Home Mchanganyiko KESI ZA UCHAGUZI KUMALIZIKA NDANI YA MIEZI MINNE

KESI ZA UCHAGUZI KUMALIZIKA NDANI YA MIEZI MINNE

0

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi akifunga awamu ya kwanza ya mafunzo ya namna bora ya uendeshaji wa kesi za uchaguzi kwa baadhi ya Majaji wa Mahakama Kuu leo jijini Dodoma.

……………………………………………………………………………………………….
Na Lydia Churi-Mahakama, Dodoma
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi
amewataka Majaji wa Mahakama Kuu kuwa tayari kusikiliza mashauri
yatakayofunguliwa kutokana na uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi
Oktoba mwaka huu.
Akifunga awamu ya kwanza ya mafunzo ya namna bora ya uendeshaji wa
mashauri ya uchaguzi kwa baadhi ya waheshimiwa Majaji wa Mahakama Kuu ya
Tanzania, Jaji Kiongozi amesema Mahakama itampangia Jaji yeyote kusikiliza
mashauri ya uchaguzi hivyo kila Jaji anapaswa kuwa na hali ya utayari na
kujiandaa kutekeleza wajibu huo muhimu.
“Mafunzo mliyopata yana lengo la kuweka mazingira sahihi ili Jaji yeyote
atakapopangiwa kusikiliza mashauri yatokanayo na uchaguzi Mkuu awe tayari
wakati wote”, alisisitiza Jaji Kiongozi.
Alisema Mahakama imepanga kumaliza mashauri yatakayotokana na uchaguzi
Mkuu wa mwaka huu ndani ya miezi minne (4) kwa kuwa tayari imeshaonesha
mwelekeo wa kuyashughulikia. Aliongeza kuwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka
2015 mashauri ya aiona hiyo yalisikilizwa na kumalizika ndani ya miezi sita (6)
tangu kufunguliwa kwake.
Jaji Feleshi amewataka Majaji Wafawidhi kujiandaa na pia kuhakikisha
wanawaandaa Naibu Wasajili pamoja na Mahakimu ili wawe tayari kusikiliza
mashauri hayo. Kiongozi huyo pia ameagiza mashauri mengine yaliyopo na
yanayoendelea kufunguliwa mahakamani yaendelee kusikilizwa na kumalizika
kwa wakati licha ya kuwepo kwa mashauri yatakayotokana na uchaguzi Mkuu.
Aidha, ametoa wito kwa Majaji wote kuendeleza ushirikiano uliopo baina yao,
kujaliana na kupendana wakati wote kwa kuwa mahakama ni familia.
Mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na
Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) yamesaidia kuwajengea uwezo
Maafisa wa Mahakama na kuwaandaa kutoa haki kwenye mashauri ya Uchaguzi
Mkuu ujao wa Rais, Wabunge na Madiwani.
Mafunzo yaliyomalizika leo yaliwahusisha baadhi ya Waheshimiwa Majaji wa
Mahakama Kuu ya Tanzania. Awamu inayofuata pia itawahusisha Majaji wengine

wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Jumatatu Agosti 24 yataanza mafunzo hayo
kwa Wasajili, Naibu Wasajili na Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa Mahakama za
Hakimu Mkazi.
Mafunzo haya pia yatatolewa kwa waheshimiwa Majaji wa Mahakama ya Rufani
kuanzia Septemba 2-4, 2020 mkoani Morogoro. Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa
Mahakama za Wilaya nao watapatiwa mafunzo hayo baadaye katika Chuo cha
Uongozi wa Mahakama Lushoto-Tanga.
Wawezeshaji wa mafunzo hayo ni baadhi ya Majaji wa Mahakama ya Rufani na
Mahakama Kuu waliopo na wastaafu, Naibu wasajili, Mahakimu pamoja na
wawezeshaji kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na Tume ya
Kurekebisha Sheria ambao ni wadau muhumu katika masuala ya Uchaguzi.