Home Siasa BAADHI YA WAGOMBEA WAKOSA SIFA JIMBO LA BUMBULI, JANUARI MAKAMBA APETA

BAADHI YA WAGOMBEA WAKOSA SIFA JIMBO LA BUMBULI, JANUARI MAKAMBA APETA

0
 
Msimamizi wa uchaguzi Jimbo la bumbuli Mkoani Tanga akimkabidhi barua ya utambulisho January Makamba inayomtambua kuwa mgombea pekee aliyepita bila kupingwa katika jimbo hilo
……………………………………………………
Na Mwandishi wetu ,Bumbuli 
Baadhi ya wagombea ubunge wa jimbo la Bumbuli kupitia vyama vya upinzania wamekosa sifa kuendelea kushiriki uchaguzi jimbo la Bumbuli huku Jamuary Makamba aliyekuwa mbunge wa  Jimbo la Bumbuli, wilaya Lushoto Mkoani akikidhi sifa za kuendelea na mchakato wa uchaguzi na hivyo kumfanya kuwa mgombea pekee wa jimbo hilo kwa tiketi ya CCM.
Mgombea mwingine  aliyerudisha fomu, Abubakar Mashambo wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)  kushindwa kuambatanisha picha, hivyo kushindwa kukidhi vigezo katika uwasilishaji wa fomu.
 Akizungumza mara baada ya Msimamizi wa Uchaguzi, Jimbo la Bumbuli, George Haule kumtangaza kuwa mgombea pekee aliyekidhi vigezo, Makamba alisema kuwa amefurahi kuvuka kiunzi hicho lakini amesikitika kutokuwa na mpinzani ambaye angemuwezesha kujipima yeye kama mgombea ubunge na kupima imani ya wapiga kura wa jimbo hilo kwa Chama cha Mapinduzi.
Alisema kuwa mwaka 2015 alipata kura asilimia 84 ya kura zote na Raisi alipata asilimia 86.
Alitoa wito kwa wananchi kujitokeza kupiga kura kwa sababu bado wana jukumu la kuhakikisha Mgombea Urais wa CCM, Dk. John Pombe Magufuli anapita kwa kura nyingi zaidi ya zile alizopata uchaguzi uliopita.
Alisema pia wapo wagombea udiwani kwa kupitia chama hicho ambao wanatakiwa kunadiwa ili CCM ipite kwa kishindo.
Aliahidi kupita kata hadi kata na maeneo yote ya Jimbo hilo na nje ya jimbo kuhakikisha wagombea wa CCM wanapita na Dk Magufuli anapata kura nyingi zaidi ya zile za mwaka 2015.
“Mwaka 2015 wilaya ya Lushoto na Kilindi ziliongoza kwa kura za Rais. Tunataka tuhakikishe tunampa kura nyingi Rais na CCM ili Mkoa wa Tanga uendelee kuwa ngome ya CCM,” alisema Makamba.
Akizungumzia demokrasia, alisema matatizo yanayojitokeza katika uteuzi ambapo wagombea wa vyama vya upinzani wanaondolewa kutokana na kukosa vigezo au kushindwa kukidhi masharti katika kujaza fomu, alisema kuwa Tanzania ina njia ndefu ya vyama hivyo kushiriki kwa usawa kwenye chaguzi za kidemokrasia.
Alisema kuwa vyama hivyo bado vina kazi ya kujifunza katika kushiriki kwa usawa na CCM katika chaguzi za kidemokrasia.
Msimamizi wa Uchaguzi, George Haule alisema kuwa jumla ya wagombea wanne walichukua fomu  ambapo wagombea wa CUF na ACT – Wazalendo hawakurudisha fomu.
Haule alisema kuwa mgombea wa Chadema ameenguliwa kutokana na fomu yake kutokidhi vigezo. Alisema kuwa mgombea huyo wa Chadema fomu yake haikuwa na picha nne zinazotakiwa kuwasilishwa pamoja na fomu hizo, hivyo kuenguliwa. Pia alieleza kuwa saa 24 zilizowekwa kwa wagombea kuweka pingamizi zimepita bila kuwepo na pingamizi lolote na hivyo kumfanya mgombea wa CCM, Makamba kuwa mgombea pekee akiyekidhi vigezo vyote