Home Mchanganyiko BILIONI 100 KUPELEKA UMEME PEMBEZONI MWA MIJI

BILIONI 100 KUPELEKA UMEME PEMBEZONI MWA MIJI

0

Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (katikati), akisisitiza jambo kwa wataalamu aliofuatana nao katika ziara yake kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme, wilayani Arusha, Agosti 16, 2020. Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dkt Tito Mwinuka na kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Amos Maganga. Wa pili kutoka kushoto ni Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga.

Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani, akiwahamasisha wananchi wa Mtaa wa Bondeni Kati, Kata ya Terrat, wilayani Arusha, kulipia shilingi 27,000 tu ili waunganishiwe umeme. Waziri alikuwa katika ziara ya kazi wilayani Arusha, kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme

Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (katikati), akikata utepe kabla ya kuwasha rasmi umeme katika Shule ya Sekondari Moivaro, wilayani Arusha, Agosti 16, 2020. Wa pili kutoka kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Kenan Kihongoji.

Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (katikati), akiwakabidhi Waandishi wa Habari, Mkoa wa Arusha, vifaa vya Umeme Tayari (UMETA), ili waunganishiwe katika nyumba zao. Waziri alikuwa katika ziara ya kazi kukagua miradi mbalimbali ya umeme wilayani Arusha

Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Kenan Kihongoji akizungumza, wakati wa hafla fupi ya kuwasha umeme katika Shule ya Sekondari Nyahiri Terrat. Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (kulia-Meza Kuu) ndiye aliwasha rasmi umeme katika Shule hiyo akiwa katika ziara ya kazi

Mwonekano wa Jengo lenye baadhi ya vyumba vya madarasa katika Shule ya Sekondari Nyahiri Terrat, wilayani Arusha, baada ya kuwashiwa rasmi umeme na Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani, akiwa katika ziara ya kazi

Sehemu ya umati wa wananchi wa Kata ya Terrat, wilayani Arusha, wakimsikiliza Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (hayupo pichani), alipokuwa akizungumza nao, muda mfupi kabla ya kuwasha rasmi umeme katika Shule ya Sekondari Nyahiri Terrat

Baadhi ya Wafanyakazi wa TANESCO wakimsikiliza Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (hayupo pichani), alipokuwa akizungumza  katika hafla ya kuwasha rasmi umeme katika Shule ya Sekondari Nyahiri Terrat, wilayani Arusha

……………………………………………………………….

Veronica Simba – Arusha

Serikali imetenga shilingi bilioni 103.8 kwa ajili ya kupeleka umeme katika maeneo yaliyo pembezoni mwa majiji, mikoa, manispaa na miji, nchi nzima.

Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani, alibainisha hayo kwa nyakati tofauti, Agosti 16, 2020 alipokuwa katika ziara ya kazi wilayani Arusha.

Akizungumza muda mfupi kabla ya kuwasha umeme katika Shule ya Sekondari Moivaro na baadaye Shule ya Sekondari Nyahiri Terrat, Dkt Kalemani alisema kuwa Serikali inaendelea kuwaunganishia umeme wananchi wa maeneo ya aina hiyo nchini kote kwa gharama ya shilingi 27,000 tu kama ilivyo kwa vijijini.

Alisema, Mpango huo wa Serikali ni kutokana na uhalisia kuwa maeneo hayo kwa kiasi kikubwa, yanashabihiana na yaliyoko vijijini, ambapo asilimia kubwa ya wakazi wake wana kipato kidogo.

“Tulikaa tukaona maeneo haya yaliachwa muda mrefu bila kuwa na miundombinu ya umeme. Tukaona tuwapunguzie gharama kutoka mlivyokuwa mnalipa zamani shilingi 177,000 na katika baadhi ya maeneo 380,000 hadi shilingi 27,000 tu.”

Akizungumzia Wilaya ya Arusha, Waziri Kalemani alisema kuna mitaa takribani 26 iliyo pembezoni mwa Mji na kwamba Serikali ilianza kuipeleka umeme kutoka mwaka 2018.

Alimpongeza Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Arusha, Mhandisi Herin Muhina, kwa kazi nzuri anayoifanya na kumwagiza atumie muda wa miezi mitatu kuanzia hivi sasa, kukamilisha kazi ya kupeleka umeme katika mitaa yote iliyo pembezoni mwa Mji, ambayo haijafikiwa na huduma hiyo.

Aidha, Waziri alikiri kufurahishwa na Uongozi wa Shule ya Sekondari Moivaro kuona umuhimu wa kulipia gharama za kuunganishiwa umeme na kupata huduma hiyo, ikiwa na mwaka mmoja tu tangu ianzishwe.

Alitoa rai kwa viongozi wengine katika maeneo mbalimbali nchini, kuiga mfano huo kwa kuhakikisha taasisi zote za umma zinapewa kipaumbele katika kuunganishiwa umeme ili kuongeza tija katika utoaji huduma kwa wananchi.

Kuhusu suala la wananchi kulipia nguzo ili waunganishiwe umeme, Dkt Kalemani aliendelea kusisitiza msimamo wa Serikali kuwa ni marufuku kwa kitendo hicho na alitoa tahadhari kwa yeyote atakayebainika kwenda kinyume na maagizo hayo, atachukuliwa hatua kali.

Alisisitiza wananchi kuendelea kulipia huduma ya umeme pasipo kusubiri nguzo akisema hilo siyo jukumu lao. “Wewe lipia kisha udai umeme,” amesisitiza.

Katika hatua nyingine, Waziri aligawa vifaa vya Umeme Tayari (UMETA) kwa waandishi wa habari wa Mkoa wa Arusha, ikiwa ni ishara ya kuthamini mchango wao kwa Taifa kupitia kazi wanayoifanya katika kuhabarisha na kuelimisha jamii juu ya masuala mbalimbali, yakiwemo ya sekta ya nishati.

Aidha, aligawa vifaa hivyo kwa shule alizoziwashia umeme pamoja na walimu wake huku akielekeza kuwa vitumike kuwaunganishia umeme wa gharama nafuu ambao haulazimu kutandaza mfumo wa nyaya katika jengo husika.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Kenan Kihongoji, alimpongeza Waziri Kalemani kwa uchapakazi wake hususan katika kuhakikisha wananchi wa maeneo mbalimbali nchini kote, wanapata huduma ya umeme.

“Uchapakazi wako unadhihirisha kwa vitendo kuwa unamuunga mkono Rais wetu mpendwa, Mheshimiwa John Magufuli katika kuwatumikia Watanzania ili kuhakikisha wanajipatia maendeleo ya kiuchumi.”

Katika ziara hiyo, Waziri aliambatana na viongozi mbalimbali akiwemo Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dkt Tito Mwinuka, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Amos Maganga na wataalamu wengine mbalimbali kutoka wizarani na taasisi hizo.