Mwenyekiti wa The Desk & Cair Foundation (TDCF), tawi la Tanzania, Alhaji Sibtain Meghjee (wa tatu kutoka kulia) jana akitoa maelezo kwa uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Sekou Toure kuhusu ukarabati wa kisima cha maji cha hospitali hiyo ambacho kimekarabatiwa na taasisi hiyo
Mwenyekiti wa The Desk & Chair Foundation (TDCF) Alhaji Sibtain Meghjee (kushoto) kipokea cheti cha shukurani kutoka kwa kaimu Mganga Mfawishi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza, Sekou Toure, Dr. Engelbert Rauya (kulia) jana.
Baadhi ya watumishi wa hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza, Sekou Toure wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wadau na watumishi wa The Desk & Chair Foundation (TDCF), wa nne kutoka kushoto ni Mwenyekiti wa TDCF, Alhaji Sibtain Meghjee na wa tano ni kaimu Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dr. Engelbert Ruya na katikati ni Katibu wa hospitali hiyo pia Lilian Munisi.Picha zote na Baltazar Mashaka
.Mwenyekiti wa The Desk & Cair Foundation (TDCF), tawi la Tanzania, Alhaji Sibtain Meghjee akihojiwa na baadhi ya waandishi wa habari baada ya kukabidhi mradi wa kisima cha maji kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza, Sekou Toure jana.
**************************************
NA BALTAZAR MASHAKA, Mwanza
HOSPITALI ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza,Sekou Toure, imepata mwarobaini wa changamoto ya upungufu wa maji na gharama ya Ankara za matumizi ya maji baada ya The Desk & Chair Foundation (TDCF), kukarabati kisima cha maji na kuongeza uwezo wa kuhifadhi maji kwa gharma ya sh. milioni 30.5.
Kisima hicho kirefu cha maji kimefungwa mashine ya kusukuma maji kwenda kwenye matenki manne ya kuhifadhi maji yenye ujazo wa lita 10,000 pamoja na kifaa cha kubaini upungufu wa maji kwenye tenki (sensor).
Mwenyekiti wa TDCF, Alhaji Sibtain Meghjee, akikabidhi mradi huo kwa uongozi wa hospitali hiyo jana, alisema ukarabati na uboreshaji wa kisima hicho kwa kufunga pumpu na kuongeza uwezo wa miundombinu ya kuhifadhi maji kwenye hospitali hiyo unaunga mkono juhudi za serikali kwenye sekta ya afya.
Alisema mradi huo utapunguza gharama za malipo ya maji kila mwezi na utaondoa tatizo la maji kwenye hospitali hiyo kutokana uwezo wa miundombinu ya kuhifadhi maji iitakayowezesha upatikanaji wa maji ya uhakika na kufanya huduma za tiba na upasuaji kufanyika bila shida.
Alhaji Meghjee alisema mradi huo umegharimu sh.30,562,000 umeonyesha matokeo chanya ya kushuka kwa gharama za maji baada ya majaribio yaliyofanyika zaidi ya miezi miwili licha ya kuwepo kasoro ya umeme kwenye pumpu ya kusukuma maji na kushauri irekebishwe haraka ili kuepusha mashine hiyo isiungue.
Kwa mujibu wa imani ya madhehebu ya Shia Ithna Sheria sadaka ya maji ni jambo la thawabu kubwa kiimani na kwamba fedha za ukarabati wa kisima hicho zilitolewa na familia ya Virji Albhai kwa ajili ya kumbukumbu ya mtoto wao, marehemu Sabrina Virji Alibhai.
Pia imejenga jengo la CT Scan la vyumba vitano kwenye Hospitali ya Sekou Toure kwa gharama ya sh. milioni 60, vyoo matundu 20 kwa ajili ya wagonjwa na watumishi9 wanaume vyoo vitatu na vinne vya wanawake, imejenga vyoo vinne kwenye eneo la chumba cha kuhifadhia maiti na kuweka tenki la maji la lita 2,000 kwa gharama ya sh. milioni 10.
Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo wa TDCF taasisi hiyo imewahi kutoa msaada wa mashine ya kufulia nguo, mashine ya kupima msukumo wa damu, madawa na vifaa tiba,magodoro zaidi ya 100, vyandarua na mashuka kwa gharama ya sh. milioni 60 hospitalini hapo.
Pia imekuwa mdau mkubwa wa Kituo cha Damu Salama Kanda ya Ziwa, imezilipia familia 200 michango ya NSSF, kuwakatia bima ya afya watoto 370 na kulipia familia 213 zisizojiweza Bima ya Afya iliyobereshwa (ICHIF).
Akizungumza kwa niaba ya serikali na uongozi wa hospitali, Katibu wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza, Sekou Toure, Lilian Munisi , alisema gharama za matumizi ya maji zilikuwa juu ambapo walikuwa wakilipa kati ya sh. milioni 15 hadi 18 kwa mwezi hivyo kisima hicho cha maji kitasaidia kupunguza gharama za matumizi ya maji .
Alisema kwa miezi mitatu (Mei, Juni na Julai) gharama za maji zimeshuka ambapo Julai wamelipa sh. milioni 1.4 kutoka sh. milioni 18 kwa mwezi hivyo kwaa kutumia maji ya kisima wataokoa fedha nyingi ambazo watazitumia kununua dawa na vifaa tiba