Home Mchanganyiko NEW LIGHT YAANDAA WATAALAMU WAJAO

NEW LIGHT YAANDAA WATAALAMU WAJAO

0
Mwalimu mkuu wa shule ya awali na msingi New Light ya Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Tumaini Mbise akizungumza kwenye kikao cha wazazi, walezi, wanafunzi na walimu wa shule hiyo. 
Wanafunzi wa shule ya awali na msingi New Light ya Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wakiwa kwenye kikao cha wazazi, walezi na walimu wao.
…………………………………………………………………
Na Mwandishi wetu, Mirerani 
JAMII imetakiwa kutambua kuwa wasomi wanapaswa kuandaliwa ili baadaye wawe na faida kutokana na elimu waliyonayo kwa watanzania wanaowazunguka na siyo kuelimika kisha kutokuwa na msaada. 
Mwalimu mkuu wa shule ya awali na msingi New Light ya Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Tumaini Mbise aliyasema hayo juzi kwenye kikao cha wazazi, walezi, walimu na wanafunzi wa shule hiyo. 
Mwalimu Mbise alisema elimu inapaswa kuwa inalenga matatuzi na siyo kuwa na maarifa mengi yasiyo na ufumbuzi kwa jamii inayowazunguka. 
Alisema kutokana na hilo walimu wa shule hiyo ya New Light wanawajenga misingi bora wanafunzi wao waweze kuwa jamii bora kuanzia sasa na miaka ijayo. 
“Watu hawatakiwi kuwa na mashaka na mtu mwenye elimu kwa kufanya mambo chanya kwani wasomi wanapaswa kuandaliwa ili baadaye wawe na faida kutokana na elimu waliyonayo,” alisema Mbise. 
Alisema elimu inapaswa kuleta mabadiliko chanya kwenye maisha inayozunguka hivyo wanafunzi wao wanawaandaa tangu wakiwa wadogo wakishirikiana na wazazi. 
Katibu wa bodi ya shule hiyo, Oscar Gunewe alisema shule hiyo inafungwa kwa muda wa wiki moja ili kutoa nafasi ya likizo fupi kwa wanafunzi wa shule hiyo. 
Gunewe alisema japokuwa kwenye muhula huu kulitokea janga la corona, lakini walimu wametumia muda wa ziada kufidia masomo waliyokosa wanafunzi hao. 
Mwenyekiti wa kamati ya wazazi wa shule hiyo, George Martin aliwataka wazazi na walezi walipe ada kwa wakati ili fedha hizo ziweze kutumika kwenye matumizi mbalimbali. 
“Kutokana ada mnazozitoa ndiyo mishahara ya walimu inapatikana hapo na kama huna fedha zote muwe mnalipa kidogo kidogo hadi mmalize,” alisema.