea kazi vipya vya karakana mara baada ya kuvizindua na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Matengenezo na Huduma za Ufundi Mhandisi Sylvester Simfukwe, kushoto ni Mtendaji Mkuu TEMESA Mhandisi Japhet Y. Maselle na Mwenyekiti wa Bodi ya ya Ushauri ya Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Prof. Eng. Idrissa B. Mshoro. Hafla hiyo imefanyika katika karakana ya Mt. Depot Keko jijini Dar es Salaam.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi) Arch. Elius A. Mwakalinga katikati akikata utepe pamoja na viongozi waandamizi wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA)   kuzindua rasmi vitendea kazi vipya vya karakana katika hafla iliyofanyika karakana ya Mt. Depot Keko jijini Dar es Salaam.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa  Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Y. Maselle akisoma taarifa kuhusu utendaji wa karakana katika hafla ya uzinduzi na usambazwaji wa vitendea kazi vya karakana iliyofanyika karakana ya Mt. Depot Keko jijini Dar es Salaam.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi) Arch. Elius A. Mwakalinga aliyenyoosha mkono akisistiza jambo wakati akikagua vitendea kazi vya karakana katika hafla ya uzinduzi na usambazwaji wa vitendea kazi hivyo iliyofanyika karakana ya Mt. Depot Keko jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Y. Maselle

Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Prof. Eng. Idrissa B. Mshoro akisisitiza jambo wakati akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi na usambazwaji wa vitendea kazi vya karakana iliyofanyika karakana ya Mt. Depot Keko jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya Mameneja wa vituo na mikoa mbalimbali wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) wakimsikiliza Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi) Arch. Elius A. Mwakalinga (hayupo pichani) alipokua akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi na usambazwaji wa vitendea kazi vya karakana iliyofanyika karakana ya Mt. Depot Keko jijini Dar es Salaam.

**********************************

Serikali kupitia Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) imetenga kiasi cha shilingi bilioni 9,538,970,000/= katika bajeti ya mwaka wa fedha 2020/2021   kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya karakana kutoka Mfuko Mkuu wa Serikali (GOT) ili kuboresha na kuimarisha miundombinu na vitendea kazi kwenye karakana kwa aijili ya kukidhi matarajio ya wateja.

Hayo yamebainishwa leo na Mtendaji Mkuu wa Wakala huo Mhandisi Japhet Y. Maselle wakati wa hafla fupi ya uzinduzi na usambazaji wa vitendea kazi vipya vya karakana ambavyo vinatarajiwa kusambazwa katika mikoa 14 nchini.

Awali, akizungumza katika hafla hiyo ambayo imefanyika katika karakana ya MT. Depot iliyopo Keko jijini Dar es Salaam, mgeni rasmi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi) Arch. Elius A. Mwakalinga ameupongeza uongozi na menejimenti ya Wakala kwa kuweza kufanikisha ununuzi wa vitendea kazi hivyo na kuongeza kuwa vitendea kazi hivyo vitaongeza chachu ya utendaji kazi wa karakana za Wakala wa kiasi kikubwa.

“Kupata vitendea kazi ni moja, lakini lakini kuvitumia sasa vile vitendea kazi ili kuleta matokeo chanya kwa wahitaji wa huduma inayotokana na vitendea kazi hivi ndio jambo la msingi” alisema Katibu Mkuu ambapo aliagiza vifaa hivyo visambazwe haraka sana kwa mameneja husika ili vikaanze kazi mara moja. Aliongeza kuwa Wizara imepanga kutengeneza karakana mpya mkoani Dodoma ambayo itakuwa karakana ya mfano kwenye utoaji wa huduma bora na za kisasa zaidi.

“Tukishaitengeneza ile na tukaridhika sasa kwingine kote kutafwatia, na kwa mwaka huu wa fedha tumeshatenga bilioni 3 kwa ajili ya kazi hizo”.

Awali akisoma taarifa kuhusu ununuzi wa vitendea kazi hivyo katika hafla hiyo, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Y. Maselle alisema vitendea kazi hivyo vimegharimu serikali kiasi cha Tsh 430,823,810.23 na vitagawiwa katika mikoa/vituo 14 ambavyo ni

Dar es salaam (Vingunguti), Mtwara, Mara, Simiyu, Kagera, Tabora, Iringa, Rukwa, Manyara, Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Songwe na Same.

“Katika mwaka wa fedha 2019/2020 tulipokea kiasi cha Tsh 2,533,080,000/= kutoka Serikalini kupitia Wizara kwa ajili ya miradi ya maendeleo kwenye karakana”. Alisema Mhandisi Maselle ambapo aliishukuru Serikali kwani kwa  kupitia agizo la Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Kassim Majaliwa (Mb) la kuzitaka taasisi zote zinazodaiwa na TEMESA ziwe zimelipa madeni yao kufikia Julai 30, 2020, kiasi cha Tshs. 771,496,076.39 zimelipwa kati ya Tshs 25,882,593,038/= zilizokuwa zinadaiwa.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya ya Ushauri ya Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Prof. Eng. Idrissa B. Mshoro, akizungumza katika hafla hiyo alisema anaishukuru Wizara ya Ujenzi kwa kuendelea kuhakisha Wakala unaendelea kutoa huduma bora kwa taasisi za Serikali na binafsi hasa katika kugharamia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ya TEMESA.