Home Mchanganyiko AFISA TARAFA ITISO ATOA ELIMU KWA VIONGOZI WAKE WA KIJIJI KUPATA UELEWA...

AFISA TARAFA ITISO ATOA ELIMU KWA VIONGOZI WAKE WA KIJIJI KUPATA UELEWA JUU YA KILIMO

0

………………………………………………………………..

Afisa Tarafa Itiso, Wilaya ya Chamwino – Mkoani Dodoma Bw. Remidius Emmanuel katika kipindi cha Maonyesho ya Nane Nane kwa mwaka 2020 ni miongoni mwa watu waliogeuka kivutio na gumzo kwa wengi kutokana na ubunifu wake alioonyesha katika maonyesho hayo.

Katika maonyesho hayo kiongozi huyo alionekana kivutio kufuatia muonekano wa idadi ya watu alioambatana nao katika maonyesho hayo, walioonekana wakimfuata nyuma kutoka eneo moja kwenda jingine.
Kiongozi huyo aliambatana na Wenyeviti wa Vijiji, Watendaji wa Vijiji na Kata, Maafisa Ugani wa Vijiji na Kata pamoja na uwakilishi wa makundi ya Wafugaji na wakulima wote kutoka Tarafa ya Itiso jambo ambalo halijazoeleka kufanywa na viongozi wengi.

“Sio suala lililozoeleka kumuona kiongozi wa namna hii kuambatana na viongozi kutoka eneo lake na ukizingatia Tarafa hiyo iko umbali wa zaidi ya Km 90 kutoka eneo hili.. Natamani viongozi wengine waige mfano huu” Alisikika mwananchi mmoja akizungumza

Mapema akizungumza na mwandishi wetu, Afisa Tarafa huyo alisema lengo la Maonyesho hayo ni pamoja na kuona, kujifunza kwa kuongeza maarifa na mbinu mpya katika mambo mbalimbali hususani Kilimo lakini muhimu zaidi ni kwenda kuyatekeleza hayo katika maeneo yao.

” Nawashukuru viongozi wenzangu hawa kwa kuona umuhimu wa kuambatana nami kuja kujifunza katika maonyesho haya, sio rahisi Wananchi wa Itiso wote kusafiri na kufika hapa, lakini sisi tunapofika hapa ni rahisi kuhamisha kile tunachojifunza katika utekelezaji kwenye maeneo yetu.” Remidius Emmanuel