Home Mchanganyiko DCPC yapata viongozi wapya

DCPC yapata viongozi wapya

0

Meneja Uhusiano wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Taifa (NHIF), Angela Mziray akizungumzia mbele wa Waandishi wa Habari Wanachama wa Klabu ya Waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam (DCPC) wakati wa mkutano mkuu na uchaguzi mkuu wa viongozi.

Waandishi wa Habari wanachama wa DCPC wakiwa katika picha ya pamoja na wawakilishi kutoka NHIF baada ya kufunguliwa mkutano mkuu wa klabu hiyo mwishoni mwa wiki.

*******************************

NA MWANDISHI WETU
KLABU ya Waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam (DCPC), imefanikiwa kupata viongozi wapya ambao watahudumu miaka mitatu kwa mujibu wa Katiba.
Viongozi hao wamepatikana kupitia uchaguzi uliofanyika Agosti 15, 2020 katika Ukumbi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ilala na kusimamiwa na Wakili
wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Arettas Kyara kutoka Global Advocates co.
Akizungumzia kabla ya uchaguzi kuanzia msimamizi wa uchaguzi alitaja nafasi zinazogombewa kuwa ni Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu, Katibu Msaidizi, Mwekahazina, Mwekahazina Msaidizi na Wajumbe Sita.
Kyara alisema uchaguzi huo unafanyika kwa mujibu wa Katiba ambapo nafasi zote zilipata wagombea kasoro nafasi ya Mwekahazina Msaidizi.
Aliwataja wanachama wa DCPC ambao wamejitokeza kugombea uongozi kuwa ni Irene Mark, Angela Mang’enya na Paul Maregesi waliomba nafasi ya uenyekiti ambapo Irene Mark alifanikiwa kushinda.
“Katika nafasi ya Makamu Mwenyekiti waliomba ni Chalila Kibuda na John Livoti na Chalila aliibuka mshindi. Katibu Mkuu alikuwa mgombea mmoja Hussein Siyovelwa na amefanikiwa kushinda na Katibu Msaidizi aligombea Fatma Jalala ambaye pia ameshinda,” alisema Kyara.
Alisema nafasi ya Mwekahazina walijitokeza watu wawili ambao ni Arodia Peter na Patricia Kimelemeta na Kimelemeta kuibuka mshindi.
Msimamizi huyo wa uchaguzi alisema nafasi ya Wajumbe wa Kamati ya Utendaji ambapo walipaswa kuwa sita waliomba watu sita ambao ni Christina Gauluhanga, Cecilia Jeremia, Shabani Matutu, Selemani Msuya, Tausi Mbowe na Kamugisha Muchunguzi na wote walishinda hivyo kuwa wajumbe wa kamati ya utendaji.
Kyara alisema uchaguzi huo ulikuwa wa kidemokradia, huru na haki hivyo ni matumaini yake kuwa viongozi waliochaguliwa watafanya kazi vizuri kujenga DCPC.
Akizungumza baada ya uchaguzi Mwenyekiti mpya wa DCPC Irene Mark aliwaahidi wanachama uongozi uliotukuka, kujituma, ushirikiano na ubunifu kuhakikisha klabu inafikia malengo iliyojiwekea.
Mark alisema DCPC inapaswa kuwa mfano wa kuigwa na klabu nyingine nchini kutokana na wingi wa waandishi waliopo Dar es Salaam jambo ambalo ameahidi kulisimamia.