…………………………………………………….
Na Karimu Meshack
Wananchi wa Ngorongoro wamempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Joseph Magufuli kwa kujenga na kudumisha amani nchini.
Wameyasema hayo wakati wa Kikao na Kamati ya Kitaifa ya Ujenzi wa Amani na Kuzuia Mauaji ya Kimbari kilichofanyika leo katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, Mji mdogo wa Loliondo jijini Arusha.
Katika kikao hicho kilichohusisha viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, Wadau wa Amani ambao ni wakulima na wafugaji katika Wilaya hiyo pamoja na Wataalamu wa Kamati ya Kitaifa ya Amani kimelenga kubaini viashiria au vyanzo vya migogoro inayohusisha rasilimali na kusababisha uvunjifu wa amani ili kuitafutia suluhisho la kudumu kabla haijaleta madhara kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.
“Tunamshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa uongozi wake makini uliojaa busara na hekima na kuwezeha kuwa na amani katika jamii yetu. Siku hizi hatugombani na unaweza kuuza ng’ombe hata 1000 na ukatembea huku umeshika pesa mkononi na ukawa salama jambo ambalo halikuwepo hapo zamani Mbung’ai Ole Sasi.
Kwa upande wake Katibu wa Kamati ya Kitaifa ya Ujenzi wa Amani na Kuzuia Mauaji ya Kimbari Bw. Miraji Maira amewashukuru wadau wa Amani walioshiriki kwa kubainisha viashiria vya migogoro na kuahidi kuyafanyia kazi. Aidha, Katibu Maira amesema amefurahishwa kuona watu wanashuhudia kazi kubwa inayofanywa na Mhe. Rais John Pombe Joseph Magufuli na kuwataka waendelee kumuunga mkono kwa kuendelea kujenga amani katika jamii kwani ni wajibu wao na ikitokea migogoro waitatue kwa njia ya amani.
“Nimefurahi kusikia hamgombani badala yake mnatatua changamoto zenu kwa amani, endeleeni hivyo kwasababu wajibu wa kulinda amani upo mabegani mwenu, hakuna mtu mwingine wa kuwatatulia migogoro yenu” amesema Miraji Maira.
Kamati ya Kitaifa ya Ujenzi wa Amani na Kuzuia Mauaji ya Kimbari iliyoanzishwa Februari, 2012 chini ya itifaki ya Kuzuia Mauaji ya Kimbari na kuridhiwa na serikali ya Tanzania kupitia Mkataba wa nchi za Maziwa Makuu wa Usalama, Utulivu na Maendeleo kesho itaendelea na mkakati wa utekelezaji wa majukumu yake ya msingi ya kujenga na kudumisha amani na utengamano katika mikoa ya Manyara na baadae Rukwa na Morogoro.