Home Mchanganyiko RAIS MAGUFULI ATOA MILIONI 500 KWA AJILI YA MIRADI MIWILI MKOANI TABORA...

RAIS MAGUFULI ATOA MILIONI 500 KWA AJILI YA MIRADI MIWILI MKOANI TABORA –KUSAYA

0

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bwana Gerald Kusaya akitia saini kitabu cha Wageni mara baada ya kupokelewa na Mwenyeji wake Mkuu wa mkoa wa Tabora, Dkt. Philemon Sengati,  mwengine ni Dkt. Geoffrey Mkamilo, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Mazao ya Kilimo (TARI).

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bwana Gerald Kusaya akishuhudia namna mzani unavyopima robota la tumbaku iliyotoka kwenye Vyama vya Kuuza Mazao (AMCOS) mbalimbali baada ya kupokelewa katika ghala la tumbaku la Kampuni ya JTI, mjini Tabora

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bwana Gerald Kusaya akiangalia sampuli ya tumbaku iliyopokelewa kabla ya kuanza zoezi la ununuzi katika ghala la Kampuni ya JTI ambayo imekuwa ikinunua tumbaku kutoka kwenye Vyama Vikuu vya Ushirika mkoani Tabora.

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bwana Gerald Kusaya akishuhudia zoezi la ununuzi wa marobota ya tumbaku katika ghala la Kampuni ya JTI anayemuelezea ni Bwana Albert Chale Mteuzi Mkuu wa zao la tumbaku kutoka Bodi ya Tumbaku Tanzania

 …………………………………………………………………

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bwana Gerald Kusaya ametembelea mkoa wa Tabora kwa ajili ya kukagua na kujionea shughuli za maendeleo ya Sekta ya Kilimo hususan tasnia ndogo ya zao la tumbaku na kumwambia Mkuu wa mkoa wa Tabora Dkt. Philemon Sengati kuwa mkoa wake umepata upendeleo wa kupata zaidi ya milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa miradi miwili.

Katibu Mkuu Kilimo Bwana Kusaya amesema fedha hizo zitakwenda katika Halmashauri ya wilaya ya Nzega Mjini na Nzega vijijini ambapo maeneo yatakayonufaika na pamoja na kijiji cha Idudumo (Nzega Mjini) na kijiji cha Busondo (Nzega Vijijini).

Awali katika taarifa yake ya maendeleo ya Sekta ya Kilimo; Mkuu wa mkoa wa Tabora Dkt. Philemon Sengati amemwambia Katibu Mkuu Kusaya kuwa uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara umekuwa mzuri licha ya kukabiliwa mabadiliko ya tabia nchi na kuiomba Wizara isaidie katika utaalam na mbegu bora na zenye kutoa matokeo mazuri kwenye maeneo yenye ukame.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Kilimo Bwana Kusaya amemwambia mwenyeji wake kuwa Wizara inafanya kazi karibu na Watendaji wengi wa mkoa wa Tabora ambapo, jana tarehe 12 Agosti, 2020 alitembelea Halmashauri ya Wilaya ya Nzega mjini na vijijini kwa ajili ya utekelezaji wa miradi miwili mikubwa.

Katibu Mkuu Kusaya aliutaja mradi wa kwanza ni ukarabati wa miundombinu ya skimu ya uwagiliaji katika kijiji cha Idudumo Halmashauri ya wilaya ya Nzega mjini ambapo Katibu Mkuu Bwana Kusaya alisema Wizara imetenga kiasi cha shilingi milioni 100 (100,000,000) ambapo zitatumiaka kuanza ukarabati na ujenzi wa mifereji ya Bwawa.

Mradi mwengine ni ujenzi wa ghala ya kuhifadhia mazao ya kilimo; Ghala hilo lina uwezo wa kuhifadhi tani 2,000. Katibu Mkuu Kusaya amesema Halmashauri ya Nzega vijijini imepata fursa hiyo baada ya Mhe. Rais wa Awamu ya Tano, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kutoa kiasi cha shilingi bilioni 80 kupitia Mradi wa Kudhibiti Changamoto ya Sumukuvu (TANPAC).

Katibu Mkuu Kusaya ameongeza kuwa fursa ya kujengewa maghala hayo imetoka kwenye Mradi wa Kudhibiti Sumukuvu (TANPAC) ambapo jumla ya Halmashauri 12 za Tanzania Bara na mbili (2) za Zanzibar zimenufaika kwa ujenzi huo wa maghala.

Katibu Mkuu Bwana Gerald Kusaya amemwambia Mkuu wa mkoa wa Tabora, Dkt. Philemon Sengati kuwa jana jioni alipitia ili kujionea eneo hilo katika kijiji cha Idudumo na kijiji cha Busondo na kukagua maeneo hayo yote. Katika Kijiji cha Busondo jumla ya Wanakijiji 22 wakiongozwa na Mwenyekiti wa Serikali ya kijiji Bwana Mustafa Kasalu Maganga pamoja na Katibu Tawala wa kijiji hicho Bwana Laurent Mtunga Iholong’wa waliridhia na kutoa hekari 5 kwa ajili ya ujenzi huo ambao unataraji kuanza mwezi Disemba, 2020.

Akiongea kwa niaba ya Wanakijiji wenzake Bibi Easter Msafiri amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kuleta Mradi huo kwa wanakijiji wenzake.

“Napenda kuishukuru Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuona umuhim wa kutuletea Mradi mkubwa kama huu; Hatukuwa na Mradi kama huu hapo kabla”. Amekaririwa Bi. Easter Msafiri, mkazi wa kijiji cha Busondo.