Home Mchanganyiko WANANCHI WAFURAHIA UJENZI KUENDELEA

WANANCHI WAFURAHIA UJENZI KUENDELEA

0

…………………………………………………………………….

Na Mwandishi wetu Mihambwe

Wananchi wa Kijiji cha Mitondi A kilichopo kata ya Kitama wamefurahishwa na kitendo cha mradi wa ujenzi wa ofisi ya Kijiji chao kuendelea kwani kilikuwa kilio na kiu yao ya siku nyingi kuona mradi unakamilika.

“Ukamilifu wa ofisi hii ilikuwa kilio chetu cha siku nyingi kwani sisi tunajua hela ya kujenga ilitolewa lakini ujenzi ulikwama kwa muda. Tunaishukuru Serikali yetu ya sasa kusimama nasi kidete hatimaye ujenzi unaendelea na sasa tupo hatua ya upauaji.” alisema Rajabu Nayama mkazi wa Kijiji cha Mitondi A.

Ndugu Hamis Mohamed Adam, Mwenyekiti kitongoji cha Chimbuko amemshukuru Afisa Tarafa Mihambwe Emmanuel Shilatu kwa kusimama kidete hadi leo hii ujenzi unaendelea.

“Tunamshukuru sana Afisa Tarafa Mihambwe kwa kuwa upande wetu kutatua kero yetu hii kwa kudai Mabati, Mbao na Misumari ambayo hatukutegemea kama tungeweza kupata tena, tulijua tumeshaliwa. Hatuwezi kuacha kumshukuru kwa mradi huu wa ujenzi kuweza kuendelea leo hii.” Alisema Ndugu Hamis Mohamed Adam ambaye ni Mwenyekiti kitongoji cha Chimbuko.

Hayo yamejitokeza kwenye mwendelezo wa ziara ya Afisa Tarafa Mihambwe Emmanuel Shilatu ya kukagua ujenzi miradi ya kimaendeleo ambapo aliwasisitiza Wajumbe kamati ya ujenzi kusimamia ipasavyo ujenzi huo mpaka ukamilike pasipo kujitokeza hali ya kukwama tena.

“Ujenzi huu ulisimama tangu mwaka 2016 huku kwenye makaratasi unaonyesha umekamilika lakini kiuhalisia ni tofauti, ilikuwa kero na kilio kikubwa kwa Wananchi wa Kijiji cha Mitondi A. Tumepambana vifaa vilivyoyeyushwa kama Bati 70, Mbao, Misumari na vifaa vinginevyo vya umaliziaji ujenzi vikarudishwa na tukafanikiwa kupata fedha ya kuendelea na ujenzi wa mradi. Nawasisitiza Wajumbe wa Kamati kutorudia makosa yaliyojitokeza nyuma, simamieni mradi huu ukamilike na uanze kutumika mara moja.” Alisisitiza Gavana Shilatu wakati akizungumza na Wajumbe wa Kamati ya ujenzi na Wajumbe wa Halmashauri ya Serikali ya Kijiji cha Mitondi A.

Mradi wa ujenzi wa ofisi ya Kijiji cha Mitondi A ulianza mwaka 2010 na kusimama mwaka 2016 na hatimaye umeweza kuendelea tena Agosti 2020.

Katika ziara hiyo Gavana Shilatu alipokelewa na Wajumbe Halmashauri ya Serikali ya Kijiji ambapo alikagua maendeleo ya ujenzi na kisha kuzungumza na Wananchi waliojitokeza kwenye ziara hiyo.