Home Mchanganyiko MOROGORO DC YAONA FURSA USMJ VIJIJINI

MOROGORO DC YAONA FURSA USMJ VIJIJINI

0
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Rehema Bwasi akizunguza na waandishi wa habari ofisini katika mji wa Mvuha kwake kuhusu fursa zilizopo katika  Usimamizi Shirikishi wa Misitu ya Jamii (USMJ)
(PICHA NA JOHN BUKUKU-MOROGORO)
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Rehema Bwasi akipokea majarida mbalimbali kutoka kwa Bettie Luwuge kutoka Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG).
Bettie Luwuge kutoka Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG) akimuonesha vipeperushi na majarida mbalimbali yanayoelezea mradi wa utuzaji shirikishi wa mazingira Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Rehema Bwasi.
Bettie Luwuge kutoka Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG) akiwa na baadhi ya waandishi wa habari katika ofisi za Halmashauri ya wilaya ya Morogoro.
Ofisa Maliasili wa wilaya hiyo Waida Salim akielezea jambo katika kikao cha kamati za utunzaji wa Misitu katika kijiji cha Matuli.
Afisa Mtendaji wa kijiji cha Matuli ambako mradi unatekelezwa akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufika katika kijiji hicho.
Bettie Luwuge kutoka Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG) akiwa na baadhi wanakamati za utunzaji shirikishi wa misitu katika kijiji cha Matuli.
Mmja wa wananchi akielezea faida za utunzaji wa Misitu na baadhi ya changamoto wanazukumbana nazo.
Elida Fundi Elida Fundi  Afisa Uragibishi kutoka shirika la Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG) akitoa ufafanuzi jambo katika kikao hicho kilichofanyika kijiji cha Matuli.
…………………………………………………………….
MKURUGENZI wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Rehema Bwasi, amesema kutokana na fursa zilizopo katika  Usimamizi wa Shirikishi wa Misitu ya Jamii (USMJ) wameamua kusambaza fursa hiyo katika vijiji vipya vitano.
Bwasi aliyasema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari ambao wapo katika ziara ya kuangalia  faida na changamoto zilizopo kwenye Mradi wa Kuleta Mageuzi katika Sekta ya Mkaa Tanzania (TTCS), ambao umetekelezwa kwenye vijiji vitano vya halmashauri hiyo.
Alisema mradi wa TTCS umeonesha matokeo chanya katika vijiji vitano vya Matuli, Diguzi, Lilongwe, Mlilingwa na Tununguo hivyo katika bajeti ya 2020/2021 wataanza kutekeleza vijiji vipya vitano.
“Mafanikio ambayo tumeyapata kwenye vijiji vitano vya awali tunataka tuhamishie kwa vijiji vipya vya Rumba Chini, Sesemba, Kiropa na Pangawe  ambapo kuna misitu ya asili,” alisema.
Alisema dhamira yao ni kuona wananchi wanapata maendeleo kupitia rasilimali zao na misitu imeonesha matokeo chanya kwa wananchi wengi wenye misitu.
“Kutokana na maendeleo ambayo wilaya pamoja na wananchi hao imeyapata kutokana na mradi huu, mkakati uliopo ni kuwepo kwa mradi wa aina hiyo katika vijiji vingine hasa kwa kuzingatia Wilaya ya Morogoro imejaaliwa kuwa na eneo kubwa la misitu ya asili,” alisisitiza.
Mkurugenzi huyo alisema USMJ imechochewa na Shirika la Kuhifadhi wa Misitu ya Asili Tanzania (TFCG) na Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA), kupitia TTCS hivyo wanaamini kuanzisha vijiji vipya ni uamuzi wa kuwaunga mkono wadau.
“Kama mnavyofahamu halmashauri yetu ya Wilaya ya Morogoro imebarikiwa kuwa na misitu mingi ya asili , na misitu hii kwa kiasi kikubwa iko chini ya uhifadhi lakini vile vile inamilikiwa na vijiji, kwa hiyo nichukue fursa hii kushukuru TFCG na MJUMITA, wameweza kushirikiana na halmashauri yetu na vijiji vyetu vitano.
“Katika kuimarisha na kuzalisha mkaa asili kama tunavyofahamu shirika hili uwepo wake katika halmashauri yetu umeweza kutengeneza tija kubwa kwa halmashauri na wananchi wa vijiji ambavyo vinafanya kazi na shirika hili,” alisema. 
Alisema mbali na uhifadhi wa asili kama shirika lenyewe dhima yake, lakini uwepo wa shughuli hiyo ya mkaa endelevu katika halmashauri yetu kumeleta maendeleo makubwa kwa wananchi wetu.
“Kwa kweli haijawahi kutokea kuwepo na mkaa endelevu katika halmashauri yetu, vijiji hivyo vitano vimeweza kujipatia fedha nyingi sana,  kwa mfano kijiji kimoja kimepata zaidi ya shilingi milioni 100, ni kitu ambacho kwa kweli hakijawahi kutokea miaka yote ya nyuma.
Kuwepo na shughuli ya uzalishaji mkaa endelevu kumepanua wigo mkubwa, kwanza kujikusanyia mapato ya kutosha, ambapo mapato hayo yapo chini ya vijiji ambavyo vinatekeleza mradi huo,” aliongeza.
Pia alisema kumekuwepo na mpango wa matumizi bora ya ardhi ambao umesaidia kutengeneza wigo wa kuandaa mipango bora ya matumizi ya ardhi.
Kwa upande wake Ofisa Maliasili wa wilaya hiyo Waida Salim, alisema mradi wa TTCS, umeleta mapinduzi maakubwa katika vijiji husika hivyo baada ya kutoa elimu zaidi vijiji vingine vipya vimeonesha uhitaji.
Salim alisema rasilimali misitu ikitumiwa katika mipango sahihi inauwezo wa kubadilisha maisha ya jamii husika huku uhifadhi ukiimarika zaidi.
“Misitu ni uhai na maendeleo iwapo jamii itaamua kuitumia vizuri na hapa kwetu tumethubutu na tumeweza sasa ni wakati wa kuhamishia mafanikio haya na matunda yanaonekana Matuli, Mlilingwa, Diguzi na kwingineko,” alisema.
Naye Sadiki Kondo ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Maliasili katika Kijiji cha Matuli, alisema USMJ ni fursa ambayo ilijificha kwa muda mrefu hivyo wanaitumia vizuri kuchochea maendeleo.
Alisema wananchi wa kijiji chao kwa sasa ni walinzi wa rasilimali misitu kutokana na manufaa ambayo yametokana na USMJ.