Home Mchanganyiko TANNA-MLOGANZILA WAFANYA UCHAGUZI WA VIONGOZI

TANNA-MLOGANZILA WAFANYA UCHAGUZI WA VIONGOZI

0

Mjumbe wa Tume ya Uchaguzi-TANNA Taifa, Bi. Kulwa Kaombwe (kushoto) akiwa na Katibu wa Tume ya Uchaguzi Hospitali ya Taifa Muhimbili- Mloganzila, Sr. Kanaeli Uriyo wakiwasikiliza wagombea wa nafasi mbalimbali wakijinadi wakati wa kuomba kura.

Bi. Mpoki Senje akijinadi wakati wa kuomba kura katika nafasi ya katibu
mwenezi wa chama hicho.

Baadhi ya wanachana wa TANNA-Mloganzila wakisikiliza sera za wagombea
wakijinadi wakati wa kuomba kura.

Msimamizi wa Uchaguzi kutoka TANNA-Taifa, Bi. Jema Kajange na viongozi wa kamati ya uchaguzi MNH-Mloganzila wakihesabu kura.

Mwenyekiti wa Uchaguzi MNH-Mloganzila Bw. Julius Hhara akitangaza matokeo ya kura zilizopigwa kwa wagombea wa nafasi mbalimbali.

Viongozi wa TANNA-Taifa katika picha ya pamoja na viongozi wa TANNA-
tawi la MNH-Mloganzila.

……………………………………………………………..
Wajumbe wa Chama Cha Wauguzi Tanzania (TANNA) tawi la Hospitali ya Taifa
Muhimbili- Mloganzila wamefanya uchaguzi rasmi wa viongozi kujaza nafasi nane
katika ngazi ya mwenyekiti, katibu, mweka hazina, katibu mkuu mwenezi pamoja
na wasaidizi wao lengo ikiwa ni kupata viongozi watakaosaidia kuendesha tawi
hilo jipya lenye wanachama takribani 200.
Kati ya vipaumbele vilivyonadiwa ni pamoja na kuboresha sera za kusimamia
utendaji kazi wa wauguzi, kuitangaza vema taaluma hiyo, kudumisha umoja na
ushirikiano baina yao na watumishi mbalimbali kuanzia ngazi ya chini yaani
kwenye vitongoji hadi kimataifa na kuielimisha jamii juu ya majukumu na
mchango wao katika kutoa huduma bora.
Akizungumza wakati wa uchaguzi huo Mjumbe wa Tume ya Uchaguzi-TANNA
Taifa ambaye pia kitaaluma ni Afisa Muuguzi Mwandamizi, Bi. Kulwa Kaombwe
amesema taaluma ya uuguzi inahitaji ushirikiano sana baina ya wauguzi na Serikali
au waajiri wao ili kuwawezesha kutoa huduma bora kwa jamii.
“Ili taaluma hii izidi kusonga mbele na kuwawezesha wauguzi kufanya kazi kwa
ufanisi inahitaji wauguzi kushirikiana bega kwa bega na waajiri wao ili
kuwawezesha kutoa huduma bora kwa jamii” amesema Bi. Kaombwe.
Aidha Bi. Kaombwe ameushukuru uongozi uliopita kwa kusimamia vizuri tawi
hilo kwa kipindi cha miaka miwili tangu kuanzishwa kwake mwaka 2018 likiwa na
idadi ya wanachama hai 55.
Kwa upande wake Mwenyekiti aliyechaguliwa kuongoza tawi hilo, Bw. Wilson
Fungameza amewashukuru wajumbe kwa kumchagua kuongoza nafasi hiyo na
kutoa rai kwa wanachama, viongozi wenzake pamoja na Uongozi wa TANNA-
Taifa kushirikiana kwa ajili ya kusongesha mbele gurudumu la taaluma ya uuguzi.
Miongoni wa majukumu ya viongozi hao ni pamoja na kutunza kumbukumbu za
wanachama, kuhamasisha wauguzi kujiunga na chama, kusimamia mapato na
matumizi ya chama ambayo yanatokana na michango ya kila mwezi ya
wanachama, wafadhili na marafiki wenye mapenzi mema na chama hicho.